ATHARI za kupanda kwa kodi katika bajeti iliyotangazwa hivi karibuni na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, sasa zimeanza kuwaumiza Watanzania licha ya kauli za kila mara zinazotolewa na serikali za kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili kwa siku kadhaa jijini Dar es Salaam umeonyesha kuwa bei ya mafuta, bidhaa za vyakula pamoja na vifaa za ujenzi ndizo zinazopanda bei kila kukicha.
Uchunguzi huo umeonyesha kuwa, bei ya mafuta katika vituo kadhaa vya jijini bado iko juu licha ya Waziri Meghji kuiamuru Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) kuhakikisha kuwa bei haipandi kiasi cha kuwaumiza watumiaji.
Kituo cha mafuta cha Bonjour kilichopo Kinondoni Morocco, bei ya mafuta ya Petroli kwa wiki nzima sasa ni sh 1,495 kwa lita moja na kwa mafuta ya dizeli ni sh 1,407 kwa lita.
Katika kituo cha mafuta cha Hass kilicho eneo la Victoria, dizeli imekuwa ikiuzwa kwa sh 1,400 kwa lita, na sh 1,480 kwa lita ya petroli.
Kituo cha Oil Com cha Mbezi Tangi bovu, dizeli inauzwa sh 1,400 kwa lita na petroli sh 1,480 kwa lita, katika kituo cha BP Mwenge bei ya dizeli ni sh 1,480 na petroli ni sh 1,495 kwa lita, na katika kituo cha ORXY cha Posta Mpya, dizeli ni sh 1,420 na petroli sh 1,500 kwa lita moja.
Uchunguzi zaidi uliofanywa na gazeti hili, umeonyesha kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kumesababisha mfumko wa bei za bidhaa na vyakula, nauli na hata bidhaa nyingine kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Bidhaa za chakula zilizopanda bei kwa zaidi ya wiki moja sasa katika sehemu mbalimbali za jijini ni pamoja na mikate ambayo awali ilikuwa ikiuzwa sh 500, lakini sasa inauzwa sh 550.
Sukari nayo imepanda bei katika sehemu kadhaa za jijini hadi kufikia sh 1,400 badala ya sh 1,000 iliyokuwa ikiuzwa awali.
Katika maeneo kadhaa ya Kinondoni, Kipawa, Kimara na Mburahati, kilo moja ya mchele inauzwa sh 1,300 badala ya sh 800 za awali, na bei ya kilo moja ya unga wa sembe imepanda kutoka sh 400 hadi sh 500.
Nishati ya mkaa imepanda kutoka sh 25,000 kwa gunia hadi sh sh 30,000.
Bidhaa nyingine iliyoathirika na upandaji wa bei za mafuta ni pamoja na simenti ambayo awali ilikuwa ikiuzwa sh 8,000 kwa mfuko wa kilo 50, lakini sasa inauzwa sh 12,000 hadi 13,000.
Wakati bidhaa hizo zikizidi kupaa, gharama za nauli za usafiri wa mabasi yanayofanya safari za kwenda mikoani na yale yanayosafirisha abiria jijini hapa nazo zimekuwa hazina kiwango naalumu kwa sasa.
Uchunguzi uliofanywa katika Stendi Kuu ya mabasi Ubungo umeonyesha kuwa baadhi ya mabasi yanayosafiri kati ya Dar na Mbeya sasa zinagota sh 25,000 badala ya sh 20,000 za awali, na nauli za daladala katika sehemu kadhaa za jijini zimepanda kwa sh 50.
Mapema wiki hii, EWURA, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilitoa tamko la pamoja kuwa akiba ya mafuta iliyokuwepo hadi Juni 30, 2007 inatosheleza mahitaji ya taifa kwa siku zisizopungua 15 kuanzia Julai mosi, 2007 ikiwa imefanyiwa tathmini ya kodi na TRA.
Tamko hilo lilieleza kuwa kwa kuzingatia ongezeko la kodi la sh 124 kwa lita kwa mafuta ya petroli na sh 122 kwa lita kwa mafuta ya dizeli, Serikali haikutarajia wamiliki wa vituo vya mafuta kupandisha bei ya bidhaa hiyo hadi kufikia kiasi cha sh 1,400 kwa lita ya mafuta ya petroli na sh 1,365 kwa lita kwa dizeli.