“TUPO makini, tupo ndani ya wakati na tunaweza kutekeleza tuliyokusudia. tumesikia mengi yakichangiwa katika mjadala wa ofisi yangu, lakini ninachoweza kuwaeleza Watanzania ni kwamba maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana.”
Haya si maneno yangu, ni sehemu ya maelezo ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, bungeni siku akifunga mjadala wa hotuba ya makadirio ya matumizi ya ofisi yake Julai 2, mwaka huu.
Ilikuwa ni siku ya pili tu tangu kuanza kutekelezwa kwa mwaka mpya wa fedha wa 2007/08 na hivyo kutekelezwa kwa kodi mpya ambazo zimeongezwa kwenye bajeti hiyo, kama alivyowasilisha Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, Juni 14, mwaka huu.
Kodi hizo ambazo zililalamikiwa sana hadi kumfanya Meghji kukosa subira na kushambulia vyombo vya habari kwa madai ya kuwa vimekosa uzalendo kwa kuwa vilisema kwamba bajeti hiyo ni ya maumivu kwa wananchi, ni pamoja na ongezeko la kodi ya barabara kwa asilimia 100, kutoka sh 100 kwa lita hadi sh 200, na kodi nyingine kwenye bidhaa za jamii ya petroli.
Katika siku hiyo, mchana, Lowassa si tu alionyesha kwamba serikali yake au yao ipo, bali uchumi wa nchi ulikuwa ukielekea kupaa kama ndege inayochukua kasi kuruka.
Tangu Lowassa atoe kauli hii bungeni yapata siku 10 zilizopita, yapo mambo mengi yamejitokeza kuamsha mjadala kama kauli halisi ya uchumi kupaa ilikuwa inalenga nini hasa.
Hoja hizi zinaibuka kwa sababu kama kile wanachosema kwa kimombo “serendipity au coincidence” yaani mambo kutokea kwa bahati fulani. Yaani kutangazwa kwamba uchumi unapaa wakati huo huo maumivu ya kodi yakiwa yameanza.
Siku Lowassa anatangaza uchumi kupaa, bei ya petroli ilipaa hadi sh 1,500 kwa lita kutoka sh 1,380. Ndiyo maana tunasema je, kauli ya kupaa na kodi mpya ni coincidence au serendipity? Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba hakuna kitu kinachotokea bila kuwa na sababu.
Hoja hapa inakuwa kwamba ni jambo la kujihoji na kujitafiti sana kwamba Lowassa anaposema maisha yenye neema yanawezekana na kueleza uchumi unapaa, siku wananchi wanaanza kupata maumivu ya bajeti mpya maana yake ni nini?
Kupaa kwa bei ya vitu, au kupaa kwa ughali wa maisha au uchumi kupaa kama zile zama za bei ya vitu kupaa (kurushwa) na hivyo kutokuwa na uwezo wa kununuliwa na wananchi?
Kuna usemi unasema kwamba ukienda kwa Warumi basi sharti uishi kama Warumi.
Ufafanuzi wa msemo huu ni mpana sana na unasaidia kuweka mwelekeo wa kutenda mambo katika maisha ya kila siku, kwamba huwezi kwenda kwenye msiba watu wakilia nawe uanze kuangua kicheko (hapa ninaomba radhi makabila yenye utani kwenye misiba yanivumilie).
Kwa maana hiyo, kusema kwamba uchumi unapaa wakati siku hiyo hiyo ndipo maumivu ya kodi mpya na hali ngumu ya maisha kuzidi kuwakabili wananchi, ni sawa na kufanya utani kwenye mambo magumu na mazito ambayo hakika ndiyo viongozi walioko madarakani sasa waliahidi kuyaondoa.
Maisha bora kwa kila Mtanzania maana yake halisi ni nini hasa?
Sijui kilichomo kwenye mioyo ya viongozi wanaotumia kauli hii ya maisha bora.
Lakini kwa vyovyote itakavyochukuliwa maisha bora ni kauli ya ulinganifu. Neno bora linatumika kuonyesha kwamba kutaka kuondoka kwenye hali fulani ya maisha (maisha duni) kwenda kwenye maisha yenye hadhi nzuri zaidi.
Yaani ongezeko la uwezo wa kuweza kumudu huduma na mahitaji ya msingi. Kutoka kula mlo mmoja hadi miwili kwa siku; kutoka kutembea kwa miguu hadi kuweza kupata nyenzo ya usafiri inayompunguzia mwananchi adha ya kutwanga mguu umbali mrefu; kutoka kunywa maji yasiyo salama na kupata maji salama na ya uhakika.
Kutoka kuishi nyumba za tembe hadi nyumba ya kuezekwa kwa bati na kujengwa kwa matofali bora zaidi, ya sementi au kuchoma.
Kutoka kushindwa kuwasomesha watoto kwa sababu ya kushindwa kulipa ada hadi kuweza kuwapeleka watoto shule bila kuumia sana.
Ubora huu ni kwa maisha halisi, mabadiliko ya kweli kutoka kupungua kwa gharama za maisha ambazo mwananchi hawezi kumudu hadi gharama ambazo anaweza kucheza nazo kulingana na kipato chake, iwe ni kwa kuajiriwa, kujiajiri au hata kwa mkulima kuzalisha mazao yake. Mlolongo ni mrefu bila kusahau njia za mawasiliano na ushiriki wa wananchi kuingia katika vyombo vya maamuzi yanayowahusu wao na hatimaye kuwa na sauti ya kweli katika vyombo hivyo.
