MWENYEKITI wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameahidi kumsomesha hadi ngazi ya chuo kikuu, Rwechuhura Gozbert.
Mtoto huyo alipata ahadi hiyo baada ya kumhoji Mbowe kwa nini safari hii hakuja na helikopta katika mkutano.
Mbowe alikuwa wilayani humo hivi karibuni, akiwa ameongozana na viongozi wenzake wa vyama vya upinzani katika ziara ya kuichambua bajeti ya mwaka 2007/08.
Kwa mujibu wa maelezo ya kijana huyo, alimuona Mbowe akiwa na helikopta wakati alipofika kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na alitarajia kuwa na safari hii angekuja nayo.
Kijana huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minane, alimkimbilia Mbowe mara baada ya kiongozi huyo kushuka kwenye gari akiongozana na viongozi wenzake kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa hadhara uliokuwa umeandaliwa na umoja wa vyama vya siasa.
Alipomfikia, alimshika mkono na kisha kumsalimia na kumuuliza kuwa helikopta iko wapi? Hata hivyo, Mbowe hakumjibu swali hilo ingawa alimnyanyua na kumbeba mpaka kwenye meza kuu walipoketi.
Ilipofika zamu yake ya kuhutubia, Mbowe alipanda na mtoto huyo jukwaani na kuuambia umati uliokuwepo katika viwanja vya Polisi mjini Kamachumu kuwa, hawezi kuhutubia chochote kwani yule mtoto alikuwa amekamilisha hotuba yake.
Akiwa jukwaani alimuuliza yule mtoto kuwa wazazi wake wako wapi, na akiwa amevalia nguo zilizochakaa, lakini akionekana mchangamfu, alimwambia kuwa baba yake alikuwa anatengeneza pombe na mama yake alikuwa anapika chakula.
“Ndugu wana wa Muleba, siwezi kuhutubia chochote leo, kwani hotuba yangu imebebwa na huyu mtoto, masikini, mtoto mdogo bado ananikumbuka mimi, aliponiona tu nashuka kwenye gari alinikimbilia na kunishika mkono kisha akaniuliza leo nimeacha wapi ndege,” alisema.
Kwa mujibu wa Mbowe, swali la mtoto huyo lilikuwa limemgusa sana kwani inaonyesha kumbukumbu aliyoiacha miongoni mwa Watanzania na maelezo ya kazi wanazofanya wazazi wake, yanaonyesha jinsi Watanzania wengi wanavyohangaika katika maisha.
“Naahidi kumsomesha kwa kipindi chote cha uhai wangu, hata Marekani atakwenda,” alisema Mbowe.
Baada ya maneno hayo alitoa sh 20,000 na kumkabidhi mtoto huyo jukwaani ili akanunuliwe nguo. Ili kuhakikisha kuwa ahadi ya kumsomesha inakamilishwa, alimkabidhi kwa Balozi Christopher Ngaiza, ili awasiliane na wazazi wake kwa ajili ya kumpeleka Dar es Salaam ili kuanza harakati za kupata elimu.