Na Daniel Mjema, Dodoma
KAMA ni kilio cha barabara basi wabunge walitumia siku ya jana kila mmoja kwa staili yake, kuwasilisha kilio hicho huku baadhi wakitaka ujenzi wa barabara za lami nchini ufanywe kwa kuzingatia uchumi wa kijiografia.
Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), ndiye alikuwa wa kwanza kutoa hoja ya barabara kujengwa kwa kuzingatia kigezo cha uchumi wa kijiografia akisema anasikia uchungu kuona barabara za korido ya kati hazijapewa umuhimu wa kutosha.
Selelii aliliomba Bunge na Serikali kufanya maamuzi mazito ya kujenga barabara
muhimu za Dodoma hadi Singida na Tabora na reli ya Tabora hadi Kigoma ili kufungua fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
�Ni aibu kwa Tanzania kwamba sasa ni karibu miaka 50 tangu tupate uhuru, na bado wananchi wetu wanaotoka Musoma na Mwanza kwenda Arusha na Dar es Salaam wanalazimika kupitia Kenya,� alisema Selelii.
Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango Malecela (CCM), alishangaa namna ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Jimboni kwake 2005 ya kujenga barabara ya Mkomazi-Ndungu-Same haiko kwenye orodha ya barabara zilizoahidiwa na Rais.
�Ninasimama hapa kuzungumza kwa uchungu sana kwamba barabara hii ni ya kisiasa zaidi�Rais aliwaahidi wananchi wangu kuwa ataijenga kwa kiwango cha lami na wakamchezea mpaka ngoma kwa furaha, lakini haipo,� alilalamika Kilango.
Mbunge huyo alitoa tuhuma nzito dhidi ya mhandisi mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, ambaye taarifa zake zinaonyesha alitumia mamilioni ya fedha kukarabati barabara ya Lugulu-Ndungu, lakini barabara hiyo ni kichaka hadi sasa.
�Baada ya kufuatilia sana naona Waziri Mkuu sijui ni Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro
amemhamisha Mhandisi huyo, lakini ninachotaka si kuhamishwa kwa mkurugenzi au mhandisi, ninachotaka ni barabara ijengwe kwa kuwa serikali ilishatoa fedha,� alisema Kilango.
Mbunge wa Longido, Michael Laizer (CCM) alisema kama ni maeneo ambayo yamekithiri kwa baadhi ya watendaji kupokea asilimia 10, basi ni eneo la fedha za
barabara kwa kuwa halina ukaguzi makini.
Laizer alionyesha kushangazwa kwake na hatua ya Serikali kwamba tangu mwaka 1996 bajeti ya Serikali inaonyesha kuna fedha za kukarabati au kujenga barabara ya Namanga - Arusha, lakini barabara hiyo haijengwi kila mwaka.
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Manyinyi (CCM) alitaka Serikali iruhusu mabasi ya kutoka Musoma kwenda Arusha yapitie ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti bila kulipa kodi yoyote ili kuwapunguzia wananchi gharama.
Manyinyi alisema kila gari lenye uzito wa tani 10, yakiwamo mabasi yanayopita katika hifadhi hiyo, hutakiwa kulipia Sh400,000 hali inayofanya nauli za mabasi na gharama za kusafirisha bidhaa muhimu kuwa juu kuliko kawaida.
Mbunge wa Gando, Khalifa Khalifa (CUF), alitaka kipaumbele cha serikali kwa sasa na miaka ijayo kiwe ni ujenzi wa barabara na kuonya kuwa tatizo la serikali ni kutaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja wakati haina uwezo huo.
Suala la kupanda kwa bei za mafuta nalo liliibuka tena bungeni jana, baada ya Mbunge wa Muleba Kaskazini, Wilson Masilingi (CCM), kutaka serikali iandae utaratibu wa kuwa na akiba ya mafuta itakayotumika kusawazisha bei inapopanda.
�Anzisheni Strategic Oil Reserve (mafuta ya akiba) ili hao wafanyabiashara
wakituletea uhuni wa kupandisha mafuta basi serikali inamwaga mafuta kwenye soko ili kuwamaliza,� alisema Mbunge huyo.
Masilingi alisema kwa kuwa imethibitika kuwa hali ya usafiri katika mikoa ya Kanda ya Ziwa bado ni tatizo, ni vyema serikali ikarudi kuendesha biashara ya usafiri wa majini kwa kununua meli kubwa itakayotoa huduma katika mikoa hiyo.
Pia alitaka Serikali iuwekee lami haraka Uwanja wa Ndege wa Bukoba ambao ni tegemeo kubwa kwa usafiri na akaenda mbali kwa kudai kuwa kwa hali ilivyo sasa ni hatari sana, hasa wakati ndege zinapotua na kuruka.
Mbunge wa Viti Maalumu, Fatuma Mikidadi (CCM), alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Kibiti-Lindi sasa kumegeuka kuwa wimbo wa taifa kwa kuwa imeahidiwa miaka nenda rudi, lakini hadi sasa haikamiliki.