Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Jamii  »  Kwa nini tunasherehekea kupeleka madaraka kwa wananchi? (2)
Kwa nini tunasherehekea kupeleka madaraka kwa wananchi? (2)
By Habari Tanzania | Published  07/6/2007 | Jamii | Unrated
WAKATI tunasherehekea Siku ya Serikali za Mitaa, ni lazima tuzame katika tafakuri na kuendelea kuufahamu zaidi mfumo huu mpya.

Mwaka huu ni sherehe ya tatu, tangia sherehe hizi zilipoanzishwa mnamo mwaka 2005.

Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa na hasa dhana nzima ya Upelekaji wa Madaraka kwa Wananchi unazua maswali, utata na wasiwasi miongoni mwa wadau.

Kwa mwanachi wa kawaida anayeifahamu Katiba ya taifa letu na mbaye amekuwa akifuatilia mfumo wa utawala wa Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, hawezi kuzungumzia ‘Maboresho’ bali mapinduzi katika mfumo wa Serikali za Mitaa na Serikali Kuu. Nitaelezea baadaye.

Kwa mwananchi wa kawaida ambaye hajui katiba, hana habari kabisa kwamba taifa huongozwa na katiba. Hajawahi kuiona wala kuigusa katiba ya taifa lake.

Hajashirikishwa hata mara moja kutengeneza katiba ya nchi yake. Hajui kabisa kwamba serikali inawajibika kwa wananchi na wazo hili halijaingia akilini mwake hata siku moja.

Akipelekewa madaraka, si maboresho bali ni mapinduzi makubwa! Asilimia kubwa ya Watanzania ni wa aina hii. Ingawa sina takwimu lakini matukio mbalimbali yanayojitokeza yanayovunja katiba, hakuna anayejitokeza kuuliza wala kuhoji.

Mfano katiba yetu inataja kwamba : “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.” (Ibara 3(1) ). Ujamaa umezikwa, hakuna anayeuliza wala kuhoji.

Bado kuna hali ya watu kufikiri kwamba vyama vya upinzani ni usaliti. Lakini kumbe vyama hivi vipo kwa mujibu wa katiba.

Hivyo ni muhimu madaraka yanapopelekwa kwa wananchi, iwe wazi kabisa kwamba katiba ni msingi wa hatua zote zinazochukuliwa na viongozi wetu katika harakati za kuleta maendeleo. Hili linahitaji mapinduzi makubwa katika fikra na utendaji wa wananchi na viongozi pia.

Kwa viongozi na watendaji waandamizi katika ngazi mbalimbali za Serikali, dhana nzima ya upelekaji wa madaraka kwa wananchi ni mapinduzi na wala si maboresho.

Mpango wa uboreshaji wa mfumo wa serikali za mitaa unahimiza ushirikishwaji, utawala bora, uwazi wa kutangaza matatizo na mafanikio ya halmashauri, ushirikishwaji wa wadau katika mipango ya maendeleo.

Hii inaleta wasiwasi kwa mambo mengi yaliyokuwa yakifanyika kichwa chini miguu juu.

Mfano wafanyakazi hewa ambao mishahara yao ilikuwa ikilipwa kila mwezi na kuiingia mifukoni mwa watu wasiojulikana, rushwa, upendeleo katika kutoa ajira, matumizi mabaya ya fedha, uzembe n.k.

Wadau wanaoshinikiza kushirikishwa katika mipango ya maendeleo wanaonekana kama wachochezi wa kuwafumbua wananchi macho ili waache kulipa kodi na kuanzisha utamaduni wa kuiwajibisha serikali.

Hivyo viongozi na watendaji waandamizi katika ngazi mbalimbali za Serikali wanakumbwa na hofu ya kupunguzwa kazini, kushitakiwa na pengine kufungwa.

Mpango wa uboreshaji wa mfumo wa serikali za mitaa na serikali kuu ni harakati za kuupindua mfumo uliokuwa kichwa chini miguu juu, ili uwe miguu chini na kichwa juu. Haya si maboresho. Ni mapinduzi!

