MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), imepanga kukutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Matumizi ya Maji, Nishati na Mazingira (EWURA), ili kupanga mikakati ya pamoja ya kuwabana wauzaji wa mafuta kupunguza bei ya nishati hiyo.
Baada ya kusomwa kwa bajeti ya serikali na kuonyesha ongezeko la kodi katika mafuta ya petroli na bidhaa zake, bei ya mafuta ilipanda ghafla na kuzusha hofu miongoni mwa wananchi kuhusiana na ughali wa maisha.
Hatua ya taasisi hizo mbili kukutana, imekuja baada ya baadhi ya mabasi ya abiria ya mikoani kupandisha nauli huku wamiliki wa mabasi na daladala nao wakiwasilisha mapendekezo ya kupandisha nauli, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ya dizeli na petroli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Mawasiliano wa Umma wa SUMATRA, David Mziray, alisema kuwa, mazungumzo hayo yatalenga kuhakikisha bei ya mafuta katika vituo vinavyouza rejareja inapungua na pia kuwa na bei ya pamoja katika vituo vyote.
“SUMATRA imeshawasiliana na EWURA kuhusu kufanya majadiliano hayo ili kuangalia ni jinsi gani inaweza kudhibiti vituo vyote vilivyopandisha mafuta ambayo ndiyo sababu kubwa ya mabasi kutaka kupandisha nauli,” alisema Mziray.
Mziray alikiri SUMATRA kupokea maombi kutoka kwa Chama cha wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani (TABOA) na Chama cha wamiliki wa daladala (DAKOBOA) ya kutaka kupandisha nauli.
Alisema jana maofisa wa SUMATRA walikutana kujadili mapendekezo hayo, nia ikiwa ni kuchanganua ili kupata kiasi cha nauli mpya kinachofanana na mazingira ya hali za maisha za wananchi wengi.
Hata hivyo, SUMATRA haikuweka wazi kuhusu kiasi ambacho wamiliki wamependekeza kiongezwe.
“Hayo yanajadiliwa… mpaka kikao kijadili tutatoa taarifa yetu ni kiasi gani kilitakiwa kiongezwe… kwa sasa siwezi kusema lolote, nitakuwa nimeingilia kikao ambacho bado hakijasema lolote,” alisema Mziray.
Aidha, alisema kuwa mabasi saba yaliyobainika kupandisha nauli kinyemela yameandikiwa barua ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Wakati taasisi hizo zikifikiria kuchukua hatua, tayari nauli za mabasi yanayosafiri kwenda mikoani zimeshapanda.
Utafiti uliofanywa na Tanzania Daima ulibaini kuwa, nauli za mabasi ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza zimepanda kutoka sh 43,000 hadi sh 55,000, Dar es Salaam - Mbeya kutoka sh 20,000 hadi sh 25,000, Dar es Salaam - Shinyanga kutoka sh 33,000 hadi sh 45,000, Dar es Salaam - Dodoma kutoka sh 7,000 hadi sh 15,000, Dar es Salaam kwenda Morogoro kutoka sh 3,000 hadi sh 5,000.
Dar es Salaam-Ifakara kutoka sh 10,000 hadi sh 13,000, Dar es Salaam Bukoba kutoka sh 60,000 hadi sh 78,000. Hata hivyo yapo baadhi ya mabasi ambayo hadi hivi sasa bado hayajapandisha nauli.