Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Barua kwa vijana wa Tanzania
Barua kwa vijana wa Tanzania
By Habari Tanzania | Published  07/6/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

SALAMU vijana!

Leo nimeona niwasiliane nanyi kupitia safu hii. Wengi wenu mnanifuatilia vipindi vyangu vya luninga na kwenye safu hii hasa mfululizo wa makala saba zilizotangulia kuhusu haja ya chama tawala kuwa na taswira mpya.

Naona ile ya mwisho iligubikwa na msiba wa kuondokewa na yule binti - kijana mwenzenu, hivyo huenda hamkuipitia. Sasa sijui kama jina la mtu aliyeitwa Shaaban Robert mnalikumbuka au mmelisoma au kusoma kazi zake mahali.

Mtu huyu alikuwa mwanafalsafa. Kwa kweli miongoni mwa wanasalfa wachache sana katika historia ya nchi hii. Alikuwa mshairi. Alipoondokewa na mkewe aliandika shairi ambalo ubeti wa kwanza ulisema hivi:

Amina umejitenga
Kufa umetangulia
Kama ua umefunga
Baada ya kuchanua
Nakuombea mwanga
Peponi kukubaliwa….

Nadhani Mohamedi Mpakanjia naye angekuwa mshairi angeandika shairi kama hili baada ya kuondokewa na mkewe, Bi Amina.

Kwa kuwa dini zote zinasema kila kilichoumbwa kitaonja mauti, basi kilichobaki baada ya kuomboleza ni kumrehemu mwenzetu aliyetangulia. Baada ya hapo kutazama mbele.

Sasa nimekuwa nafikiri baada ya msiba huu wa kijana mwenzenu ni jambo gani ninyi vijana mkazanie ili mwendeleze pale alipoachia mwenzenu.

Tazameni vijana: kinachomwendeleza mtu kuishi duniani baada ya kuondoka ni fikra zake.

Ndiyo maana watu wanawakumbuka watu kama Shaaban Robert, Mwalimu Julius Nyerere, Mathias Mnyampala, Seithy Chachage na wengine kama hao.

Huyu wa mwisho, Chachage sasa katimiza mwaka mmoja tangu afariki dunia. Wiki hii hapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kumefanywa makongamano na maonyesho ya kumuenzi.

Watu kwa mamia wamejumuika pale chuoni kumkumbuka na kuainisha kile alichokiamini katika maisha yake. Wamefanya hadidu rejea za vitabu vyake na kazi zake mbalimbali.

Majira kama haya mwaka jana, mimi nilikuwa miongoni wa maelfu ya watu waliomiminika chuoni hapo baada ya kusikia habari za kifo chake.

Nilishangaa sana. Mtu huyu hakuwa ‘mheshimiwa’ mbunge au waziri. Hakuwa na mamlaka yoyote ya kidola. Sasa kwa nini watu walimiminika kwa wingi namna ile kumuaga alipofariki dunia?

Jibu ni rahisi: alikuwa na msimamo. Wakati wote alijitambulisha na wanyonge wa nchi yetu. Alijitambulisha na matabaka ya kihistoria ya ulimwengu huu: wakulima na wafanyakazi. Alikuwa na upeo mpana na mkubwa wa dunia hii tunayoishi; hivyo akang’amua haraka kwamba kumbe ‘utandawazi’ ulikuwa utandawizi!

Kumbe ‘soko huria’ haikuwa lolote na si chochote ila mfumo wa kuneemesha makabaila wa kimataifa.

Na hawa makabaila wa kimataifa walikuwa na makuwadi wao katika nchi kama zetu. Hakuishia hapo. Alitaka kuwaelewesha na wananchi wenzie. Ndipo akaandika kitabu – Makuwadi wa Soko Huria.

Nilipojiunga na maelfu ya Watanzania wenzangu majira kama haya mwaka jana nilipata somo moja. Kumbe mtu akisimamia fikra sahihi lazima ataenziwa na kuheshimiwa na watu wenzie kama ilivyojitokeza kwenye msiba wa Profesa wa wananchi, Seithy Chachage.

