ZIMETOLEWA ahadi nyingi lakini moja mbayo iliwashtua watu wengi na baadaye kuanza kuwafurahisha, ni ile iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika siku za mwanzo za utawala wake, akiwataka wananchi wajiandae kukabiliana na maamuzi magumu yatakayofanywa na serikali.
Iliwashtua wengi kwa sababu kwao huo ulikuwa ni mwanzo wa kubadili mwelekeo wa mambo. Walidhani kuwa huo ulikuwa ni mwanzo wa enzi mpya, ambapo maamuzi ya viongozi yasingeongozwa na utashi wa kisiasa.
Wengi hawakuamini kuwa kitu kama hicho kinaweza kutokea. Ilikuwa ni ishara ya kuanza kwa enzi mpya itakayoachana na mtindo wa viongozi kufanya mambo yaliyozoeleka. Waziri mkuu anauita mtindo huo ‘business as usual’ na kwa kuonyesha kuwa haumpendezi, ilikuwa ni jambo lake la kwanza kulikemea alipoingia ofisini kuanza kazi rasmi kama waziri mkuu.
Lakini ahadi hiyo iliwafurahisha. Wengi waliamini kuwa yanayosemwa yatatekelezwa ipasavyo. Bado walikuwa na matumaini kuwa Awamu ya Nne ndio mwarobaini wa matatizo yaliyotamalaki kwa miongo zaidi ya minne tangu nchi ijitawale.
Hawakuwa na wasiwasi kuwa ingekuwa tabu kidogo kulishughulikia suala hilo, hasa ukizingatia kuwa hado sasa, kufanya kazi kwa mazoea, licha ya kukemewa na Lowassa alipoingia ofisini siku ya kwanza, limekuwa ni donda ndugu, kuanzia uraiani hadi serikalini. Walikuwa bado wamelewa ule mvinyo wa ahadi za awamu hiyo kuwa imedhamiria kuyaondoa matatizo yao na kuyafanya maisha yao yawe bora.
Lakini wapo waliokuwa kina Tomaso, ambao hawakusadiki kuwa jambo hilo linawezekana. Baadhi yao walikuwa si rahisi kufanya mapinduzi ya haraka namna hiyo dhidi ya mfumo wa utawala uliopo, ambao umedumishwa kwa zaidi ya miongo minne. Walidai kuwa hali ya kulindana iliyotamalaki, ni vigumu mno kuondoka.
Walidai kuwa mfumo uliojengeka, ulikuwa hautoi nafasi kwa kiongozi yeyote, hata mkuu wa nchi, kufanya mambo ambayo kwa namna fulani yangehesabika kama mapinduzi. Na hilo lililokuwa linaahidiwa ni sawa tu na mapinduzi.
Miezi kadhaa imepita tangu ahadi hiyo itolewe na mambo kadhaa yametokea. Ni vigumu kujua moja kwa moja kuwa yapi ni maamuzi magumu na yapi yalikuwa maamuzi ya kawaida kwa sababu yalipotangazwa haikuelezwa wazi kuwa yalikuwa ni sehemu ya maamuzi magumu ambayo Watanzania walitakiwa kukaa chonjo kuyasubiri.
Lakini, siku chache baada ya ahadi hiyo ya Rais Kikwete, aliyoitoa wakati wa semina elekezi ya viongozi waandamizi wa serikali iliyofanyika Ngurdoto mkoani Arusha, Waziri Mkuu alizuru eneo la Kunduchi ambalo lilikuwa maarufu kwa uchimbaji wa mawe na kokoto jijini Dar es Salaam.
Shughuli katika eneo hili ilikuwa inatishia mazingira kwa kiasi kikubwa na kwa hakika iwapo uchimbaji huo ungeachwa uendelee, leo hii hali ya barabara ya Bagamoyo ingekuwa tofauti na ilivyo.
Viongozi katika ngazi ya mkoa walikuwa wametoa maagizo kadhaa kuhusiana na usitishaji wa shughuli katika eneo hilo. Watu walishafikia hatua ya kuamini kuwa wachimba kokoto hao wasingeweza kuondoka na wangeendelea na shughuli zao bila kujali kuwa wanaharibu mazingira na kutishia uhai wa barabara hiyo muhimu.
