Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, amewataka viongozi wa CCM Zanzibar, kuvunja ukimya na kuwajibu mapigo wapinzani wanapotoa kauli zisizofaa katika kujenga demokrasia.
Akiwahutubia viongozi wa CCM mikoa na wilaya za Zanzibar katika hoteli ya Bwawani, Rais Kikwete aliwataka wana-CCM hao kama wakirushiwa maneno yasiyofaa, basi nao siku inayofuata waitishe mkutano wa hadhara na kujibu mapigo.
’’Sifa ya kiongozi hodari anatakiwa ajibu mapigo ya wapinzani, ikiwa wamekutukana tarehe 21 katika mkutano wa hadhara, wajibiwe tarehe 22 katika mkutano wa hadhara na sio kuandika taarifa katika karatasi na kugonga muhuri wa siri, hiyo haitasaidia,’’ alisema Rais Kikwete.
Aliwaeleza wana-CCM hao kuwa, wakati umefika kwa Chama cha Mapinduzi kuendeshwa kikomandoo kulingana na mienendo na tabia za wapinzani.
Alisema kazi kubwa hivi sasa katika CCM ni kuhakikisha viongozi wanatangaza sera ipasavyo ili kuongeza wanachama zaidi kutoka kambi ya upinzani.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema, malengo hayo yataweza kufanikiwa iwapo mikutano ya mara kwa mara itafanyika kwa vile ndiyo njia pekee ya kumshawishi mwananchi kukiunga mkono chama.
Alisema maeneo yenye upinzani mkubwa kisiasa ndiyo maeneo muafaka kwa viongozi wa CCM kwenda kufanya kazi ya siasa, ili kuhakikisha ngome za wapinzani zinasambaratishwa na kurejesha nguvu za CCM.
Aliyataja maeneo yanayohitaji kufanyiwa kazi katika kisiwa cha Unguja kuwa Tumbatu, Nungwi, Bububu na Mji Mkongwe ambayo yalitoa upinzani mkubwa wa CCM katika uchaguzi mkuu uliopita.
’’Kama mtaitisha mikutano wananchi watajitokeza na watawasikiliza na msijali hata kama siku ya kwanza atakuja mmoja au wawili, kwani kuna siku nyingine watazoea na kusema waje kusikiliza na hapo ndipo mtawavuta watu wengi kujiunga na CCM,’’ alisema Rais Kikwete.
Alisema suala la kuimarisha umoja ndani ya chama hicho ndio msingi pekee unaohitaji kuendelezwa katika kukipigania chama hicho kuwa imara zaidi.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema hakuna sababu ya kiongozi kuwa muoga kwani atakuwa hawezi kukitetea na kukipigania chama hicho.
Kuhusu hali ya uchumi wa Zanzibar, alisema serikali zote mbili zimeanza kuangalia ni maeneo gani ambayo yanaweza kuimarishwa kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi wake.
Alisema serikali ya Muungano inaangalia uwezekano wa Zanzibar kulitumia zaidi soko la Tanzania Bara kwa bidhaa ambazo zitazalishwa ndani ya Zanzibar.
Rais Kikwete alisema katika mpango huo, serikali itaangalia mkakati wa kushawishi watu kuwekeza viwanda vya ndani na kuondoa utamaduni wa kutegemea bidhaa kutoka nje ya Zanzibar.
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa mpya wa CCM, Bw. Yussuf Makamba, aliwataka viongozi wa CUF kuacha kumlinganisha Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete na Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba.
’’Rais Kikwete anasimamia serikali na kufanya hivyo ni sawa na kulinganisha kichuguu na mlima Kilimanjaro,’’ alisema Bw. Makamba.
Alisema atahakikisha anafanyaa kazi kubwa ya kuitangaza Ilani ya CCM na kuwataka wapinzani kuacha kufanya siasa za kibabe na kujigamba kuwa na yeye mwenyewe ni mbabe.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Rais Amani Abeid Karume na viongozi mbali mbali wa CCM Zanzibar.