Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni jana, Waziri Profesa Peter Msolla, alisema bajeti hiyo kimsingi inazingatia umuhimu wa kukuza rasilimali watu kwa ajili ya maendeleo endelevu, kama msingi wa mkakati wa kupiga vita umasikini.
Alisema sambamba na hilo, kiwango cha mikopo kwa ajili ya chakula na malazi kwa ajili ya wanafunzi, kimeongezwa kutoka sh 3,500 hadi 5,000 kwa siku.
Aidha, alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali itadhamini wanafunzi 1,772 wa shahada ya kwanza ya udaktari (MD), kati ya hao 50 ni wa udaktari wa meno (DDS) katika vyuo vikuu vitano vya sayansi ya afya nchini.
Pia watadhamini wanafunzi 90 raia wa Uganda katika utaratibu wa kubadilishana wanafunzi wa shahada ya kwanza katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki.
Kuhusu suala la mikopo kwa ujumla, Profesa Msolla alisema Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, inatarajia kutoa mikopo katika viwango kati ya asilimia 0 na 100, kulingana na uwezo wa kiuchumi wa kila mwombaji katika ada, elimu kwa vitendo na mahitaji maalum ya vitivo.
Alisema katika kuondoa tatizo la uhaba wa watumishi katika bodi hiyo, wataajiri wafanyakazi 33 wa uchambuzi na utoaji mikopo na kuongeza kasi ya kukusanya madeni kutoka kwa waliokopa kuanzia mwaka 1994.
Waziri huyo alisema hadi sasa wadaiwa 113,240 wametambuliwa na kiasi kinachodaiwa ni sh 51,103,685,914 na kiasi kilichokusanywa hadi Juni mwaka huu ni sh 53,616,011.22.
Aidha, alisema wizara itaongeza idadi ya rasilimali watu kwa kuongeza wataalamu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi waliofaulu katika daraja la pili wavulana na wanaochukua masomo ya sayansi.
Kuhusu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), alisema kilianzisha majaribio ya kutumia panya buku kutambua kuwepo kwa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) pamoja na panya hao kuendelea kutumika katika kufichua mabomu.
Alisema matokeo ya awali yameonyesha kuwa, panya buku wana uwezo mkubwa wa kutambua TB kwa kunusa makohozi ya wagonjwa kwa kasi zaidi kuliko binadamu anapotumia hadubini.
Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika kipindi cha mwaka huu wa fedha, wizara itakamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi wa Mlimani City.
Kuhusu Chuo Kikuu cha Dodoma, alisema wizara imetenga nafasi za kazi kwa ajili ya wanataaluma 80 na waendeshaji 134. Pia kimetangaza nafasi za masomo katika fani za elimu, sayansi ya jamii na sayansi za kompyuta.