Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Zitto awatega CCM
Zitto awatega CCM
By Habari Tanzania | Published  07/23/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Peter Nyanje


MAFUNZO yaliyotokana na nia ya kutaka kuwasilisha hoja binafsi iliyotolewa na Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa, (CHADEMA) kuhusiana na tuhuma za ubadhirifu wa Benki Kuu (BoT), yameacha somo kubwa kwa wapinzani.

Mafunzo hayo ndiyo yaliyomfanya Mbunge mwingine wa chama hicho kutoka Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kutumia upenyo tofauti kuhoji uamuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kusaini mkataba na kampuni moja ya madini nje ya nchi.

Baada ya kuibua sakata la tuhuma za ubadhirifu ndani ya BoT, Dk. Slaa alionyesha nia ya kutaka kuwasilisha hoja binafsi, kulitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza tuhuma hizo.

Lakini, hata kabla Dk. Slaa hajawasilisha hoja hiyo, serikali ililidaka suala hilo na kueleza kuwa itafanya uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo na hivyo kumuweka katika wakati mgumu Dk. Slaa kuitetea hoja yake.

Ingawa hakukiri iwapo mlolongo huo wa matukio ndio uliomfanya achukue njia nyingine kuhoji aliyoyafanya Karamagi, Zitto alilithibitishia gazeti hili jana kuwa ametumia kanuni tofauti kuwasilisha hoja yake.

“(Mimi na Dk. Slaa) tumechukua approach mbili tofauti ambazo zote zipo katika kanuni. Mimi siwasilishi hoja binafsi kama alivyofanya Dk. Slaa, mimi nitawasilisha hoja ya kulitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza yaliyofanywa na waziri kuhusiana na mkataba huu wa madini aliousaini nje ya nchi,” alisema Zitto alipozungumza na gazeti hili.

Uchambuzi uliofanywa na gazeti hili kuhusiana na kanuni za Bunge, unaonyesha kuwa utaratibu alioutumia Dk. Slaa unaliruhusu Bunge kujadili hoja yake bungeni.

Akieleza nia yake baada ya kuibua sakata ya tuhuma za BoT, Dk. Slaa alitumia kanuni ya 43(2) inayosema: “Bila kuathiri masharti ya katiba na ya kanuni hizi, waziri au mbunge yeyote mwingine aweza, kwa kutoa hoja, kupendekeza kwamba suala lolote lijadiliwe bungeni; na hoja hiyo itaamuliwa kwa kufuata kanuni hizi.”

Kanuni hii inaruhusu hoja itakayotolewa na mbunge kujadiliwa na wabunge, ikimaanisha pia kuwa na serikali nayo, ambayo inawakilishwa bungeni.

Inaaminika kuwa huo ndio mwanya ambao serikali iliutumia kusema kuwa italichunguza jambo hilo na hivyo kufanya uwezekano wa kuundwa kwa kamati teule ya Bunge, kama ilivyokuwa nia ya Dk. Slaa, kuwa mgumu.

Tofauti na Dk. Slaa, Zitto inaelekea amenuia kuitumia kanuni ya 104 ambayo inatoa ufafanuzi kuhusu uundwaji wa kamati teule na Bunge kwa madhumuni maalumu, kwa hoja mahususi itakayotolewa kwa ajili hiyo na kuafikiwa.

Uchambuzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa kanuni hii haitoi mwanya kwa hoja itakayotolewa kujadiliwa, hivyo serikali haitakuwa na mwanya wa kuidaka hoja ya Zitto kama ilivyofanywa kwa hoja ya Dk. Slaa.

Hata hivyo, mtego uliopo kwenye kanuni hii unaweza kumkwamisha Zitto kwani kwa mujibu wa kanuni, Bunge linaweza kuunda kamati teule iwapo tu wabunge watakubaliana na hoja hiyo baada ya kuhojiwa na Spika.

Inaaminika kuwa kwa kuwa Bunge lina wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kutokana na uzoefu uliopatikana katika kupitisha bajeti za wizara kadhaa sasa, haiyumkiniki kwa wabunge hao wa CCM kukubali hoja ya Zitto ya kutaka kuundwa kwa kamati teule kumchunguza waziri wa serikali inayoongozwa na chama chao.

