Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Slaa afufua mzuka wa Richmond tena
Slaa afufua mzuka wa Richmond tena
By Habari Tanzania | Published  07/6/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
MBUNGE wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), ameibua upya sakata la zabuni ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond Development Company (RDC) ambalo lilitangazwa kufungwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU).

Dk. Slaa aliliibua suala hilo wakati Bunge likiwa limekaa kama Kamati ya Matumizi, kupitia kifungu kwa kifungu, bajeti ya Ofisi ya Rais, ambayo ilipitishwa juzi jioni.

Mbunge huyo ambaye kwa wiki kadhaa sasa hoja yake dhidi ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuwa msumari wa moto, juzi tena alihoji ni kwa nini Waziri anayeshughulikia masuala ya Utawala Bora, alikubali suala hilo lifungwe, wakati hata uchunguzi uliofanywa na TAKURU ulibaini kuwepo kwa uzembe katika utoaji wa zabuni kwa Richmond.

Dk. Slaa, ambaye licha ya vikwazo kadhaa alijitahidi kujenga hoja zake, aliitaka serikali, kuileta ripoti hiyo ya TAKURU bungeni, ili wabunge waiangalie na kujadili uzembe unaotajwa ndani ya ripoti hiyo.

“PCB walifunga ule mjadala kwa kusema kwamba wamemaliza. Lakini, wakati wanafunga wakaeleza kwamba kuna mapungufu machache yameonekana katika taratibu zilizotumika. Sasa, kwa mtu anayesimamia shughuli za serikali kama mbunge, anapenda kujua haya mapungufu ni yapi!

“Waziri wakati wa kujibu anasema hili ni suala la kijinai jinai, kwa hiyo taarifa ile haiwezi kuwasilishwa bungeni. Lakini, mimi sina tatizo na hiyo sehemu ya kijinai, nadhani hata wakati tunatunga sheria ya PCB hilo pia tulilisema.

“Lakini, inapofika mahali kwamba kuna mapungufu ambayo wanasema kwenye lile tangazo walilotoa kwenye gazeti kwamba siyo tu upungufu, kuna uzembe pia ulitokea.

Sasa, nadhani taarifa zile zinaacha kuwa za kijinai, kuna element ya kiutendaji ambayo inaenda kwenye uzembe,” alisema Dk. Slaa.

Mbunge huyo alihitimisha kwa kumtaka Waziri Philip Marmo kulieleza Bunge namna ambavyo wabunge wanaweza wakaijadili ripoti hiyo baada ya kuletwa bungeni.

Hakuishia hapo kwani alikwenda mbali zaidi na kuuliza iwapo kweli taarifa hiyo ya TAKURU ilikuwa ni ya siri, basi ni kwa nini ilichapishwa kwenye magazeti badala ya kuwaamini wabunge.

“Naona hapa sasa kuna tatizo kwamba, PCB inaweza ikakwepa kutoa taarifa yake kwa vyombo vinavyosimamia serikali, lakini ikatoa taarifa ile kwa magazeti na Bunge halitakuwa tena na namna ya kuhoji,” alifafanua.

Akijibu hoja hiyo, Marmo alisema PCB muda wote inashughulikia masuala ya rushwa na rushwa ni vitendo vya jinai na mkondo wa matendo ya jinai hatimaye hufika katika hatua ya aidha mashitaka au uchunguzi kufungwa na kuelekea mahakamani na hata siku moja si bungeni.

“Narudia tena taarifa za PCB kwa asilimia mia moja zinahusiana na masuala au matendo ya jinai na mkondo wa matendo ya jinai hata siku moja hauwezi kuwa bungeni isipokuwa mahakamani,” alisisitiza.

Alisema kuwa iwapo mbunge au raia yeyote, ana ushahidi ambao anafikiri utaisaidia TAKURU au pengine taasisi hiyo haikufuatilia kwa makini, basi hazuiwi hata kufungua mashitaka binafsi (private prosecution).

Alisema kuwa taarifa hiyo si ya siri kwa maana ya siri ya Serikali na kwamba inaweza kujadiliwa mahali popote.

Hata hivyo, Dk. Slaa aliibuka tena akisema kuwa hakuridhika na majibu ya waziri akisema alichokuwa akihoji kilikuwa si suala la jinai bali ni uzembe ambao nao ni kosa kwa mujibu wa sheria ya rushwa.

Ingawa alikiri kuwa uzembe ni kosa, hata hivyo, Marmo alisimamia msimamo wake akimtaka mbunge huyo kama anafikiri kuna uzembe kwa jinsi suala la Richmond lilivyoshughulikiwa, kwa utaratibu wake anaweza kulileta bungeni.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.