MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), jana alikuwa mwiba mkali kwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.
Ukali wa Kabwe, mbunge kijana na mdogo kuliko wabunge wote wa kuchaguliwa, ulikuja wakati alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza kwa kujiamini, Kabwe alieleza kushangazwa na uamuzi wa Waziri Karamagi kusaini mkataba wa madini kati ya serikali na Kampuni maarufu ya madini hapa nchini, Barrick Gold Mine kwa ajili ya mgodi ya Buzwagi, London, nchini Uingereza badala ya Dar es Salaam.
Mbali ya kuhoji uhalali wa Waziri Karamagi kusaini mkataba huo, kinyume cha maelekezo ya Rais Kikwete ambaye aliagiza kupitiwa upya kwa mikataba yote mipya ya madini, Kabwe alikielezea kitendo hicho kuwa kinachoweza kuongeza wasiwasi wa kuwapo kwa ushawishi wa rushwa.
Kabwe alilieleza Bunge kwamba, hivi karibuni, Waziri Karamagi, alisaini mkataba mpya wa madini na Kampuni ya Barrick Gold Mine kwa ajili ya mgodi wa Buzwagi, kitu ambacho ni kinyume na maagizo ya Rais Jakaya Kikwete.
“Cha kusikitisha mwaka huu, Waziri Karamagi, amesaini mkataba mpya wa uchimbaji madini huko Buzwagi. Hii ni kinyume na maagizo ya Rais, kwani mikataba ya zamani bado inapitiwa upya na kamati iliyoundwa kupitia mikataba hiyo bado haijamaliza kazi yake.
“Tunataka tuelezwe mkataba huo umesainiwa kwa masilahi ya nani wakati mikataba ya zamani bado inafanyiwa marejeo? Na kwa nini mkataba huo usainiwe London na si Dar es Salaam ama sehemu yoyote nchini? Vitu kama hivi ni vyanzo vya rushwa. Tunataka tuelezwe ili tufahamu kinachoendelea,” alisema mbunge huyo.
Kabwe pia alihoji serikali kufuta kipengele cha asilimia 15 cha Kodi ya Mapato katika Sheria ya Mamlaka ya Kodi ya Mapato, bila kupata idhini ya Bunge.
“Mimi sina tatizo la kuondolewa kwa kipengele hicho kwa lengo la kuongeza mapato ya serikali, tatizo langu ni heshima ya Bunge iko wapi? Namtaka waziri atoe maelezo kwa taratibu zipi serikali imeondoa kipengele hicho?” alihoji Zitto.
Alisema waziri huyo pia anatakiwa kutoa maelezo kwa kamati ya Bunge kwa nini anaingilia uhuru wa Bunge kwa kuondoa kipengele hicho bila ya kupata idhini ya Bunge.
Mbunge huyo machachari, alihoji serikali kuuza hisa zake asilimia 15 kwa bei ya kutupa kwa Kampuni ya Barrick Gold Mine.
“Hisa hizo zilikuwa na thamani ya sh trilioni 1.1 lakini serikali imeziuza kwa Kampuni ya Barrick kwa dola milioni tano. Hivi tunakwenda wapi? Nataka nipatiwe maelezo kwa nini serikali iliuza hisa zile na itazirejesha vipi.
“Sekta ya madini ni sekta nyeti, na nchi yetu ina rasilimali kubwa ambayo tungeweza kuitumia kwa uangalifu tungekuwa mbali,” alisema Kabwe.
Alisema Kampuni ya Barrick inamiliki migodi minne nchini na kuhoji tusipokuwa makini nchi itajikuta inatawaliwa na kampuni moja kwa asilimia 100 na matokeo yake nchi kubaki na mashimo.
Alisema dhahabu zilizopo katika migodi hiyo inayomilikiwa na Barrick ina uwezo wa kupata dhahabu kwa miaka 18 ijayo, hivyo tusipokuwa makini baada ya miaka hiyo nchi itakuwa haijafaidika lolote na matokeo yake kubaki na mashimo.
Mbali ya hilo, Kabwe alieleza kushangazwa na takwimu za kukua kwa sekta ya nishati ya umeme zilizowasilishwa na Karamagi wakati akiwasilisha bajeti yake hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kabwe alisema hoja ya waziri kwamba sekta hiyo ilikua kwa asilimia 3.3 mwaka 206 ikilinganishwa na asilimia 5.1 mwaka 2005 si sahihi kwani Taarifa ya Hali ya Uchumi inaonyesha kwamba sekta hiyo ilikuwa kwa kiwango cha asilimia -2.5.
Akijibu hoja za mbunge huyo jana jioni, Waziri Karamagi kwanza alikiri kusaini mkataba na Barrick huko London akisema alifanya hivyo kwa nia njema akirejea historia yake ya kutokea katika sekta binafsi inayoeleza kwamba, kibiashara muda ni jambo muhimu.
Hata hivyo alisema wakati akisaini mkataba huo, tayari ulikuwa umeshapitiwa na kuhakikiwa na timu ya wataalamu wa wizara yake, Mwanasheria Mkuu na Kamati ya Ushauri wa Madini kama taratibu zinavyotaka.
Aidha, Karamagi alikiri kuwapo kwa kasoro katika takwimu alizowasilisha bungeni kuhusu kukua kwa sekta ya nishati ya umeme na akamshukuru Kabwe kwa kulibaini hilo na akaahidi marekebisho hayo kufanyika.
Pamoja na hayo, Waziri Karamagi alisema Kampuni ya Barrick Gold Mine ina migodi mitatu na si minne kama alivyoeleza Mbunge Kabwe.
Naye Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), alisema wachimbaji wadogowadogo nchini ndio wavumbuzi wa madini, lakini ikishabainika hivyo serikali huwaondoa na kuwaweka wachimbaji wakubwa.
“Wachimbaji wadogo ambao mara nyingi ndio wavumbuzi, serikali huwaondoa na kuwaacha yatima pamoja na kuwalipa fidia ndogo. Wachimbaji hao wanatakiwa kupatiwa nyenzo ili waweze kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye wawe wachimbaji wakubwa. Naomba serikali iwaangalie kwani hawa ni rasilimali watu,” alisema Selelii.
Alisema kutokana na hali hiyo, wachimbaji wakubwa wakubwa wanajiona ndio wenye amri na ndio wenye mchi. “Serikali imejiondoa mno katika kuwakaba wachimbaji hawa na ndiyo maana tunaendelea kupata mapato madogo kwenye sekta ya madini. Tunawaachia kila kitu wao,” alisema.
Mbungwe wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM), alishauri serikali kuwapa nafasi Watanzania, ili nao waweze kumiliki kwenye migodi, kwani hiyo itaweza kupunguza malalamiko yaliyopo kuhusu sekta ya madini.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mhonga Said (CHADEMA), aliishauri TPDC iwe chombo cha kuleta mafuta nchini, ili serikali iweze kupanga na kudhibiti bei ya mafuta.
Alisema kutokana na kuwapo kwa ongezeko la mafuta amekuwa akipata ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa wananchi mbalimbali ambao unawataka wabunge wa CCM kuacha kulalamika kupanda kwa bei ya mafuta na kuhoji kuwa walikuwa wapi kuishauri serikali.