Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Kombani atoa agizo kwa halmashauri
http://www.habaritanzania.com/articles/3944/1/Kombani-atoa-agizo-kwa-halmashauri
By Habari Tanzania
Published on 07/6/2007
 
NAIBU Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani, ameziagiza halmashauri ambazo bado hazijatekeleza agizo la kutoa asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya mifuko ya mikopo kwa vijana na wanawake zifanye hivyo mara moja na kumpelekea taarifa za utekelezaji ofisini kwake kila baada ya miezi mitatu.

na Peter Nyanje na Rachel Chizoza, Dodoma

NAIBU Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani, ameziagiza halmashauri ambazo bado hazijatekeleza agizo la kutoa asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya mifuko ya mikopo kwa vijana na wanawake zifanye hivyo mara moja na kumpelekea taarifa za utekelezaji ofisini kwake kila baada ya miezi mitatu.

Alitoa agizo hilo baada ya kubainisha kuwa takwimu za mwaka 2005/06 zinaonyesha kuwaa halmashauri nyingi zilikuwa hazijatekeleza agizo hilo. Alisema halmashauri 36 kutoka mikoa 16 nchini hazikuchangia kabisa mfuko huo na halmashauri 15 kutoka mikoa tisa zilichangia kiasi kidogo.

“Kwa mara nyingine, naziagiza halmashauri ambazo hazijachangia kikamilifu kutekeleza agizo hilo la kutenga asilimia kumi ya mapato yake kwa ajili ya mifuko ya wanawake na vijana,” alisema wakati akijibu swali la Mbunge wa Koani, Haroub Masoud (CCM).

Aidha, Kombani alivitaka vikundi mbalimbali vya vijana na wanawake, vilivyokopa fedha kutoka katika mifuko hiyo kurejesha mikopo hiyo, ili na wenzao nao wapate fursa ya kukopa.

Alizitaka halmashauri ambazo zilifanya vizuri katika kuchangia mifuko hiyo kuwa ni Manispaa za Ilala, Morogoro, na Kinondoni, majiji ya Mbeya na Dar es Salaam pamoja na Wilaya za Bukombe, Kwimba, Mbeya, Kashama na Kilombero.