Na Nick Thiong'o
Kwa bei nafuu na tena kwa urahisi utaagiza sigara dukani; na kwa urahisi pia utaiwasha, uivute kwa ustaarabu, na utupe kipande kinachosalia ovyovyo, popote na vyovyote vile. Ni jambo la kuhuzunisha na kukeketesha maini kuona wasichana wengine hapa Nairobi wamekuwa wa bwerere kama hizi sigara zinazoeneza saratani ya mapafu.
Kabla haujandwa na mori na kuamba kuwa falsafa yangu ni potovu, kwanza tilia maanani kuwa, una sababu murwa ya kugadhabika kama uko katika kikundi hiki cha nipe-hela-nami-nikupe. Hata kama hasari zimekupanda, jaribu kuwa na bashasha angalau tuweza kujadiliana kikamilifu. Mtazamo wangu ni huu, kitu chochote cha bei ya chini, huenda kikakugharimu hela nyingi unapokinunua mara kwa mara.
Nadhani tunaweza kukubaliana na wavutaji wa sigara kwamba, ile starehe ya muda mfupi wanayopata kutokana na uraibu wao hafifu, huja na jinamizi la kuwa mtumwa wa kemikali za sigara. Na mambo yanapoenda mrama kabisa, uvutaji wa sigara uambatana na saratani.
Kuna mabinti hapa Nairobi ambao huchimba madini, hususan dhahabu. Najua washangaa, kuna dhahabu Nairobi? Vipusa hawa wajulikana kama Gold-diggers kwa lugha ya kiingereza.
Wanaweza kuwa ni wa bei ya juu, au bei duni; bei yao italingana na anyefanya upembuzi. Sababu ni mie nafanya upambanuzi huu, hawa vidosho ni bidhaa yenye gharama ya chini kupindukia, laiti bidhaa hii ingengawanywa na serikali kam mali ya umma.
Lakini wanaume wenzangu nao wamepumbaa, wanawashutmu kwa upande mmoja na kuwapapasa kwa mkono mwingine, wameshakuwa maabusu. Maulana awa rehemu sababu wameingiza guu kwenye mtego mkali.
Tu pamoja lakini? Siongei kuhusu makahaba. Makahaba ni wachuuzi wa kwaida na wamekuwepu tangu jadi. Hupata hela zao kihalali; wanakwambia bei yao,unajitetea, kasha walipa, nao wanawasilisha bidhaa. Hamna ulaghai hapo kama wewe mwenye uchechefu wa maadili.
Hata wagiriki wanaweza kubainisha haya, juzi tu uchumi wao ulimarika kwa asilimia 25 kwa kukusanya ushuru nje ya uchumi rasmi, ukahaba ukiwa mojawapo wa huu uchumi mbadala.
Kama bado haujapevuka katika haya mambo nyeti, wacha nikuarifu bayana bila kupiga chenga. Najadilia kuhusu huyo kidosho anayekuahidi kuwa amedata nawe hadi mauti, ilhali ukitizama kwa makini utaziona ishara za dolla ya kimarekani machoni mwake.
Hana haja na uzito wa mahaba yako ndungu, ni uzito wa mfuko wako anaonyemeleo kwa ustadi, tena kimya kimya. Ama haujui samba mwenda pole ndiye mla nyama?
Hawa wachimba dhahabu; wanajifanya juha lakini wamepeveka na wanaona zaidi ya upeo ya upeo wa macho yako. Wanaiona shilingi, watakapo kupora, ndio utangamua nani bonge la juha kati yako na wao. Wana ukali wa meno, urefu wa makucha na utamu wa lugha.
Watakufanya ujihisi kama sultani mwenye staha ya kufana. Ukisha chovya asali, utailamba kwa ncha ya kisu, na utamu utakapokunogea utaukata ulimi wako. Nakupiga msasa usije ukaangamia; kufumba macho na kufumbua; watakuwa wamekurarua kama simba araruavyo mlo wake.
Muulize tajiri mmoja hapa Jijini Nairobi; bado hajakuwa nafuu tangu ashikwe na mbumbuwazi na kupigwa na butwaa vilivyo. Hawa wachimba dhahabu wanapanga foleni mlangoni kwake na kesi za kudai mamiliona; huku wakiandama na mawakili wao. Ole wake!
Natarajia unamfamu Anna Nicole Smith na ulifikiwa na habari za kifo chake. Kama haumfahamu basi wapaswa kusoma habari kwa upana. Jarida moja la Marekani liliripoti kuwa Nicole Smith alikuwa mchimba dhahabu sugu, yaani gold-digger.
Sidhani kuna jina lingine mwafaka ambalo lingefaa kuliko mchimba dhahabu. Yule binti alikuwa azma gani akimuoa mzee wa miaka 89 mwenye mabilioni ya pesa, ilhali msichana huyu alikuwa wa miaka 26. Mzee huyu alipofariki, Nicole aliwasilisha kesi hadi Mahakama Kuu ya Marekani ili apate nusu ya mali ya yule tajiri.
Hawa wachimba dhahabu si lazima wawe wajanja ili wakupore mapeni, la hasha. Kulingana na jarida hilo, hakimu mmoja aliandika kuhusu Nicole, upungufu wake wa masomo ni wakustaajabisha. Jambo la simanzi nikuwa Nicole aliaga dunia kabla ya mahakama kutoa uamuzi.
Kushiriki kimapenzi na wachimba dhahabu kunaweza kulinganishwa na kuingiza mkono kwenye mdomo wa mamba ukijaribu kutoa kipande cha nyama.
Wakishakuhadaa, hautakuwa unalalama tu kama mpenzi aliyepewa talaka, utakuwa masikini hohe hahe. Haya ndio malipo ya kutamani vyote kwa pupa.
Kaka, hawa wapenzi wenye kuenzi madini wakikuona, wanaona nchi yenye asili mali ya dhahabu. Hivyo ukiwaona toka shoti kama mende aliyefumaniwa jikoni na mpishi akilamba mlo.
Mausia yangu ni haya; usingwafue mnofu usioweza kuutafuna, huenda ukpoteza meno yote nakuwa kielelezo kwa jamii.
Tamati//