GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Balali, amesema moja ya udhaifu wa taifa kiuchumi umetokana na tabia ya kuomba bila aibu.
Balali alisema hayo jana wakati akieleza hali ya mwelekeo wa uchumi wa taifa pamoja na mapungufu ya taifa yanayofanya kuendelea kuwa na uchumi unaosuasua.
Alisema Tanzania kama taifa, linajiona wanyonge na hali hiyo imetawala pia kwenye vichwa vya wananchi wengi.
“Tuna tatizo la kujiona sisi wanyonge kwa kila kitu. Mtu akipata tatizo kidogo badala ya kufikiria jinsi ya kutatua, kitu cha kwanza anafikiria mhisani, tena sio wa nje ila mjomba, kaka, shangazi, hatuwezi kupiga hatua kwa kuendelea kuwa tegemezi,” alisema.
Alisema suala la kuomba hisani, linapaswa kuwa la hatua ya mwisho baada ya kila jitihada kushindwa, lakini kwa sasa Watanzania wametoa aibu katika kuomba kwani wanaomba bila aibu.
Mbali ya kubeza kuwa ombaomba, Balali alisema jambo lingine linalosababisha kusuasua kukua kwa uchumi ni kukosa moyo wa uzalendo.
Alisema baadhi ya viongozi hawana uzalendo na ndio maana wanapopata nafasi za kuwatumikia wananchi, wanafanya ubadhirifu bila kuchukuliwa hatua.
“Tuache kuwa ombaomba, tuwe na uzalendo, tulinde maliasili zetu, tupende kazi na tubadili fikra zetu kwamba kuondoa umasikini inawezekana,” alisema Balali.
Alisema kaulimbiu ya viongozi wa serikali ya ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’ ni kauli inayowasaidia wananchi kujijenga kisaikolojia, kwamba kuondoa umasikini ni jambo linalowezekana.
Akizungumzia hali ya uchumi nchini, Balali alisema hali ya ukuaji wa uchumi ni nzuri na kwamba serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa na kufanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei.
Pia aliipongeza bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2007/2008 kuwa imezingatia hali halisi ya sera ya kukuza uchumi wa taifa.
Alisema hali ya mfumuko wa bei, imedhibitiwa kuanzia mwaka 1995 ambapo Januari mwaka huu, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 35 na Januari mwaka 1999, ulishuka hadi asilimia 9.1 na lengo la serikali ni kushusha mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 4.5.
Alisema mafanikio ya kasi ya ukuaji wa uchumi na kuondoa umasikini, yataanza kuonekana kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, kukuza uchumi ni jambo la polepole na sera zilizopo za kukuza uchumi, zinapaswa kuwa endelevu.
Akizungumzia kupanda kwa bei ya mafuta, Balali alisema ingawaje bei ya mafuta katika soko la dunia iliendelea kupanda, na kwa miaka miwili iliyopita ilipanda kwa zaidi ya dola za Kimarekani 60 kwa pipa na sasa imefikia dola 75.
Alisema matokeo ya kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kwa upande wa mfumuko wa bei, ulitarajiwa kuwa mdogo kwa mwaka 2007/08 kuliko ilivyokuwa kwa mwaka wa fedha ulioisha mwaka 2007.
“Wakati wa maandalizi ya bajeti, mambo mengi yalizingatiwa ikiwemo ongezeko la pato la taifa (GDP), hivyo bajeti ya 2007/08 ilitarajiwa kuwezesha mafanikio ya mipango ya ukuaji wa GDP kwa asilimia 7.3 kwa mwaka 2007,” alisema.
Hata hivyo, alisema mwaka wa 2007/08, serikali haitakopa toka kwenye vyanzo mbalimbali kwa ajili ya upungufu wa bajeti yake hali ambayo itapunguza wasiwasi wa mfumuko wa bei.
Kuhusu kuanguka kwa shilingi, Balali alisema kunatokana na mabadiliko ya fedha za kigeni, lakini bado haijaathiri ukuaji wa uchumi.
Alisema kuporomoka kwa shilingi, kumeifanya BoT kufikiria kutengeneza noti kubwa zaidi ya sh 10,000.