MKAZI wa Kijiji cha Mwamalili, wilayani Shinyanga, Mande Manyanya (22), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi akiwa msibani.
Manyanya, anadaiwa kumuua mama yake, Wande Bulungu (60) kwa kutumia mapanga. Mama huyo alikuwa kwenye msiba wa mama yake mzazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Shaibu Ibrahimu, alisema Manyanya alimuua mama yake kwa kumtuhumu kumfunga uzazi mkewe. Tukio hilo lilitokea Julai mosi mwaka huu, saa moja usiku katika Kijiji cha Ihapa, Wilaya ya Shinyanga.
Alisema tukio hilo lilitokea wakati mama huyo akiwa amelala na wanawake wengine nje ya nyumba iliyokuwa na msiba.
“Katika shambulio hilo, Wande alikatwakatwa kwa mapanga na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake… alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga alikolazwa na siku iliyofuata alifariki dunia,” alieleza kamanda huyo wa polisi na kuongeza kuwa, muuaji huyo yupo mikononi mwa polisi.
Kamanda Shaibu alieleza kuwa, baada ya kuhojiwa na polisi, mtuhumiwa alikiri kuhusika na mauaji hayo, akidai kuwa mama yake alimloga mke wake kwa kumfunga kizazi.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo alisema mama yake huyo pia alisababisha kuvunjika kwa ndoa ya dada yake kwa mumewe.
Alidai, katika maelezo ya mtuhumiwa huyo kwa polisi, alisema mpango wa mauaji hayo ulifanywa kwa ushirikiano na shemeji yake aliyemlipa sh 10,000 na panga, ili akamilishe azma ya kumuua mama huyo kwa imani za kishirikina.
Kamanda huyo, alisema polisi inaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.