FEDHA za mifuko ya barabara katika halmashauri, zitaongezeka na kuongeza idadi ya barabara zitakazotengenezwa katika mwaka wa fedha 2007/08, Bunge limeelezwa.
Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani, aliliambia Bunge mjini hapa kuwa, ongezeko la fedha hizo litatokana na ongezeko la ushuru kwa mafuta ya dizeli na petroli.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), Kombani alisema fedha za mfuko wa barabara zimekuwa zikiongezeka kila mwaka, lakini kwa mwaka wa fedha 2007/08 lipo ongezeko kubwa katika fedha hizo.
Selelii alitaka kujua halmashauri zitanufaika vipi na fedha zilizoongezwa katika ushuru wa mafuta ya magari ili kuzifanyia matengenezo barabara zake.
Katika swali lake la msingi, Selelii alitaka kujua kama Serikali ipo tayari kuzifanyia matengenezo barabara za vijijini zilizopo Nzega ili kufungua soko katika maeneo hayo kutokana na halmashauri ya wilaya hiyo kutokuwa na uwezo wa kutengeneza barabara hizo.
Akijibu swali hilo, Kombani alisema jukumu la kutengeneza barabara za vijiji ni la halmashauri husika kama itaona upo umuhimu wa kutengeneza barabara hizo.
Alisema serikali kupitia Bodi ya Mfuko wa Barabara imekuwa ikitoa fedha katika halmashauri kwa ajili ya matengenezo ya barabara za wilaya na za mjini ambapo Halmashauri ya Nzega pia imepatiwa fedha hizo.
Alisema kama barabara za vijiji zitapatiwa matengenezo na kukidhi vigezo vya kuwa barabara za wilaya, zitapandishwa hadhi na kupatiwa fedha za matengenezo kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara.
Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2007/08 Halmashauri ya Wilaya ya Nzega itapatiwa jumla ya sh milioni 73.102 kutoka TAMISEMI kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo barabara zake ambapo kiasi hicho kimeongezwa ikilinganishwa na mwaka uliopita.