Kwa wahisani, ambao wanasaidiana na serikali yetu kuendesha mradi huu wa mpango wa uboreshaji wa mfumo wa serikali za mtiaa Tanzania Bara, wanauona mradi huu (programu) kama maboresho.

Wahisani wanatoka kwenye nchi zilizoendelea. Nchi hizi zinaheshimu sana katiba na kuifuata. Watu wote katika nchi zao wanaijua katiba. Wanaweza kununua vitabu vya katiba katika maduka ya vitabu au kuisoma katiba katika mitandao na kwenye magazeti.

Kwao katiba ni mali ya wananchi na kila mtu ana uhuru wa kuwa nayo. Hawa wahisani wakiisoma katiba yetu wanayakuta mambo yote yanayosisitizwa katika programu nzima.

Mfano dhana ya upelekaji wa madaraka kwa wananchi, si jambo jipya. Lina msingi katika katiba yetu Ibara ya 8. Na mfumo wa Serikali za Mitaa uliopo unatokana na dhana ya madaraka kwa umma. Katika nchi yetu suala la madaraka kwa umma lina msingi wake katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo katika Ibara 145 na 146 inaeleza kuwa:

“ 145 (1) Kutakuwa na vyombo vya Serikali za Mitaa katika kila mkoa, wilaya, miji na kijiji ambavyo vitakuwa vya aina na majina yatakayowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge au Baraza la Wawakilishi.

(2) Bunge au Baraza la Wawakilishi, kwa kadiri itakavyokuwa, litatunga sheria itakayofafanua utaratibu wa kuanzisha vyombo vya Serikali za Mitaa, miundo na wajumbe wake, njia za mapato na utaratibu wa utekelezaji wa shughuli.”

“146 (1) Madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao za nchini kote kwa ujumla.

(2) Bila ya kuathiri maelezo ya jumla yaliyomo katika ibara hii, kila chombo cha Serikali za Mitaa, kwa kuzingatia masharti ya sheria iliyokianzisha, kitahusika na shughuli zifuatazo:

(a) kutekeleza kazi za Serikali za Mitaa katika eneo lake.

(b) Kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi.

(c) Kuimarisha demokrasi katika eneo lake na kuitumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi.”

Hivyo kwa wahisani, kinachofanyika sasa hivi ni maboresho. Ni kwamba mifumo ipo labda utekelezaji ndo ulikuwa mbovu. Kinachohitajika ni kufanya maboresho.

Sitaki kuwa Thomas, lakini imani yangu ni kwamba kadri watakavyoendelea kushiriki katika programu hii ndivyo watakavyogundua kwamba kazi si kuboresha jengo bali ni kujenga upya!

Kama ni wa kweli na wanaifanya kazi hii bila unafiki, kipindi walichokimaliza katika programu hii kinatosha kuwafumbua macho na kuona kwamba tatizo ni kubwa kuliko linavyoonyeshwa kwenye makaratasi.

Kwa upande wetu programu hii ni mapinduzi, maana ni mambo yaliyokuwepo lakini kichwa chini miguu juu! Mbaya zaidi ni kwamba na macho yetu yalikuwa yamefumbwa, bila kutambua hali tuliyokuwemo! Hivyo kazi iliyo mbele yetu ni kubwa: Kuondoa upofu ili tuweze kuusimamisha mwili katika hali yake ya kawaida.

Ndiyoo maana inashangaza kuona watu hawaitaji programu hii inayolenga kumkomboa Mtanzania. Hatujasikia vya kutosha juu ya programu hii – vyombo vya habari vingekuwa vinarudia na kurudia hadi masikio yakauma.

Tunahitaji kusikia na kuona mengi juu ya programu hii – maana kusema kweli Serikali za mitaa ni msingi wa maendeleo. Zinapoboreshwa au kufanyiwa mapinduzi makubwa, ni lazima kila mwananchi kufahamu hatua zote tunazozipitia na ni muhimu wananchi wote kushiriki.

Vyombo vya habari ni muhimu sana kwa jambo hili la kuhabarisha na kuelimisha.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.