Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Muungano majaribuni
Muungano majaribuni
By Habari Tanzania | Published  07/6/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
SERIKALI inamtafuta mshauri mwelekezaji atakayeishauri kuhusu mgawanyo wa mafuta yanayoonyesha dalili kubwa ya kugundulika nchini, kati ya Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar.

Hayo yalielezwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2007/08.

Dk. Hussein Mwinyi, alisema kuwa hivi sasa wizara husika, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), zimeandaa rasimu ya hadidu za rejea ambazo zitatumiwa na mshauri mwelekezi huyo katika kufanya kazi hiyo.

“Serikali zetu kwa kutambua umuhimu wa nishati hii kwa maendeleo ya taifa letu, zilikubaliana kuwa kabla ya kufanya maamuzi mengine, ni vema atafutwe mshauri mwelekezi ili aweze kushauri namna bora ya kulishughulikia suala hili kama linavyoshughulikiwa na nchi zilizoungana na zenye rasilimali ya mafuta,” alisema.

Kuhusu suala la muungano, waziri huyo alisema Ofisi ya Makamu wa Rais inaandaa ratiba ya vikao vya ushirikiano kwa ajili ya wizara, idara, taasisi na asasi za Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisema, lengo la vikao hivyo ni kujadili masuala ya kisekta, kubadilishana ujuzi, uzoefu, utaalamu, sera na uwakilishi katika vikao vya majimbo na kimataifa.

“Vikao hivi vimekuwa vikifanyika na taarifa kuletwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa lengo la kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi yanayofikiwa na kushauri ipasavyo,” alisema.

Alibainisha kuwa vikao hivyo vimesaidia kuongeza ushirikiano baina ya pande mbili za muungano katika sekta mbalimbali.

Aidha, aliainisha mikakati ya kutunza mazingira na kuliomba Bunge likubali kuidhinisha jumla ya sh 35,490,349,000 kwa ajili ya kugharamia shughuli za kawaida katika Ofisi ya Makamu wa Rais.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliochangia hotuba hiyo walihoji sababu za serikali kung’ang’ania mafuta na gesi ni suala la muungano lakini imeshindwa kuipatia Zanzibar mgawo unaotokana na gesi ambayo inazalishwa nchini.

Baadhi ya wabunge waliochangia waliishangaa serikali kushindwa kuigawia Zanzibar mapato yatokanayo na rasilimali nyingine zinazopatikana nchini kama vile madini na mazao ya maliasili.

Kheri Khatib Ameir (Matemwe-CCM), alisema Tanzania ina bahati kuwa na muungano ambao umedumu kwa miaka mingi na kutahadharisha hatari ya kuvunjika kwa muungano huo iwapo hautajengwa kwa moyo wa kizalendo.

Akionyesha kuwepo kwa dalili za kuudhoofisha muungano huo kwa sababu zisizo na msingi, mbunge huyo alihoji uhalali wa magari yanayosajiliwa Zanzibar kudaiwa kodi yanapoingia Tanzania Bara.

“Hivi hata magari ya Zanzibar kuingia Bara iwe kero ya muungano? Nalo hili linahitaji kufanyiwa vikao? Mali zetu mafuta na gesi, tutafute ‘expert’ (mtaalamu) wa kutushauri jinsi ya kugawana? Haiwezekani,” aliuliza Ameir.

Aidha, alitaka kero hizo zirekebishwe katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja ili kuwapa wananchi imani kuwa viongozi wao wamedhamiria kuuimarisha muungano.

Alisema, vitendo vya kuendeleza kero vinasababisha wabunge wanaotoka upande wa Zanzibar kusutwa na wapiga kura wao wakidaiwa kutokuwa na msimamo unaoonyesha kujali masilahi yao kwa Zanzibar.

Naye Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe-CUF), alisema kuwa mfumo wa ukusanyaji mapato, ni moja ya sababu zilizowakimbiza wafanyabiashara kuikimbia Bandari ya Zanzibar na kufanya uchumi wa Zanzibar kuporomoka.

“Tuliingia katika muungano kwa imani kubwa kabisa kuwa ninyi (Tanzania Bara) mpo karibu na sisi tupo karibu nanyi, lakini inashangaza kuwa ‘inflation’ (mfumuko wa bei) Zanzibar sasa umefikia asilimia 11,” alisema.

Bunge liliipitisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais jana jioni.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.