JINAMIZI la tukio la ujambazi lililotokea katika benki ya NMB, wilayani Mwanga mwishoni mwa wiki iliyopita, limeitikisa miji ya Arusha na Moshi.
Katika tukio hilo la Mwanga, polisi mmoja aliyekuwa katika doria, aliuawa na mwenzake akajeruhiwa, huku kiasi cha fedha kinachokadiriwa kufikia shilingi milioni 234 kikiporwa na majambazi hayo.
Huko Arusha, kundi la majambazi wanaosadikiwa kuhusika katika tukio hilo, jana lilipambana kwa risasi na mabomu ya kutegwa na polisi katika tukio lililochukua muda wa takriban saa saba.
Mapigano hayo makali na ya kwanza ya aina yake kati ya askari polisi na majambazi hayo, yalitokea katika nyumba moja ya ghorofa iliyoko eneo la Njiro katika Jiji la Arusha.
Kuibuka kwa mapigano hayo, kulianza muda mfupi tu majira ya saa 11:00 alfajiri baada ya polisi waliokuwa wamejizatiti kwa silaha nzito na mbwa kuizingira nyumba hiyo ambayo ndimo walimokuwa wamejificha majambazi hao watano waliokuwa na wapenzi wao wa kike wawili.
Hata baada ya kutakiwa kujisalimisha kabla ya mapambano kuanza, majambazi hao wanaosadikiwa kuwa ni raia wa nchi jirani ya Kenya, waliamua kuanza kuwarushia polisi risasi kutokea vyumba vya ghorofani, huku wakiwa wametega mabomu katika sebule.
Kitendo hicho cha majambazi kilifuatiwa na uamuzi wa polisi kuanza kujibu mashambulizi hayo wakitumia silaha mbalimbali, zikiwamo nzito kama LPG, na hali hiyo ikaendelea kwa saa saba zaidi kabla ya wahalifu hao kusalimu amri na kuweka silaha chini.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Blasio Matei aliwataja majambazi hao waliojisalimisha baada ya kuzidiwa nguvu kuwa ni Samwel Gitao Saitoti au Josephat (33), kabila Mkikuyu mkazi wa Ng'ong Nairobi na dereva wa matatu (daladala).
Jambazi mwingine aliyekamatwa ni Peter Michael Kimenya (40), Mkikuyu pia, mkazi wa Thika Nairobi anayeendesha magari makubwa na Samson Falme Chonjo mkazi wa Ngulelo Manispaa ya Arusha, ambaye ni dereva wa kampuni ya utalii ya mjini hapa aliyekamatwa juzi kabla ya tukio hilo la jana.
Kamanda huyo alisema pia kuwa, katika upekuzi uliofanyika katika nyumba hiyo, zilipatikana bunduki mbili aina ya SMG zenye magazine tatu na risasi 85, bastola tano zenye magazini nne na risasi 30.
“Pia sambamba na kukamata silaha hizo, tumekamata dola za Marekani 8,145 na fedha za Tanzania shilingi 978,000, majaketi mawili ya kuzuia risasi zisipenye mwilini ambazo ni za kijeshi na bangi,” alisema.
Habari zaidi zilizopatikana kutoka katika eneo la tukio zilisema kuwa, nyumba hiyo ambayo ilionekana kuharibiwa vibaya kwa risasi, inamilikiwa na mtumishi wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) ambaye jina lake limehifadhiwa.
Kamanda Matei alisema baada ya majambazi hao kujisalimisha, polisi walilazimika kuomba msaada kutoka kwa wataalam wa mabomu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kutegua mabomu yaliyotegwa sebuleni, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi katika nyumba hiyo na maeneo ya jirani.
Hivi sasa polisi wameshaanza kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo wakishirikiana na wenzao wa Kenya ili kubaini mtandao mzima wa ujambazi unaojihusisha na matukio ya uporaji kwa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali.
Kutoka huko Moshi, Jeshi la Polisi linawashilia watu zaidi ya 10 wakiwamo wafanyabiashara wakihusishwa na tukio hilo hilo la uporaji wa tawi la NMB, Mwanga.
Habari za uhakika ambazo zimelifikia Tanzania Daima, zinasema miongoni mwa wanaoshikiliwa ni Mkurugenzi wa Kampuni moja ya Utalii ya Moshi Mjini.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mkurugenzi huyo anashikiliwa na polisi kwenye Kituo Kikuu cha Polisi kilichopo kwenye mji mdogo wa Himo uliopo zaidi ya kilometa 30 kutoka Moshi Mjini.
Chanzo cha kuaminika cha habari kutoka ndani ya polisi kinasema watuhumiwa wengine wametawanywa kwenye vituo mbalimbali vya polisi vilivyopo katika miji ya Bomang'ombe, Same na Rombo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, polisi hao pia wanamshikilia askari polisi anayefanya kazi wilayani Mwanga (Bwawa la Nyumba ya Mungu) akihusishwa kupanga na kufanikisha uporaji huo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (ACP), Lucas Ng'hoboko, jana kwa mara ya pili alikataa kutaja majina ya watuhumiwa wanaoshikiliwa na jeshi hilo hadi sasa.
Kamanda huyo wa polisi alisema jana ofisini kwake kuwa, taarifa rasmi zitatolewa na jeshi hilo mara baada ya kuwatia mbaroni watuhumiwa muhimu ambao jana walizingirwa na jeshi hilo mkoani Arusha.
Katika tukio hilo la uporaji wa NMB, polisi walimuua kwa risasi kichwani, polisi mwenye namba E.6825 PC. Michael na kumjeruhi mwenzake mwenye namba F.6973 PC. Naftari.
Kabla ya uporaji huo, majambazi hao walimteka Meneja wa tawi hilo, Robert Marandu na familia yake pamoja na meneja uendeshaji, Salome Matemu.
Katika tukio hilo, polisi nao walifanikiwa kumuua mmoja wa majambazi hao aliyekuwa ndani ya gari dogo lenye namba za usajili T 979 AMY Toyota Corolla 100 baada ya tukio la kurushiana risasi.
Imeandaliwa na David Frank, Mustafa Leu wa Arusha na Charles Ndagulla, Moshi.