Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Nauli zapanda rasmi
Nauli zapanda rasmi
By Habari Tanzania | Published  07/21/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mkolo Kimenya na Mobini Sarya


MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga, Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) umetangaza rasmi kupanda kwa nauli mpya za usafiri wa mabasi ya masafa marefu na daladala.

Mbali na kukubali ongezeko la nauli kwa wastani wa asilimia 20, SUMATRA pia imeyafungia mabasi manne ya kampuni tofauti kwa kupandisha nauli bila kibali.

Taarifa iliyotolewa jana na SUMATRA inaonyesha kuwa, mabadiliko ya nauli hizo mpya yataanza Jumatano ya wiki ijayo.

Aidha, akitoa tamko hilo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Israel Sekilasa, alisema mabasi ya kampuni za Hood, Abood, Buffalo na Najimunisa, yamefungiwa kwa siku 60, kuanzia Julai 23, mwaka huu kwa kupandisha nauli ya kwenda mikoani bila kibali.

Aidha, SUMATRA katika mabadiliko hayo imesema kuwa nauli ya Dar es Salaam-Tanga inapaswa kutozidi sh 7,500 na Moshi-Arusha isizidi sh 8,000 na kwa Morogoro-Tanga isiwe zaidi ya sh 11,000.

Kwa mabasi yenye hadhi ya kati (Semi-Luxury buses), kiwango cha juu kitakuwa sh 35 kwa abiria kwa kila kilometa na mabasi yenye hadhi ya juu (Luxury Buses) kiwango cha juu cha nauli kitakuwa sh 43 kwa abiria kwa kila kilometa.

Aidha, kila basi linapaswa kuwa na orodha ya abiria wanaosafiri kwa safari na siku husika, ambapo nakala ya orodha hiyo itunzwe katika ofisi ya kampuni ya basi husika.

Baada ya SUMATRA kupitia mapendekezo ya wamiliki wa daladala katika sehemu husika, imeridhia nauli mpya kuongezeka kwa sh 50 badala ya sh 100 kama walivyoomba.

Kwa maana hiyo, akitolea mfano wa nauli za Dar es Salaam, Sekilasa alisema safari ambayo abiria walikuwa wakilipa sh 200, sasa watapaswa kulipa sh 250 na pale walipokuwa wakilipa sh 250, sasa watapaswa kulipa sh 300 na pale ambapo nauli ilikuwa sh 300, sasa hivi itakuwa sh 350.

Alisema kwa safari za pembezoni mwa miji, kuanzia kilometa 20 na kuendelea, nauli itapanda kutoka sh 400 hadi sh 500.

“Kimsingi nauli ya wenye daladala, ongezeko haliwezi kuzidi asilimia 20 kwa hiyo kama nauli inapanda ni sh 50 tu,” alisema Sekilasa.

Mkurugenzi huyo, alisema pia kuwa, kabla ya kukubali ombi la kupandisha nauli, mamlaka ilipata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ambao ni wamiliki wa vyombo vya usafiri na watumiaji wa huduma hiyo.

“Tulipokea mapendekezo ya kupandishwa kwa nauli za daladala katika Jiji la Dar es Salaaam, yalivyowasilishwa na Umoja wa Wamiliki wa Mabasi ya Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA) na Usafiri Dar es Salaam (UDA) kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta,” alisema Sekilasa.

Katika mapendekezo yao DARCOBOA, walitaka askari wa majeshi yote hapa nchini walipe nauli ili kukidhi kiwango cha ongezeko la bei ya mafuta, nauli ya wanafunzi ipande kutoka shilingi 50 hadi sh 100 wakati wakisubiri serikali kutoa tamko la wanafunzi kulipa nauli sawa na mtu mzima.

Aidha, katika mapendekezo yao, pia walitaka ongezeko la nauli la sh 100 kwa kila safari.

Alisema wamiliki wa magari yanayofanya safari za mikoani, walipeleka mapendekezo yao wakitaka nauli ipande na kutoa mfano wa kutoka Tanga –Dar kutoka sh 6,500 hadi sh 8,000 na Tanga –Moshi kutoka sh 7,500 hadi sh 8,500.

Sekilasa alisema baada ya kupokea mapendekezo hayo, walishauriana na kuyachambua mapendekezo hayo kwa kutumia vigezo mbalimbali vikiwamo vya kupanda kwa bei ya mafuta, gharama za uendeshaji, mfumuko wa bei kwa ujumla kwa mujibu wa vifungu namba 6(1) (b) (iv) na 16 (1) vya sheria ya SUMATRA.

“Kuhusu askari wetu kulipa nauli, tumeona si vema kuweka mjadala, kwani tunaheshimu kazi zao na wako kazini kwa saa 24, kwa hiyo si vema wakalipa nauli,” alisema.

Na kwa nauli ya wanafunzi, SUMATRA imesema itabaki kuwa sh 50 hadi utafiti wa matatizo ya usafiri wa wanafunzi katika majiji na miji utakapokamilika.

“Katika kuboresha utekelezaji wa nauli mpya, wamiliki wa mabasi watalazimika kutoa tiketi kwa kila abiria na tiketi hizo lazima zionyeshe jina la mmiliki, namba za usajili wa basi, njia na vituo, nauli na tarehe, ambapo pamoja na hayo kila basi litalazimika kuweka nakala ya jedwali la nauli kwa njia husika katika kila basi,” alisema Sekilasa.

Katika taarifa hiyo, SUMATRA ilisema kwamba, kwa mabasi ya kawaida, imeridhia kiwango cha juu cha nauli kisizidi sh 25 kwa kilometa moja kwa abiria.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.