Lowassa alipofika katika eneo hilo, alitoa amri kuwa wachimba kokoto hao waondolewe katika eneo hilo haraka iwezekanavyo.
Lowassa alisema kuwa mazingira na barabara hiyo ni bora sana kwa taifa kuliko shughuli hizo za uchimbaji kokoto katika eneo hilo, akaagiza kuwa wachimba kokoto hao watafutiwe eneo jingine ambako wataendelea na shughuli zao.
Hilo lilifanyika, na leo hii suala la wachimbaji kokoto hao na ung’ang’anizi wao wa eneo hilo limebakia kuwa historia.
Ingawa siku za mwanzo walipinga, lakini serikali ilipobaki ‘ngangari’ walijua kuwa hawana lao, polepole wakalazimika kuyazoea mazingira mapya na leo wanaendelea na kazi zao bila matatizo.
Suala la kuwahamisha wachimba kokoto hao halikuwa la kitaifa. Halikustahili waziri mkuu kuingilia kati na kutoa amri.
Lakini lilitoa nafasi kwa Lowassa kuwafunza viongozi wa chini yake ni nini kilichomaanishwa na Rais Kikwete aliposema maamuzi magumu.
Kuwaondoa watu hao ilikuwa ni moja ya maamuzi machungu kwa watu zaidi ya 3,000 ambao walikuwa wanaendesha maisha yao kwa kutegemea sehemu hiyo.
Lowassa aliwaonyesha viongozi wa mkoa nini walitakiwa kufanya kama sehemu ya maamuzi magumu. Hilo halikuwa lake lakini ilikuwa ni nafasi ya kuwafundisha viongozi wengine katika ngazi mbalimbali kuwa jasiri wa kufanya maamuzi magumu.
Inasikitisha kuwa hadi hii leo, hakuna jambo lolote kubwa ambalo viongozi wa Dar es Salaam wamelifanyia maamuzi na kuhesabika kuwa ni maamuzi magumu.
Lipo suala la kuwahamisha wafanyabiashara ndogondogo kutoka katika mitaa ya jiji na kuwaweka katika maeneo yaliyotengwa rasmi kwa ajili yao.
Sidhani kama hilo linapaswa kuwa ni sifa kwa viongozi wa Dar es Salaam kwa sababu walikuwa wanatekeleza maamuzi yaliyofanywa na Lowassa kwamba, si tu Dar es Salaam, bali miji yote nchini inapaswa kuwa katika mpangilio.
Aliagiza kuwa wafanyabishara wote wanaofanya shughuli zao katika mitaa na kuleta bughudha, waondolewe. Kwa Dar es Salaam, aliagiza pia kuwa uongozi wa jiji uchukue hatua za kulipendezesha jiji. Hili lilikuwa ni agizo la Lowassa, haiyumkini kwamba viongozi wa Dar es Salaam wajichukulie ‘ujiko’ kuwa yalikuwa ni maamuzi yao magumu.
Kama ambavyo viongozi wa Dar es Salaam wasivyoweza kujichukulia sifa kwa maagizo ya Lowassa, Lowassa naye hastahili kupata sifa kwa hayo kwa sababu kufanya hivyo ni kumdhalilisha.
Masuala aliyoyafanyia maamuzi magumu yalikuwa ya chini yake, si saizi yake hata kidogo. Sana sana alichokifanya ni kutoa fundisho kwa walio chini yake kuwa ni nini wanachotakiwa kufanya katika suala la kutoa maamuzi magumu.
Ukiachana na magizo hayo ya Lowassa, jambo jingine kubwa ambalo limetolewa maamuzi na usimamizi wake ukatekelezwa kwa usimamizi wa karibu ukiambatana na malalamiko makubwa ni kuhusiana na utunzaji wa mazingira.
Yapo maamuzi makubwa mawili ambayo hadi hii leo yanabaki kuwa ya kupigiwa mfano. Uamuzi wa kuwaondoa wafugaji waliokuwa wametamalaki katika bonde la Ihefu, mkoani Mbeya pamoja na uamuzi wa kuchukua hatua za kupunguza uzalishaji, uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki, ili kuyanusuru mazingira.
Maamuzi hayo, hata yalipotangazwa, yalibezwa na baadhi ya watu wakidai kuwa ni jambo lisilowezekana. Lakini kwa ujasiri mkubwa, Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo ndiyo ilitoa tangazo hilo, ililisimamia suala hili na hivi sasa matokeo yake yanaonekana.
