Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mwinyi: Kosoeni viongozi
Mwinyi: Kosoeni viongozi
By Habari Tanzania | Published  07/20/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


WAKATI baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakionyesha kutokuwa wavumilivu kutokana na ukosoaji unaofanywa na vyombo vya habari, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili ameibuka na msimamo tofauti na huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili (1985-1995), Ali Hassan Mwinyi, amewataka waandishi wa habari kuandika habari za kuikosoa serikali na viongozi wake.

Mwinyi alitoa kauli hiyo nzito juzi katika hafla ya kutimiza mwaka mmoja wa gazeti la kila wiki la Kiswahili ‘Changamoto’ iliyofanyika katika Hoteli ya New Africa.

Kiongozi huyo mstaafu, pasipo kutoa mfano wa gazeti au kiongozi yeyote, alisema kuwa waandishi wana dhima ya kuikosoa serikali na viongozi wake kwa sababu imejengeka tabia ya hatari miongoni mwa viongozi hao.

Pasipo kuumauma maneno, Mwinyi alisema kuwa baadhi ya viongozi wa serikali, wakati mwingine wamekuwa wakijisahau katika utendaji wao, hivyo kukosolewa kupitia vyombo vya habari kutasaidia kuwaamsha.

Aidha, Mwinyi, kiongozi pekee nchini aliyejipatia umaarufu mkubwa kutokana na sera zake za kufungua mipaka, alisema kuwa magazeti, ni moja ya njia madhubuti zinazoweza kutumika kukuza demokrasia nchini na sehemu nyingine duniani.

Alisema kuwa watu wengi hupata habari za mambo yanayotokea kupitia magazeti, hivyo magazeti hayo na waandishi wake wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa wanawapatia habari wananchi wenye kiu ya ufahamu.

Mwinyi ambaye wakati wa urais wake ndiye aliyetoa uhuru ulioanzisha mfumo wa vyama vingi na ule wa kuanza kwa vyombo binafsi vya habari, alisema kuwa waandishi wanapofanya kazi zao, wamekuwa wakileta changamoto kwa viongozi makini ambao hufuatilia yale yaliyoandikwa kwa lengo la kutafuta ufumbuzi.

Mbali ya hayo, kiongozi huyo ambaye wakati wa utawala wake alionyesha uvumilivu mkubwa dhidi ya habari mbaya za kweli na zisizo za kweli, zilizokuwa zikielekezwa kwa serikali yake, yeye binafsi na wakati mwingine familia yake, alibainisha kuwa, wakati mwingine, mambo yanayoandikwa katika vyombo vya habari huwasaidia viongozi kufanya ufuatiliaji.

Kutokana na hali hiyo, Rais Mwinyi alitoa wito kwa Watanzania wote, na hasa viongozi, kuwa na tabia ya kusoma magazeti ili kupata taarifa za masuala ambayo yanatokea sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo ya rais amstaafu inakuja wakati serikali imeingia katika mgogoro na baadhi ya magazeti kwa kuamini kuwa yanayoandikwa yana lengo baya.

Aidha, kauli hiyo inakuja wakati harakati za kutunga sheria mpya ya uhuru wa vyombo vya habari zikiwa zimepoa kufuatia malumbano ya hoja yaliyotokea mapema mwaka huu, huku pande kadhaa zikipingana kuhusiana na maudhui ya sheria hiyo ambayo inatarajiwa kufikishwa bungeni baadaye mwaka huu.

Watu wanaounga mkono muswada huo wamekuwa wakisema kuwa utasaidia kuvifanya vyombo vya habari na waandishi wa habari kuwa waadilifu kutokana na masharti yatakayowekwa, na hivyo kutoupotosha umma katika kazi ya uandishi wa habari.

Aidha, kwa upande mwingine, wanaopinga masharti hayo katika sheria, wanadai kuwa vyombo vya habari vinatakiwa kuachwa huru, ili kuweza kuripoti kwa undani kile kinachotokea katika jamii na serikalini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ladyband, inayochapisha gazeti la Changamoto, Jamilla Abdallah, alisema kuwa, licha ya kuchapisha gazeti, kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono sera za ajira zinazotekelezwa na serikali.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uhai wake, kampuni hiyo imefanikisha wanawake wajane wapatao 74 kupata mafunzo ya ujasiriamali yaliyoendeshwa na wataalamu kutoka Chuo cha Biashara cha Dar es Salaam.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.