SERIKALI imemtaka mhariri wa gazeti la MwanaHALISI kutoa maelezo kwa nini gazeti hilo lisichukuliwe hatua kutokana na habari iliyochapishwa katika toleo lake la jana ambayo serikali imeifananisha na “lugha ya matusi na kebehi kwa viongozi wakuu wa taifa.”
Katika barua yake ya jana kwa Mhariri Mkuu wa gazeti hilo, yenye kumbukumbu Na. ISC/N.100/1/VOL. IV/140, serikali imemtaka mhariri mkuu “kujitetea kwa nini asichuchukuliwe hatua” kabla ya saa tisa alasiri jana.
“Tumeipokea. Tumewajibu kwamba wahusika wakuu hawapo. Tumeelekezwa na mhariri mkuu kuwajibu kuwa barua ya utetezi itawasilishwa kabla ya saa tisa alasiri kesho (leo),” alieleza Meneja Utawala wa kampuni inayochapisha gazeti hilo, Yusuf Aboud.
Barua ya serikali iliyosainiwa na Msajili wa Magazeti ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Kassim Mpenda, inatuhumu gazeti kwa kuandika habari ambazo zinachochea chuki miongoni mwa Watanzania dhidi ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Mpenda anasema katika barua hiyo kwamba MwanaHALISI toleo la jana liliandika habari ya uchochezi na ambayo inamkashifu Rais Kikwete kwamba “Miguu ya rais imeota malengelenge.”
“Unatakiwa kujitetea kwa nini usichukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976. Utetezi wako umfikie Msajili wa Magazeti kabla ya saa 9:00 alasiri leo Julai 18, 2007,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Aidha, gazeti hilo lilichapisha katika ukurasa wake wa kwanza habari ya mahojiano na mwanasiasa mashuhuri na wakili mahiri, Mabere Marando, ambaye amenukuliwa akisema kuwa wananchi wanaweza “kuipindua serikali kwa kutumia njia halali ya kupiga kura.”
“Wewe unatumia lugha ya kupindua. Kwa lugha ya kawaida, kupindua ni kutumia nguvu za kijeshi. Lakini yapo mapinduzi mengine yanayowezekana. Ni yale yanayotokana na mwamko wa wananchi,” gazeti lilimnukuu Marando akisema.
Aidha, kwenye kurasa za nane na tisa, gazeti hilo lilichapisha makala yenye kichwa cha habari kisemacho, “Miguu ya rais imeota malengelenge.”
Katika makala hiyo, mwandishi anaonyesha jinsi ambavyo serikali haijaweka wazi vipaumbele vyake na kwamba Rais Jakaya Kikwete amekuwa mpole, asiye na kishindo na kwamba kashfa za wateule wake ndizo zinamchelewesha kuchukua hatua.