SIKU chache baada ya Kampuni ya Khaisa Enterprises Ltd kufungua kesi ya madai ya fidia ya sh bilioni 16.8 dhidi ya serikali kwa madai ya kuvunjwa kwa mkataba wa kununua helikopta sita za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, imeibuka na kuiponda kampuni hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Abel Mwaisumo, alisema wizara yake iliamua kuachana na kampuni hiyo baada ya kubaini kuwa na mwenendo usiofaa wa kazi.
Hata hivyo, Mwaisumo alikiri kuwa, ni kweli jeshi lilikuwa na mahitaji ya helikopta kwa ajili ya shughuli zake za kiulinzi na huduma kwa taifa, lakini baada ya kubaini kuwa hali ya uchumi haikuwa nzuri, walisitisha zoezi hilo.
Alisema mradi huo ulisitishwa kutokana na kuwa wa gharama kubwa kuliko uwezo wa wizara, hali iliyoifanya serikali kutafuta wafadhili wanaoweza kugharamia mradi huo.
Alifafanua kuwa, hali ya ukata iliendelea ambapo Eurocopter walifahamishwa rasmi kwa barua, na wao wakapendekeza kupunguza idadi ya helikopta wanazohitaji kulingana na uwezo wa jeshi hilo kifedha.
Alisema pamoja na hilo, walimchunguza Khaisa Enterprises wakagundua ni Mtanzania, lakini si mzalendo kweli, kwani ilionekana bei za manunuzi ya helikopta hizo zilikuwa na utata.
“Tulimchunguza na kugundua si Mtanzania kweli kweli, tulikuta mambo mengine tofauti na sisi tulivyotaka, na kugundua kuwa nyendo zake si nzuri,” alisema Mwaisumo.
Alisema kuwa baada ya kugundua hali hiyo na kampuni hiyo kufuatilia mradi huo mara kwa mara jeshini kiasi cha kukiuka maadili ya utendaji wa kazi, uongozi wa wizara ulitoa uamuzi wa kuifahamisha Eurocopter kwamba mradi huo umefutwa.
Alisema walimwandikia barua Khaisa Enterprises kuwa walikuwa na vikwazo vya kifedha na hivyo hawatakuwa tayari kununua helikopta hizo na baadaye zabuni hiyo ikachukuliwa na Kampuni ya Agusta.
Mwaisumo alisema wanashangaa baada ya taarifa hiyo kampuni hiyo ilianza kudai inataka ifidiwe na serikali gharama ambazo hawazijui.
Aliongeza kuwa, kutokana na kitendo cha kampuni hiyo kukipaka matope chombo hicho cha wananchi, walikuwa na uwezo wa kuifungulia mashtaka, lakini waliamua kuiacha kwa kujua kufanya hivyo ni kuimaliza.
Alisema misingi na taratibu za ununuzi wowote wa vifaa vya kijeshi, umeainishwa katika sheria za kijeshi na vyombo vingine vya kitaifa, zinazolenga katika kuboresha uwazi.
Alhamisi ya wiki iliyopita, kampuni hiyo ilifungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, ikitaka ilipwe fidia ya gharama.
Wadaiwa katika kesi hiyo namba 74 ya mwaka 2007 ambayo bado haijapangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa, ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa hati ya madai, fidia hiyo ni sawa na asilimia nane ya kamisheni ya mauzo ya helikopta waliyokubaliana kati ya Kampuni ya Khaisa na JWTZ.
Mlalamikaji katika kesi hiyo, anataka alipwe fidia kutokana na kuvunjika kwa makubaliano ya awali ya kutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu baina yake na Kampuni ya Eurocopter ya Ufaransa na JWTZ.
Pia fidia ya kiasi hicho cha fedha inatokana na gharama za usafiri alizozifanya mlalamikaji nchini Ufaransa, Marekani, Afrika Kusini na Falme za Kiarabu kwa lengo la kuangalia helikopta zilizofaa kununuliwa na serikali kwa ajili ya jeshi hilo.
Kwa mujibu wa hati hiyo, mlalamikaji akiwa katika hatua za mwisho kukamilisha kazi yake, timu ya wataalamu toka ofisi ya Katibu wa Wizara ya Ulinzi, ilikwenda Ufaransa kufanya uchunguzi na kuziona helikopta hizo kabla hazijanunuliwa.
Anadai baada ya uchunguzi kufanywa, wataalamu hao walikubali kuingia mkataba wa manunuzi ya helikopta aina ya COUGAR AS523 multi-role kwa ajili ya shughuli za kiraia na kijeshi na roketi 1,200.
Mlalamikaji anadai kuwa wakati kazi ya utekelezaji ikianza, alipokea taarifa toka kwa mdaiwa wa kwanza ambaye ni JWTZ, kwamba kampuni nyingine ipo kwenye harakati ya kufanya kazi kama yake.
Hata hivyo, alisema barua haikujua jina la kampuni hiyo mpya ambayo ilikuwa ikifanya kazi ya kutafuta helikopta. Hati hiyo ya madai inasema kuwa, kampuni hiyo mpya ilikwenda nje ya nchi na kununua helikopta nne ambazo awali zilikataliwa na wadaiwa kwa madai kwamba hazifai kwa matumizi ya jeshi.
Aidha, anadai kubaini kwamba, helikopta hizo zilinunuliwa kwa gharama kubwa ya dola milioni 9.263 kwa kila moja, tofauti ya bei ambayo mlalamikaji alikuwa amekubaliana na JWTZ kwamba zingenunuliwa kwa dola milioni 4.7.