SERIKALI imesema kuwa inatambua umuhimu wa kuzigawanya wilaya kiutawala lakini imekuwa ikishindwa kutekeleza zoezi hilo kutoka na ghama kubwa ambazo huhitajika katika kuanzisha wilaya mpya.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani, aliliambia Bunge jana kuwa ili kuanzisha wilaya mpya jumla ya sh bilioni 4.5 zinahitajika kwa ajili ya kuyajenga makao makuu ya wilaya.
Alisema fedha hizo hutumika katika kujenga makao makuu ya wilaya, kujenga miundombinu muhimu katika wilaya mpya, gharama za uendeshaji na watumishi wa wilaya husika.
Alisema serikali itakapopata fedha katika bajeti yake itazigawa wilaya zote zinazohitaji kugawanywa kwa kutoa kipaumbele kwa wilaya ambazo ziliwasilisha maombi yao awali na wilaya zenye mahitaji makubwa ya kugawanywa.
Kuhusu kuigawa Wilaya ya Moshi, alisema kikao cha madiwani wa halmashauri hiyo kilikaa na kuridhia kuigawa wilaya hiyo lakini maombi hayo bado hayajawasilishwa kwenye kikao cha ushauri cha Mkoa wa Kilimanjaro.
Alimshauri Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), kuwasilisha suala hilo la kuigawa wilaya katika halmashauri yake ili maombi yapitishwe katika vikao halali na baadaye yawasilishwe kwa waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Alisema kutokana na idadi ya watu katika wilaya hiyo inakidhi vigezo vya kuigawa ambapo alitaja vigezo vinavyotumika katika kugawa wilaya kuwa ni ukubwa wa eneo kilometa za mraba zisizopungua 5,000, kata 15, vijiji 50, idadi ya watu 100,000 na eneo lenye jiografia inayozuia wananchi kupata huduma za kijamii kwa urahisi.