JUMLA ya watu milioni nne wanatarajiwa kupimwa ukimwi hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu kupitia kampeni kubwa ya kitaifa inayozinduliwa leo na Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wilson Mukama, alisema kuwa serikali imetangaza kampeni ya taifa ya upimaji wa virusi vya ukimwi kwa hiari kama mojawapo ya mkakati wa kutekeleza azma ya kutoa huduma za upimaji wa maambukizi ya VVU kwa kila Mtanzania hata wale waishio vijijini.
Alisema kuwa matayarisho yaliyofanyika katika zoezi hilo ni kutangaza siku ya upimaji wa hiari wa maambukizi ya VVU, utayarishaji wa wataalamu watakaotoa huduma ya upimaji na ununuzi na upatikanaji wa vifaa mbalimbali vitakavyotumika wakati wa utekelezaji kampeni hiyo.
Mukama alisema serikali ina utaratibu wa kupata mahitaji yake ya vitendanishi na dawa zinazotumika katika upimaji wa magonjwa na matibabu kwa kutumia fedha za serikali kupitia zabuni na misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali.
Pia alisema katika matayarisho ya kampeni ya taifa ya upimaji wa hiari wa maambukizi ya VVU, kuna vifaa mbalimbali vilivyotolewa na wahisani ikiwa ni Capillus, Determine na SD Bioline na serikali haiingilii utaratibu unaotumiwa na wahisani katika kununua vifaa vinavyotolewa kama misaada.
Alisema kuwa matumizi ya vitendanishi hivyo yanafuata utaratibu uliowekwa wa kupunguza matumizi ya Capillus na kuongeza matumizi ya SD Bioline hatua kwa hatua hadi wataalamu wote watakapokuwa wamepatiwa mafunzo ya utumiaji wa vifaa hivyo vinavyobadilishwa.
Alisema mabadiliko hayo yataenda sambamba na upatikanaji wa vifaa hivyo vya SD Bioline na upatikanaji wa vitendanishi vya SD Bioline vya kutosha kusambazwa nchini kote.
Hata hivyo, aliwahakikishia wananchi kuwa wakati wa kutekeleza kampeni hiyo, vitendanishi vitakavyotumika havina hitilafu na kuwataka wanachi kujitokeza kwa wingi wakati wa kampeni hiyo inayozinduliwa leo jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa taratibu zote za uchunguzi wa magonjwa zimekuwa zikizingatia ubora wa huduma zinazokubalika kitaifa na kimataifa na maadili ya kazi. Alisema huduma hiyo itazingatia ubora wa vipimo, wataalamu waliofuzu mafunzo ya upimaji, usiri, hiari na ushauri nasaha.
Pamoja na kutangaza kuanza kwa kampeni hiyo, alikuwa akitoa taarifa kuhusu taarifa ambazo zimekuwa zikiandikwa na vyombo vya habari kuhusu matumizi ya vitendanishi vya kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Alisema kuwa ulimwenguni kuna zaidi ya vipimo 20 vya upimaji wa haraka wa VVU vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Alisema kuwa Tanzania imekuwa ikitumia vipimo vya Capillus na Determine kwa upimaji wa maambukizi ya VVU tangu 1998 na vipimo hivyo havina hitilafu katika upimaji wa maambukizi ya VVU isipokuwa utunzaji wa Capillus unahitaji ubaridi wa nyuzi joto 2C hadi 8C.
Hata hivyo, alisema kuwa mwaka 2006 wizara ilifanya tathmini ya vipimo vya upimaji wa maambukizi ya VVU kwa kutumia SD Bioline badala ya Capillus na pia serikali ilitangaza utaratibu utakaotumika katika kipindi cha mpito ambacho vitendanishi vyote vya Capillus na SD Bioline vitatumika.