Hata hivyo, wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema kuwa huo hautakuwa mtihani kwa Zitto bali kwa wabunge wa CCM.

Mhadhiri mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa, alisema kuwa iwapo atafanikiwa kuwasilisha hoja yake kwa kufuata taratibu hizo, Zitto atakuwa ametimiza wajibu wake kama mwakilishi wa wananchi.

“Sasa hapo mtihani utahamia kwa wabunge wote na wao kuonyesha uzalendo wao kwa mali ya nchi yao... iwapo watatokea watakaopinga wananchi wanaweza kuwashangaa kwa sababu inatarajiwa siku zote wabunge wawe watetezi wa wananchi na suala hili la madini limekuwa likilalamikiwa sana na wananchi.

“Hii ni nafasi kwa wabunge kuwaonyesha wapiga kura kuwa wapo pamoja nao... hakuna haja ya kuhofu kuhusu matokeo ya uchunguzi kwani iwapo (wabunge wa CCM) wanaamini kuwa waziri wao hana makosa, wanapaswa kukubali kuundwa kwa tume ili ithibitishe hivyo... wakikataa kila mtu atakuwa na jibu lake,” alisema mhadhiri huyo.

Alipoulizwa iwapo hana hofu ya hoja yake kukataliwa na wabunge wa CCM ambao ndio wengi bungeni, Zitto alisema kuwa hilo halimtii hofu kwani anachofanya yeye ni kutimiza wajibu wake kama mwakilishi wa wananchi.

“Nitafurahi nikifanikiwa kuwasilisha hoja kwani nitakuwa nimetimiza wajibu wangu na iwapo kuna mbunge mwingine atakataa kuunda kamati teule, itabidi ahukumiwe yeye kutokana na sababu zitakamzomfanya awe na msimamo huo,” alisema Zitto.

Akizungumzia hoja anayotarajia kuwasilisha wiki hii, Zitto alisema italenga kulitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza mambo makubwa mawili.

Kwanza, alisema ataomba kamati hiyo ichunguze iwapo mkataba wa mgodi wa Buzwagi, uliosaniwa na Karamagi kwa niaba ya serikali na Kampuni ya Barrick Gold Mine, umezingatia masilahi ya taifa.

Zitto anaijenga hoja hiyo nyuma ya hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati anazindua Bunge Desemba 30, 2005, aliposema kuwa mikataba ya madini haitoi haki kwa taifa na wakati umefika sasa kwa mikataba hiyo kuangaliwa upya.

Ili kutimiza azima hiyo, baadaye Rais Kikwete aliunda timu ya wataalamu ambao waliipitia mikataba na kubaini kuwa ni kweli haikuzingatia masilahi ya taifa.

“Katika mazingira kama hayo tulitarajia kuwa iletwe sheria mpya ya madini bungeni itakayotoa maelekezo ya jinsi mikataba ya madini inavyotakiwa kuwa kwa masilahi ya taifa... hili halijafanyika na waziri ameshasaini mkataba,” aliongeza Zitto.

Hoja nyingine ya Zitto itaegemea kwenye majibu ya Karamagi kuwa kipengele cha kodi ya mapato katika sheria kilishaondolewa wakati wa moja ya mijadala ya bajeti iliyopita.

Akijibu hoja hiyo, Karamagi alisema: “Ni kwamba kipengele hiki cha sheria kililetwa hapa bungeni mwaka 2001 kwenye bajeti kikabadilishwa. Bahati mbaya yeye hakuwepo na mimi vilevile sikuwepo, lakini nilikijua. Lakini katika kubadilisha hicho kipengele yale makampuni tayari ambayo yalikwishaingizwa kwenye mkataba usingeweza kuyafutia.”

Lakini wafuatiliaji wa masuala ya Bunge wanasema kuwa hakuna kumbukumbu kuwa kipengele hicho kilibadishwa kwenye bajeti ya mwaka huo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.