Lakini kuheshimiwa huku hakuji hivi hivi tu. Kunakuja kutokana na elimu ya mtu.

Kwa sababu mchango wa elimu kwa mtu ni kupanua maradufu uwezo wake wa kufikiri. Marehemu baba yangu, mimi nilimsikia akisema mara kwa mara: “Ujinga ni mzigo mzito kweli kweli!” Wakati naandika sentensi hii nacheka peke yangu! Ni kweli. Ujinga ni mzigo mzito sana.

Hebu fikiri: hivi unawezaje kumpa mtu kura yako kwa sababu kakukaribisha wewe kula pilau, tena mara moja kwa miaka mitano wakati mwenzio hiyo pilau anakula karibuni kila siku?

Unampaje mtu kura yako kwa kuwa tu kakutupia jola la kanga, kitenge au ka- Tsheti na kofia? Au kakupa bahasha ndani yake mna hela?

Hiyo hela ndiyo utu au thamani ya fikra zako wewe?

Nina hakika kama una elimu yako utajiuliza maswali mengi kuhusu ‘zawadi’ au ‘takrima’ hiyo. Kadhalika lazima utatafakari mara mbili kuhusu vibwagizo vya kampeni za uchaguzi ambavyo sipendi kuvirudia hapa nisije nikaeleweka vibaya!

Kama una elimu utakuwa na upeo mpana zaidi kutambua kwa mfano kwamba kukithiri kwa biashara ya dawa za kulevya ni moja ya athari za mfumo wa uchumi wa gulio tulionao ambapo watu binafsi matajiri ndiyo injini ya uchumi wa nchi.

Ni athari za kukosekana kwa mpaka baina ya masilahi ya mtu binafsi na ofisi ya uongozi ambapo kutengeneza pesa ni kitu kinachokubalika wakati wowote na popote bila miko!

Ukiwa na elimu makini utajua kwa mfano kuwa kukithiri kwa ukahaba ni kielelezo cha ufukara wa watu na kuibuka kwa kikundi cha wachache walio nacho na wengi wanaozidi kudidimia kwenye lindi la ufukara.

Kwa maana hiyo hutashangaa au hutakuwa na majawabu ya haraka haraka zinapokithiri taarifa za kutia mimba watoto wa shule.

Kwa hiyo vijana, mjitahidi sana popote pale mlipo mpate fursa ya kusoma. Mkiwa mmemaliza kidato cha sita, shahada ya kwanza au stashahada ya juu kama anayochukua kijana wangu, msiridhirike.

Na hata kama mmemaliza elimu ya msingi msikate tamaa pia. Watu husema msomi mzuri zaidi ni yule aliyejisomesha mwenyewe.

Na kusoma si kwenda shule peke yake. Msome magazeti, mtazame televisheni kuona wenzenu katika nchi nyingine wanatazama masuala yanayohusu jamii zao kwa mtazamo gani.

Mtazame mazingira ya pale pale mnapoishi. Kwa nini Sinza ni tofauti na Tabata Liwiti na Vingunguti karibu na dampo la taka. Nyumba za watu zimekaakaaje?
Shule za wadogo zenu wanazosoma kama Mchikichini Shule ya Msingi na Mnazi Mmoja, kwa nini ni tofauti na zile wanazosoma watoto wa matajiri?

Kwa nini mambo haya yanatokea katika jamii moja?

Mkianza kujiuliza maswali haya, mtakuwa mmeanza kufikiri, na huko chuo kikuu mkienda mtakwenda kunolewa zaidi tu!

Vijana, ‘Aluta Continua!’

• Makwaia wa Kuhenga pia anaongoza kipindi cha televisheni: ‘Je, Tutafika?’ Channel Ten.

E-mail: makwaia@bol.co.tz


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.