Baada ya wafugaji kuhamishwa Ihefu, hali ya mazingira, iliyokuwa imezorota kwa kiasi kikubwa kuanzia Ihefu mpaka ukanda wa pwani, imeanza kuimarika na sasa, licha ya lawama zilizokuwa zimetolewa wakati wa zoezi, wananchi wanaanza kuona busara za maamuzi hayo.
Lakini dalili hizo ni rasharasha tu, matokeo mazuri ya hatua zinazochukuliwa sasa zitaonekana miaka kadhaa ijayo. Hili linaweza kueleweka zaidi na Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Profesa Mark Mwandosya, ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa mazingira.
Profesa Mwandosya anaelewa kuwa mazingira ni suala ambalo halifai sana kwa mwanasiasa, kwani maamuzi na hatua zake zinamsababishia achukiwe na watu wengi.
Alilieleza hili wiki iliyopita wakati Mbunge w Morogoro Mjini, Dk. Nibuka Mzeru, alipokuwa anang’ang’a wapiga kura wake wasiondolewe kwenye safu za milima ya Uluguru.
Suala ya uzuiaji wa mifuko ya plastiki limekuwa la kupigia mfano hadi nchi za Kenya na Uganda zimeamua kuchukua hatua za kibajeti kama zilizochukuliwa na Tanzania mwaka jana ili kuyanusuru mazingira yao nao.
Ukiachana na hilo, kubwa ambalo limefanywa katika ngazi ya Serikali Kuu, hakuna jambo jingine kubwa la kupigia mfano, ambalo linaweza kuwekwa katika kundi la maamuzi magumu ambayo yanafanywa na watawala wetu.
Lakini mambo yanayohitaji maamuzi magumu yapo, yamejaa tele. Kinachoshangaza kuwa ni kwa nini watawala hao hao, ambao ndio waliowataka wananchi wakae chonjo, wamesita ghafla na hivi sasa wanaonekana kana kwamba wamesahau kuwa wanatakiwa kuyafanya hayo maamuzi magumu ambayo yanasubiriwa kwa hamu na wananchi wanaotaka mabadiliko.
Ilitarajiwa kuwa maamuzi magumu yaliyozungumziwa, hayatawadhuru wananchi peke yao, bali wale wote ambao wamekuwa wakikwamisha juhudi za serikali kuwaletea wananchi maisha bora. Ilitarajiwa kuwa maamuzi hayo yatawahusu pia wabadhirifu wa mali na fedha za umma ukiwamo muda.
Ilikuwa ni matumaini ya watu kuwa maamuzi magumu yatawapitia pia watu waliolisababishia taifa hasara kutokana na kusaini mikataba ambayo leo imegeuka kuwa mzigo usiobebeka kwa urahisi na mpiga kura.
Na pale Rais Kikwete alipotembelea Wizara ya Fedha na kuonyesha nia yake ya kumpatia ‘meno’ Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alionyesha kuwa amepania kuwakomesha wabadhirifu.
Alipewa ripoti ya CAG na mara moja kuitisha kikao cha Baraza la Mawaziri, watu wakaanza kukaa mkao wakusikilizia kitakachowapata walioonyeshwa kuwa na matumizi mabaya katika ripoti hiyo. Kwa bahati mbaya, watu wanaendelea kusubiri hadi leo.
Na inavyoonekana wataendeklea kusubiri sana, ukitilia maanani kauli ya CAG kuwa ripoti yake haimaanishi kuwa kuna ubadhirifu serikalini. Hilo lilikuwa bao la kisigino na kwa kauli hiyo, CAG alithibitisha kuwa ahitaji meno.
Upitiaji wa mikataba ya miradi ya uchimbaji madini imegeuka kuwa wimbo wa kisiasa. Ile hoja kwamba nchi inaibiwa, inajibiwa na hesabu za wawekezaji kuilipa serikali kiasi kidogo cha fedha, ambacho hakilingani na rasilimali ambayo Watanzania wameitunza kwa miaka mingi.
Yapo mengi, lakini haya ni machache tu ambayo yanasubiri maamuzi magumu kutoka kwa watawala ili kuiweka nchi katika mstari kuelekea maisha bora kwa kila Mtanzania.