ALIYEKUWA Kaimu Gavana wa Benki Kuu na mwanasheria mashuhuri nchini, Bob Makani, amemshauri Rais Jakaya Kikwete kumfuta kazi Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daud Balali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Makani alisema kuwa, kuwepo ofisini kwa Balali kutazuia uchunguzi wa haki kufanyika dhidi ya tuhuma zinazoikabili BoT na yeye mwenyewe binafsi.
Alisema kuwa kwa kuwa Balali ametamka wazi kuwa hatojiuzulu, inampasa Rais Kikwete kumfuta kazi ili timu itakayochunguza tuhuma hizo iwe wazi na kutoa ripoti sahihi kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Makani alisema Balali anaweza kudhoofisha uchunguzi kwani anao uwezo wa kuwazuia watendaji walio chini yake kuficha nyaraka muhimu na ushahidi, hivyo ni vema uchunguzi ukafanyika bila ya yeye kuwepo madarakani.
Alisema kwamba wakati wa uchunguzi, Balali aitwe ajitetee akiwa tayari ameshajiuzulu.
Makani alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa ukweli kuhusu tuhuma zilizotolewa utajulikana bila kumuathiri Balali na watu wengine.