Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kabwe ambana Karamagi
Kabwe ambana Karamagi
By Habari Tanzania | Published  07/18/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Tamali Vullu, Dodoma


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amelitaka Bunge kuunda kamati ya kuchunguza uamuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, wa kusaini mkataba wa madini nje ya nchi.

Kabwe, mbunge mdogo kuliko wote wa kuchaguliwa, alitoa rai hiyo juzi jioni muda mfupi baada ya Bunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo.

Kikubwa kilichomfanya mbunge huyo afikie uamuzi huo wa kutaka kuchunguzwa kwa Karamagi, ni majibu ya waziri huyo kuhusu uamuzi wake wa kusaini mkataba wa madini kati ya serikali na kampuni ya madini ya Barrick nje ya nchi.

Kabwe aliielezea hatua hiyo ya Karamagi kuwa inayokwenda kinyume na maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete ya kutosainiwa kwa mkataba wowote mpya kabla ya kazi ya kuhakiki mikataba ya zamani haijakamilishwa na ripoti kuwasilishwa na kamati maalum.

Aidha, mbali ya hilo, Kabwe mmoja wa wabunge machachari wa upinzani, aliliambia Bunge kuhusu kutoridhishwa kwake na majibu ya waziri huyo, juu ya uamuzi wake wa kusaini mkataba huo wa madini, London, Uingereza badala ya Dar es Salaam.

Aidha, Kabwe alisema kuwa, sababu alizozitoa Karamagi kuhalalisha kuusaini mkataba huo nje ya nchi, bado hazijitoshelezi, hivyo upo umuhimu mkubwa wa suala hilo kuchunguzwa kwa kina na Bunge kama chombo huru kinachoisimamia serikali.

“Majibu kuhusu mkataba huo si sahihi. Waziri amedanganya katika majibu yake, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu, kwamba nitawasilisha hoja ya kimaandishi kutaka hoja hiyo iundiwe kamati teule ya kuchunguza,” alisema mbunge huyo.

Akichangia bajeti ya wizara hiyo juzi, Kabwe alimtaka Waziri Karamagi aeleze ni kwa nini aliamua kusaini mkataba mpya na Kampuni ya Barrick wakati akijua kuwa serikali ilikuwa katika mchakato wa kupitia mikataba yote ya madini nchini.

Akijibu hoja hizo, Karamagi alikiri kusaini mkataba huo huko London, akisema alifanya hivyo kwa nia njema, akirejea historia yake ya kutokea katika sekta binafsi ambayo inamfanya aone suala la muda kuwa ni jambo muhimu.

Hata hivyo, alisema wakati akisaini mkataba huo, tayari ulikuwa umeshapitiwa na kuhakikiwa na timu ya wataalamu wa wizara yake, Mwanasheria Mkuu na Kamati ya Ushauri wa Madini kama taratibu zinavyotaka.

Kabwe ni mbunge wa pili kutoka kambi ya upinzani kuonyesha nia ya kuwasilisha hoja ya kulitaka Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza jambo fulani.

Nia kama hiyo ilishatangazwa na Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), ambaye naye alilitaka Bunge liunde kamati kuchunguza tuhuma dhidi ya ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Dk. Slaa yeye alifikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa serikali kuamua kuunda kamati ya kuichunguza BoT, akisema Bunge kama chombo huru chenye kusimamia serikali, lilikuwa na wajibu wa kuunda kamati yake.

Licha ya serikali kueleza kuwa ilikuwa imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kushirikiana na kampuni za ukaguzi za kimataifa kuchunguza tuhuma za ubadhirifu kupitia akaunti ya madeni ya nje, Dk. Slaa aliendelea na msimamo wake wa kutaka kuundwa kwa kamati hiyo teule.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.