Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tatizo la wanafunzi Ukraine laibuka bungeni
Tatizo la wanafunzi Ukraine laibuka bungeni
By Marshy Abdu | Published  07/21/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Tatizo la wanafunzi Ukraine laibuka bungeni
na Tamali Vullu na Rahel Chizoza, Dodoma


KAMBI ya upinzani bungeni, imeitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tatizo la wanafunzi zaidi ya 20 wa Kitanzania waliokwama nchini Ukraine kutokana na kushindwa kulipa ada na gharama nyingine za masomo.

Mapendekezo hayo ya kambi ya upinzani, yaliwasilishwa bungeni na Susan Lyimo, wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo wakati wa kuchangia mjadala wa bajeti ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia iliyowasilishwa jana na Waziri Profesa Peter Msolla.

Akisoma maoni hayo, Lyimo ambaye ndiye msemaji mkuu wa wizara hiyo kwa upande wa upinzani, alisema kamati itakayoundwa inapaswa kuwa huru na ambayo itafanya kazi zake kwa uwazi.

Alisema kambi ya upinzani imeipendekeza Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ifanye uchunguzi wa kina na ipewe muda mfupi kuita mashahidi, vielelezo na kuwahoji wahusika wote wa suala hilo.

Lyimo alisema ni vema kamati hiyo itakapokuwa ikifanya kazi, ipewe mamlaka ya kumuita mtu yeyote na kumhoji ili ipate ukweli na ufumbuzi wa tatizo hilo ambalo lipo njia panda.

Alisema serikali kupitia vyombo vya habari, imekuwa ikitoa matamko kwamba wanafunzi waliokimbilia ubalozi wa Uingereza nchini Ukraine, waliondoka nchini bila baraka za serikali.

Msemaji huyo alisema kuwa ingawa matamko hayo ya serikali yamekuwa yakitolewa, pia Kampuni ya Ukraine Education Fund ambayo ndiyo inaratibu shughuli zote za masomo kwa vijana wanaoenda kusoma nje ya nchi, imesisitiza kwamba wanafunzi hao waliondoka baada ya kupata baraka zote za serikali.

“Tusiwaadhibu vijana kwa makosa ya kiutendaji, kama makosa yalifanyika, basi hatua muhimu zichukuliwe dhidi ya wahusika na serikali ihakikishe makosa haya hayarudiwi tena,” alisisitiza.

Kambi hiyo ilihoji iwapo serikali inaweza kuhamasisha na kuchangisha fedha kwa muda mfupi kwa timu ya soka ya taifa kwenda Brazil kwa mazoezi, ni vipi washindwe kuona umuhimu wa elimu kwa vijana hao.

Kuhusu migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, kambi hiyo iliishauri serikali isitumie nguvu katika kutafuta ufumbuzi wakati wanafunzi wakidai haki zao za msingi na badala yake wafanye mashauriano.

Kambi hiyo iliitaka serikali itakapokuwa ikihitimisha bajeti hiyo, ieleze ni hasara kiasi gani imepatikana kutoka na migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu iliyojitokeza hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Sokoine.

Alisema chuo kikuu si shule ya msingi, bali ni taasisi inayotoa elimu ya juu kwa watu wazima, vijana ambao wamefikia umri wa kufikiri mambo yao wenyewe.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, utawala wa chuo kikuu ulikiri kuwa wanafunzi 56 tu kati ya 15,840 katika vyuo vikuu vinne wametuhumiwa kuwa viongozi wa mgomo ambao ulitishia amani na kuleta vurugu.

Kuhusu suala la wanafunzi kuchangia asilimia 40, kambi hiyo ilisema ni jambo gumu na linarudisha nyuma juhudi za serikali za kuongeza namba ya wanafunzi katika elimu ya juu na kuwa chanzo cha migomo na migogoro katika vyuo hivyo.

Alisema sera hiyo ya uchangiaji elimu ni ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa wakati serikali za huko kwao zimejiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeshindwa kusoma chuo kikuu kwa sababu ya kukosa fedha.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.