SERIKALI bado haijateua mzabuni wa kutengeneza vitambulisho vya taifa nchini na kwamba kazi hiyo itasimamiwa na taasisi ya vitambulisho vya taifa iliyoanzishwa nchini.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alieleza hayo katika mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, mjini Dodoma kumuaga Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bibi Judy O’Connor.
Akifafanua hoja kuhusu taratibu za utengenezaji wa vitambulisho vya taifa, Masha, alisema aliyeteuliwa ni mshauri wa kitaalamu kuhusu utengenezaji wa vitambulisho vyenyewe.
Alisema mshauri atatoa ushauri kuhusu aina gani nzuri ya kitambulisho, kama ni cha kadi ya plastiki au vinginevyo na aina gani za takwimu zitaingizwa kwenye kitambulisho hicho.
Kumekuwa na hoja mbalimbali kuhusu utengenezaji wa vitambulisho vya taifa ambavyo ndivyo vitakuwa vinavyomtambulisha Mtanzania. Miongoni mwa hoja hizo ni kwamba tayari amekwishateuliwa mzabuni.
Baadaye katika karamu ya chakula cha mchana katika Hoteli ya New Dodoma, Waziri Mkuu, Lowassa alimsifu Bibi O’Connor kwa kuwa mwakilishi mzuri wa Benki ya Dunia katika Tanzania.
Lowassa alisema katika kipindi cha O’Connor kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya pande hizo mbili na kwamba kuna miradi mingi ambayo Benki Kuu imeisaidia Tanzania.
O’Connor anaondoka nchini wiki hii baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka minne. Nafasi yake inachukuliwa na John Mcintire ambaye alifuatana na O’Connor Dodoma katika sherehe za kuagana.