Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kifo cha Amina Chifupa chaivuruga familia yake
Kifo cha Amina Chifupa chaivuruga familia yake
By Habari Tanzania | Published  07/13/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Shabani Matutu


KIFO cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Amina Chifupa (CCM), kinaonekana kuichanganya familia yake ambayo sasa imebadili mwelekeo wake wa awali, na kuanza kulihusisha tukio hilo na sababu za kishirikina.

Wiki tatu baada ya familia hiyo kukihusisha kifo hicho na maradhi, ikisema alipoteza maisha kwa kisukari na homa kali, jana baba mzazi wa mbunge huyo, Mzee Hamisi Gabriel Chifupa, aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam taarifa tofauti na za kushangaza.

Mzee huyo, kada wa muda mrefu wa CCM alisema kuwa, baada ya Amina kuanza kuugua, familia ilipata ofa kutoka sehemu kadhaa kumpeleka mbunge huyo nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Aliwataja waliotaka kumpeleka Amina nje ya nchi kwa matibabu kuwa ni Ofisi ya Bunge pamoja na Kampuni ya Mohamed Enterprises.

“Nilikataa ofa hizo zote baada ya kujua kuwa ugonjwa unaomsumbua marehemu kuwa ni wa Kiswahili, tukaona si vyema kumpeleka nje na badala yake tukaamua kumpeleka kwa waswahili ili atibiwe… kama anaumwa ugonjwa wa Kiswahili kwanini tumpeleke Ulaya?” alisema Chifupa na kuhoji.

Akielezea matukio kabla ya kifo cha binti yake, Chifupa alisema kuwa, Mei 8 mwaka huu, alikutana na binti yake nyumbani kwake Mikocheni, alipokwenda kumtaarifu kuwa alikuwa na ziara ya kikazi mkoani Mtwara.

Hata hivyo, wakati huo hali yake kiafya ilikuwa imeshaanza kuzorota, aliamua kumzuia asiende ziara hiyo, lakini binti huyo aligoma na hatimaye akaamua kuondoka Mei 6, kwa kuwaomba wamsindikize sambamba na mdogo wake.

Alisema wakiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, walikutana na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Profesa Mark Mwandosya, akiwa katika chumba cha wageni mashuhuri (VIP) na Amina alizungumza naye kabla ya waziri huyo kuondoka.

Chifupa alisema baada ya muda, Amina alimuita mhudumu wa chumba hicho na kumuomba amrudishie mzigo wake kwa sababu alikuwa ameahirisha safari yake.

Alisema baada ya Amina kuahirisha safari, walirejea nyumbani kwao Mikocheni, lakini hali ya binti yake ilianza kubadilika huku akisema maneno makali akitaja majina ya baadhi ya viongozi na kudai kuwa wao ndio walimsababishia matatizo hayo yote.

“Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, tulimuita daktari ili amuhudumie, daktari alimpatia dawa, lakini hali yake haikuwa nzuri, ndipo tukagundua kuwa yale yalikuwa mambo ya Kiswahili… tukaamua kumpeleka kutibiwa Kiswahili kwani alikuwa hali chakula katika kipindi chake chote cha kuugua,” alisema Chifupa.

Baada ya kumtibu kwa waganga wa kienyeji, hali ilizidi kuwa mbaya na mwisho waliamua kumpeleka hospitali ambapo aligundulika kuwa na kiwango kikubwa cha sukari mwilini kilichofikia kipimo cha 400 ambacho kilikuwa hakishuki na wakaamua kumhamishia Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.

Alisema hata wakati alipokuwa hospitalini hapo, Amina bado aliendelea kutamka majina ya viongozi ambao alikuwa akiyatamka awali, na aliendelea kufanya hivyo hadi mauti yanamkuta Juni 26 mwaka huu, majira ya saa 2:45.

Hata hivyo, Chifupa hakuwa tayari kuyataja majina ya viongozi ambao binti yake alikuwa akiwataja wakati wa kuugua kwake, lakini alisema yapo baadhi ya majina ambayo tayari yameshaandikwa magazetini.

Jambo lingine lililoisababisha familia ya Chifupa kukihusisha kifo hiki na mambo ya kishirikina, anasema ni ndoto aliyoiota siku tatu baada ya kifo cha mbunge huyo.

Alisema katika ndoto hiyo, alitokewa na bibi wa marehemu Amina, Tulionana Mnyalape, ambaye alimuuliza mjukuu wake yupo wapi.

Alipomjibu kuwa alikuwa kwa Mungu, bibi huyo alisema kuwa Amina hakutaka kwenda huko mapema, ila binadamu ndio waliompeleka kabla ya wakati wake.

Pia mdogo wake, Bakari Chifupa, alimuota Amina akimwambia kwamba waishi kwa amani, wapendane na wamuombee na wawaheshimu wakubwa na pia amueleze bibi yake mzaa mama yake kuwa amekwenda hapo kijijini kuishi naye.

Kuhusu kuhusishwa kwake na vita dhidi ya dawa za kulevya, alisema kuwa iwapo kifo cha mwanawe kimehusika na wauzaji wa dawa hizo, vita hiyo itakuwa haijazima, bali itakuwa imetiwa petroli.

Wakati huo huo, Chifupa alisema kuwa familia yake imeanzisha mfuko wa kumuenzi marehemu Amina, ambao unajulikana kama ‘Amina Chifupa Foundation’ nia ikiwa ni kulienzi jina la marehemu Amina kwa yote aliyokuwa akiyafanya enzi za uhai wake kama vile kupiga vita dawa za kulevya na kusaidia wasiojiweza.

Kwa mujibu wa Chifupa, Mwenyekiti wa mfuko huo ni diwani wa Njombe, ambaye ni mjomba wake, Augostino Mbanga, ambapo pia gari la marehemu Amina litatumika katika shughuli za mfuko huo na kuanzia sasa litakabidhiwa kwa viongozi hao wa mfuko.

Aidha, alisema kuwa baadhi ya wajumbe wa mfuko huo watatoka kwenye kamati ya kampeni ya ubunge ya marehemu Amina na kamati ya mazishi yake.

Alitoa wito kwa mtu mwenye nia ya kuchangia mfuko huo, afanye hivyo kupitia akaunti katika benki ya CRDB tawi la Kijitonyama yenye namba 01J1014153400.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.