Na Waandishi Wetu, Morogoro
WAMILIKI wa mabasi yanayotoa huduma katika mjini hapa, wamegoma kutoa huduma ya usafiri huo wakipinga kutoza nauli ya zamani kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.
Mgomo huo ulisababisha wakazi wa Morogoro kutembea kwa miguu umbali wa wastani wa kilometa 20 hadi 30 kufika katika maeneo mbalimbali wanakofanyia shughuli zao.
Kutokana na kukosekana kwa usafiri wa daladala, teksi zilikuwa zikitoa huduma ya usafiri kwa kutoza nauli kati ya Sh500 hadi Sh1,000 kwa kila abiria kulingana na umbali wa eneo anakokwenda.
Magari aina ya Canter, pikipiki na baiskeli, pia zilikuwa zikisafirisha abiria mmoja kwa kutoza Sh300.
Wakati hayo yakiendelea kutokea, daladala zote zilikuwa zimeegeshwa katika kituo kikuu cha daladala kilichopo katikati ya mji, huku madereva na makondakta wakiwacheka wananchi waliokuwa wakitembea barabarani kwa miguu.
Mgomo huo uliwathiri zaidi wanafunzi wanaosoma shule za ndani na nje ya halmashauri hiyo ambao walifika katika vituo vya mabasi saa 12.00 asubuhi, wakisubiria usafiri na kusota mpaka saa 3.00 asubuhi bila kujua la kufanya.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao waliandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Said Kalembo, ili kuwashinikiza wamiliki hao kuendelea kutoa huduma hiyo.
Wanafunzi hao wa shule za sekondari za Bigwa, Kihonda, Mji Mpya, Uluguru, Mwembesongo na Muungano waliungana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Sinai kwenda kumwona Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Hawa Ng'humbi.
Baada ya kufika katika ofisi hiyo, walipokelewa na katibu tawala wa wilaya hiyo, Epharaem Wapalila.
Akizungumza na wanafunzi hao, Wapalila alisema Mkuu huyo wa Wilaya alikuwa akishughulikia suala hilo na kwamba alikuwa katika mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa wamiliki wa mabasi hayo na viongozi wa Sumatra.
Aliwataka kwenda shuleni wakati wakati suala hilo likishughulikiwa na serikali ya wilaya, ombi lililoonekana kutowaridhisha wanafunzi hao.
Mmoja wa madereva wa daladala zilizogoma, Nasibu Juma, alisema
uamuzi huo unatokana na kushinikizwa na serikali kutoza nauli ya zamani wakati wao wamepandishiwa mafuta.
Alisema vituo mbalimbali vya mafuta mkoani Morogoro vimekuwa vikiuza mafuta kwa Sh1,500 na hivyo wao kulazimika kuongeza nauli ili kuweza kufidia ongezeko hilo.
Kutokana na mgomo huo, polisi mkoani hapa wanawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kushawishi mgomo huo na kuwatishia wale wote waliokuwa na nia ya kutoa huduma hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, alisema watu hao waliwatishia madereva na wamiliki wengine wa daladala waliokuwa na nia ya kutoshiriki kwenye mgomo huo.
Pia alisema jumla ya magari 52 yalikutwa yakiwa yamesimama katika vituo mbalimbali kikiwemo cha Masika bila kutoa huduma yeyote.