MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, jana aliondoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kifua mbele baada ya mahakama hiyo kufuta mashitaka dhidi yake.
Pamoja na mambo mengine, wanachama kadhaa wa chama hicho, walifungua kesi wakiitaka mahakama ibatilishe maamuzi yaliyofikiwa katika moja ya vikao vya chama hicho pamoja na kufunga akaunti ya chama.
Wanachama waliokuwa wamefungua mashitaka hayo ni pamoja na aliyekuwa Katibu wa chama hicho, Hamad Tao, Pepetua Morio, Julieth Banigwa, Ester Kapama, Salama Juma, Abbas Salum, Leonsia Nyawale, Matrida Magesa na Waziri Semkiwa.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Adolf Mahay, alitupilia mbali maombi ya wanachama hao kwa maelezo kuwa, walishindwa kutoa sababu za kuishawishi mahakama.
Alisema kuwa, pamoja na kufungua mashitaka hayo, wanachama hao walishindwa sababu ya msingi ya kutaka kufungwa kwa akaunti ya chama yenye namba 030273300 tawi la Azikiwe, jijini Dar es Salaam.
Mahay alisema inashangaza kuwa wakati chama kina wanachama wengi, wanaolalamika ni wanane tu.
Mbali na madai ya kutaka kufungwa kwa akaunti ya chama, wanachama hao pia walifungua madai ya kutaka kufutwa kwa maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika Aprili 3 mwaka huu, ambao uliwaondoa madarakani wengi wa walalamikaji hao.
Akizungumzia hilo, hakimu Mahay alisema kuwa, hana sababu ya kufuta mkutano huo kwa kuwa wanachama hao hawajawasilisha sababu ya msingi na kutoa hoja mkutano huo uliwaathiri vipi.
“Mkutano uliofanyika Aprili ulikuwa wa halali kutokana na idadi ya wanachama walioshitaki hawafikii hata nusu ya wanachama wa chama hicho na pia hawajaelezea umewaathiri vipi na kwa kuwa gharama zilizotumika katika mkutano huo kuwa ni kubwa hivyo kufuta maamuzi yake kutaathiri chama,” alisema Mahay.
Baada ya kutolewa kwa maamuzi hayo, Mrema alifungua kesi ya madai, akiwataka Tao na wenzake wamlipe fidia ya sh milioni 100 kutokana na kumdhalilisha kwa kumwambia kuwa anafuja mali za chama na nyumba anayoishi amenunulia fedha za chama.
Kesi ya Mrema kudai fidia hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Julai 26, mwaka huu.