WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema wala rushwa walioponyoka kunaswa siku zilizopita, mwisho wao umewadia.
Amesisitiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Nne, haina suluhu na wala rushwa wote.
Waziri Mkuu alisema hayo katika hotuba ya bajeti ya ofisi yake ya mwaka 2006/2007 aliyoiwasilisha bungeni juzi.
Alisema serikali kwa kushirikiana na wahisani na mashirika yasiyo ya kiserikali, itahakikisha Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa, unatekelezwa.
“Katika mwaka 2006/2007, awamu ya pili ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa utakaozihusisha halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji na sekta binafsi, utaanza.
“Napenda kusisitiza kuwa serikali haitakuwa na suluhu na watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. Kama kuna aliyeponyoka kubanwa huko nyuma, basi ni vyema sasa akabadilika kwa kufungua ukurasa mpya wa maisha,” alisema.
Waziri Mkuu alizungumzia pia Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF), kwa kusema unafanyiwa maboresho ili uanze kulipa wanachama wake mafao ya pensheni.
“Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, kazi hiyo sasa imekamilika, hivyo serikali inatarajia kuwasilisha katika Bunge hili, muswada wa sheria kuunda Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa.
“Ili kuhakikisha kwamba mafao na maslahi ya wafanyakazi wa Serikali za Mitaa yanaboreshwa, serikali imekubali kimsingi kutoa kiasi cha sh bilioni 107.3 kama ruzuku kwa mfuko huu.
“Kiasi hicho kitatolewa kwa awamu 10 kuanzia mwaka 2007/2008 na kitawawezesha wafanyakazi wanachama wa mfuko kuwa na sifa ya kulipwa mafao yao ya pensheni kwa kuzingatia muda wao wa ajira katika Serikali za Mitaa,” alisema.
Katika hotuba hiyo, serikali ilitangaza mkakati wa kufufua kilimo ikiwamo hatua za kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ya maji ya mvua.
Pia serikali imetenga sh milioni 500 zitakazotolewa kwa kila mkoa kukopesha wananchi wenye nia ya kuanzisha miradi ya kujiondolea umasikini.