Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Balali ashtua watu
Balali ashtua watu
By Habari Tanzania | Published  07/14/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


WANASIASA na wanaharakati kadhaa, wameeleza kusikitishwa kwao na msimamo wa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Balali wa kukataa kujiuzulu wadhifa wake kutokana na tuhuma mbalimbazi zinazoelekezwa kwake.

Miongoni mwa wanasiasa walioeleza kushangazwa na msimamo huo wa Balali, ni Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (Chadema) ambaye alikuwa mwanasiasa wa mwanzo kuzungumzia kuhusu tuhuma kadhaa zinazoikabilia BoT na Balali bungeni mjini Dodoma.

Dk. Slaa katika maelezo yake kwa gazeti hili alisema, Balali alishindwa kujibu hoja zozote dhidi ya tuhuma zinazomkabili, na badala yake akasisitiza kuhusu haja ya Bunge kuunda kamati teule.

“Unafikiri mtu yeyote anayetuhumiwa atasema nini? Hata mtu akipelekwa mahakamani huwa anakana tuhuma zinazomkabili. Kutokana na tuhuma zinazomkabili, hajajibu hoja hata moja,” alisema Dk. Slaa.

Naye Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe (Chadema), alisema tuhuma zinazomkabili Balali ni nzito na kwamba, kama ilivyo kwa mtuhumiwa mwingine yeyote, ni lazima akane.

Mbunge huyo alisema kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari, Balali bado hajajisafisha, kwani tuhuma zinazomkabili ni nzito na zinafahamika ndani na nje ya nchi.

“Alipaswa kusubiri serikali iunde tume kama tulivyoomba na tume hiyo ndiyo ingeweza kumsafisha ama la, lakini yeye mwenyewe hawezi kujisafisha. Sasa na hao wenzake nao wataitisha mkutano na waandishi wa habari?” alihoji.

Kashfa ya BoT kupitia mtandao wa intaneti, ziliibuliwa kwa mara ya kwanza bungeni na Dk. Slaa wakati akichangia maoni ya kambi ya upinzani wakati wa mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha.

Dk. Slaa alisema kambi ya upinzani ilikuwa ikitaka kuona taarifa aliyoitoa bungeni kuhusu ubadhirifu mkubwa ndani ya BoT unaomgusa Gavana wa Benki Kuu, pamoja na wafanyabiashara wengine wakubwa, akiwemo Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya (CCM), kupitia kampuni anayoimiliki, zinachunguzwa kwa kina.

Alisema Dk. Mzindakaya alichukua mkopo kwa shughuli za kampuni yake ya SAAFI wa sh bilioni 6.217 na kwamba aliomba ‘Overdraft facility’ ya sh mil. 450 zitakazolipwa kwa miaka mitano; mkopo wa sh bilioni 2.8 zitakazolipwa katika miaka mitano na dola za Marekani mil. 2.528.

Kutokana na tuhuma hizo, Waziri Meghji wakati akifanya majumuisho ya hoja yake, alisema serikali imeagiza kuanza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje zinazoikabili BoT.

Waziri Meghji alisema, tayari alikuwa ameshamwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali, kuanza uchunguzi kuhusu tuhuma hizo.

Akizungumzia msimamo wa Balali, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Labour (TLP), Augustine Mrema, alisema ushujaa alionao gavana huyo unatokana na madhambi ya ubadhirifu waliyonayo viongozi wa juu serikalini.

“Hakuna anayeweza kumwajibisha Balali kwa sababu wote ni wabadhirifu… huyo gavana ni kielelezo tu cha madhambi ya watawala wetu.

“Nani wa kumfunga paka kengele katika hili?” Alihoji Mrema na kuongeza: “Kinachoendelea katika serikali hii ni kulindana na si vinginevyo, yeye (Balali) ni kipaza sauti cha wakubwa.”

Kuhusu kukua kwa uchumi, mwenyekiti huyo alisema, wananchi hawafaidiki wala hawaoni nafuu ya maisha kwa sababu mzigo wa kulipa madeni ya viongozi wameachiwa peke yao.

“Eti wanasema uchumi umekua… hakuna kitu kama hicho, umekua mifukoni mwao kwa sababu wanakopa halafu sisi tunaingia mzigo wa kuwalipia, wao wanafaidika na familia zao.

“Anajidai kwamba anakerwa na kuombaomba kwetu wakati yeye ndiyo chanzo,” alisema Mrema.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wameshinikiza Balali ajiuzulu kama alivyofukuzwa kazi mkaguzi wa mahesabu aliyetoa taarifa zilizodaiwa kuwa ni za uongo.

Hayo yalisemwa na Gemma Akilimali, Ofisa Ushawishi wa TGNP, jana, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari, ambapo aliendelea kuhoji inakuwaje Gavana wa BOT amepatikana na tuhuma, lakini hataki kujiuzulu wakati mtu aliyetoa taarifa hizo aliachishwa kazi?

Akilimali aliendelea kusema kuwa, tangu Januari mwaka huu walikuwa wakifuatilia matumizi ya fedha za bajeti ya serikali Benki Kuu na kukuta serikali imekwishatumia pesa zaidi ya zilizoainishwa kwa matumizi ya mwaka wa fedha wa 2006/07.

“Lakini tuliambiwa tusubiri mpaka muda wa kwisha kwa bajeti ndio tutapewa taarifa kamili ya matumizi ya pesa za bajeti, lakini tulishangaa kwa nini Benki Kuu ilinyamazia kauli hiyo inayoonyesha kuwa, kuna matatizo katika benki hiyo,” alisema.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.