KATIKA tukio la nadra, mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere, jana alikanusha madai ya mmoja wa watoto wake, kuhusu kukerwa na uamuzi wa kubomolewa kwa nyumba ya Magomeni, jijini Dar es Salaam, aliyopata kuishi na mumewe zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Mama Maria aliyekuwa ameambatana na mwanaye, Makongoro na kusoma tamko rasmi la familia hiyo, nyumbani kwake Msasani, walikanusha madai yaliyokuwa yakiwahusisha wao na mipango ya kuandaa maandamano yenye lengo la kupinga ubomoaji huo.
Katika tamko la jana ambalo kimsingi linakinzana na lile lililopata kutolewa na Madaraka Nyerere, mtoto mwingine wa Baba wa Taifa, familia hiyo ya Mwalimu ilisema nyumba hiyo aliyoishi kiongozi huyo haikuwa yake, bali ya serikali na kwamba wao walikuwa ni wapangaji.
Aidha, familia hiyo katika tamko lake hilo ilisema pia kwamba, baada ya kuhama katika nyumba hiyo ya serikali, Mwalimu alihamia kwenye nyumba yake yeye mwenyewe ambayo hata hivyo alikuja kuiuza kwa rafiki yake, Balozi Tibandebage.
“Hivyo familia haina umiliki, wala madai ya aina yoyote kwa nyumba zote mbili za Magomeni, ikiwamo ile ya Magomeni Maduka Sita ambayo imekuwa chanzo cha mjadala,” linasomekana tamko rasmi la maandishi lililotolewa na familia hiyo jana na kusomwa na Makongoro.
Akieleza historia ya nyumba alizowahi kuishi Mwalimu wakati wa uhai wake, kwa niaba ya familia, Makongoro aliyepata kuwa mbunge wa Arusha kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi kabla ya kurejea CCM, alisema wao hawana mamlaka juu ya nyumba hiyo na kwamba hakuna maandamano wala mazungumzo yatakayofanyika kifamilia kwa ajili ya nyumba ile.
“Huu ni mjadala ambao sipendi uitwe wa kifamilia, ni mjadala wa wote, nami nasema kwamba ile nyumba Mwalimu alikuwa mpangaji, hivyo hatuna mamlaka juu ya ukodishwaji au uvunjwaji wake.
“Ila kwa sababu Mwalimu alikuwa wa Watanzania wote, basi mimi naheshimu wadau, nawaomba watafute ufumbuzi wa mjadala huu kwa mazungumzo ya amani na si kuandamana.
“Mwalimu angekuwa hai angehuzunika sana kusikia familia yake inaandamana kwa ajili ya kuzuia shughuli za serikali kwenye nyumba aliyokuwa mpangaji… napenda kusema tena kwamba, familia haina mpango wa kufanya maandamano,” alisisitiza Mama Maria wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Kauli ya sasa ya familia inakuja siku chache tu baada ya mtoto mwingine wa Mwalimu, Madaraka, kuzungumzia suala la nyumba hiyo na kusema kuwa, alikuwa haoni sababu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuchukua uamuzi huo alioutafsiri kama uharibifu na upotevu wa kumbukumbu muhimu za taifa.
“Kwa niaba ya familia ya Mwalimu… naiomba serikali isitishe uamuzi huo, tumesikia kuwa nyumba ile inataka kubomelewa, sisi hatutaki. Tunataka iachwe kama ilivyo kwa nia ya kuihifadhi.
“Hakuna sababu ya kubomoa, swali jingine la kujiuliza, kama wanataka kujenga, nchi hii ina kilometa za mraba zaidi ya 900,000, hivi wamekosa kweli sehemu ya kujenga ila kubomoa nyumba ya kumbukumbu?
“Sisi wana familia hatutaki kabisa kunanihii… hiyo nyumba ibaki kama kumbukumbu ya Mwalimu kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisema Makongoro, katika tamko ambalo sasa linaweza linaanza kuchukuliwa kuwa ni msimamo wake binafsi.
Kwa mujibu wa sheria ya Jamhuri namba 10 ya mwaka 1964 na marekebisho yake namba 22 ya mwaka 1979, maeneo ya kumbukumbu hukabidhiwa Idara ya Mambo ya Kale chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dhumuni la sheria hiyo ni kuhifadhi, kuenzi na kutunza maeneo na vitu muhimu vya wanasiasa, viongozi maarufu wenye mchango katika ustawi na maendeleo ya taifa.
Septemba 22 mwaka jana, serikali ilitoa tangazo namba 135 likionyesha kuwa, majengo na maeneo 193 ya kumbukumbu nchi nzima yatahifadhiwa na kulindwa kwa mujibu wa sheria.
Ndani ya kipindi cha miezi sita baada ya tangazo la serikali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe, alitoa tangazo jingine namba 51 la Machi 2, mwaka huu linaloonyesha kufutwa kwa tangazo la awali.
Hivyo basi, tangazo lililotolewa na Waziri Maghembe liliidhinisha kubomolewa kwa majengo ya kale yenye kumbukumbu muhimu, hali inayopingwa na wahifadhi wa mambo ya kale kwa kile wanachodai kuwa, ni kupoteza historia ya nchi kwa vizazi vijavyo.
Habari za familia ya Nyerere kuandaa maandamano, ziliibuka baada ya NHC, kuwataka wapangaji wa nyumba hiyo kupisha ujenzi wa ghorofa la kisasa kwa ajili ya biashara.