Hapana shaka waaziri mkuu alipokuwa akizungumza habari hii alikuwa akimaanisha haya. Je, ni kweli wananchi wamekaa mkao wa kuachana na hali hizo hapo juu? je, ni mkao wa kupaa kweli kuachana na adha hizi au ndiyo kwanza mambo yamewafika shingoni wananchi?
Tunakumbuka siku Meghji anahitimisha mjadala wa bajeti ya serikali hakuonyesha kupendezwa hata kidogo na udadisi wa waandishi wa habari juu ya yale mabaya kwenye bajeti, hapana shaka alitamani ashangiliwe, apongezwe kwamba amekuja na bajeti kiboko. Mtizamo wa Meghji ni mwangwi wa matamanio ya viongozi wetu wa kutaka kusifiwa hata kama hakuna la maana lililotendwa ambalo linastahili kupigiwa mfano. Ndiyo maana hata waziri mkuu anaposema kwamba sasa uchumi unataka kupaa, anajua fika kwamba hayo si kweli. Anasema hivyo ili kutafuta kusifiwa tu!
Umma hauwezi kuachwa usadiki eti uchumi unapaa wakati bei ya bidha ana huduma zinazidi kupaa; wakati mfumuko wa bei unazidi kupaa.
Waziri mkuu anasema uchumi unapaa wakati akijua fika kwamba hata ahadi ya kuwapatia watumishi wa umma mishahara bora zaidi mwaka huu wa fedha haitatekelezwa; anajua wazi kwamba miradi mingi ya barabara imekwama, anajua kwamba uwezo wa kusomesha wanafunzi wengi zaidi elimu ya juu umepungua au hauendani na mahitaji; hapa ni kupaa kwa uchumi kwenda wapi?
Watu wengi wamesema matumaini ya wananchi walioshangilia Awamu ya Nne ilipoingia madarakani yameanza kufifia kwa kasi kubwa, hawa ni wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara na hata wasiokuwa na mbele wala nyuma, wote wanashangaa kwamba mbona ngoma inayopigwa kuhusu uchumi ni ya miaka yote hakuna mabadiliko?
Hakuna ubunifu, hakuna kusumbuka. Ni kweli awamu hii ilisema ‘no business as usual’ tena - hakuna tena kufanya kazi kwa mazoea.
Hivi hii haikuwa kauli thabiti ya waziri mkuu siku anaingia ofisini pale Magogoni?
Je, miezi 18 baadaye yeye na serikali yake amekuja na bajeti ya namna gani ambayo si business as usual? Tofauti ya kundi lililopo madarakani sasa ambalo lilijiandaa kwa miaka kumi kushika uongozi ni nini na lile kundi au makundi yaliyokuwa yanabahatisha tu?
Mbona ufanisi, utendaji na ubunifu ni kama wa watu waliopewa madaraka kwa kushtukizwa tu?
Kulikoni, mbinu za kushinda uchaguzi ndani ya chama na hata nje ya chama zilikuwapo, mbona mbinu za kubadili uchumi hazikuandaliwa mapema?
Awamu ya Nne ina jambo moja kubwa linalowatofautisha na wengine wote, walipanga kuchukua madaraka kisayansi na wakaweza. Hawakugongana na urais au uwaziri mkuu.
Hii si kudra kama ya Frederick Sumaye ya mwaka 1995, Lowassa na bosi wake walijua kwamba wamejipanga vema kwenda Ikulu, lakini kitu kinachonisumbua sasa, mbona hawaonyeshi kwamba wameamua na wamepanga kupambana na umaskini wa nchi hii kisayansi?
Hivi kama wapo watu ndani ya serikali wasioweza kuonyesha wanaweza na kuleta mabadiliko wanavumiliwa ili nini? Nini kinalipwa, fadhila au urafiki, nini kikwazo cha kuwajibishana?
Kama Awamu ya Nne inafikiri miezi 18 ni michache, wafirikirie mfano huu, kwamba kwa miezi 18 mwanamke anabeba mimba, anajifungua, anakaa likizo ya uzazi ya miezi mitatu, ananyonyesha miezi sita, na sasa anaweza kumwachisha mtoto ziwa na kubeba mimba nyingine ambayo sasa ingeweza kuwa ya miezi miwili.
Mwanamke huyu amefanya kazi kubwa ya kujenga jamii. Lakini kwa miezi 18 kwa Serikali ya Awamu ya Nne bado inafikiri ni suala la kujipanga na kuanza kupaa. Suala hapa si kupaa, ila watu wanataka kuanza kuona matunda.
Kuna kitu kimoja ningependa kuzungumzia hapa kabla ya kuhitimisha makala hii, kwamba ile kasumba ya watu walioko serikalini kudhani kwamba ni wao tu wanajua kufikiri na wengine wote hawajui, ndiyo inaelekea kuiandama awamu hii.
Sina hakika kama Meghji anaweza kuruka hili, alionyesha si dharau na kebehi tu kwa waliompa changamoto na mawazo mapya kwenye bajeti yake, bali alidhihirisha jinsi asivyoweza kusoma alama za nyakati.
Ni kwa jinsi hiyo hiyo ninashawishika kusema kwamba Waziri Mkuu wetu naye ajaribu kuwa makini na kauli zake za kisiasa, kwani gharama yake ni kubwa.
Atambue kwamba awamu hii bado haijajenga uchumi wowote endelevu ikiwa imewasilisha bajeti ya pili, atambue anawajibika kuwajibika zaidi na kuwawajibisha anaowasimamia ili wananchi waweze kuanza kuona na kuonja matunda ya mabadiliko waliyoahidiwa kwenye kampeni za uchaguzi.