WIKI iliyopita dunia ilishuhudia Uingereza ikimpata Waziri Mkuu mpya, Gordon Brown. Halikuwa ni jambo la kushtukiza kwa sababu tangu mwaka 1997 Waziri Mkuu aliyeondoka, Tony Blair, uvumi ulitanda kwamba viongozi hao walikuwa wamekubaliana jinsi ya kuachiana madaraka.
Kuna habari kwamba Blair na Brown walikubaliana kwamba waungane mkono katika kutafuta madaraka ya juu kabisa ya taifa hilo na kila mmoja angeongoza kwa kipindi chake.
Awali ilidaiwa kwamba Blair angekaa kwa vipindi vya miaka minne minne, na baadaye amwachie Brown ambaye kwa kipindi chote cha utawala wa Blair alishika nafasi ya waziri wa fedha.
Ingawa Blair hakuishia na vipindi viwili, aliwania kipindi cha tatu na kushinda uchaguzi, mwisho wa yote amemwachia madaraka Brown na kufanya fununu au uvumi ambao umetanda ndani na nje ya taifa hilo kwa ni jambo lililokuwako na hakika lililopangwa na viongozi hao ambao wamebadilisha kwa kiasi kikubwa historia ya taifa hilo, hasa kwa sera za nje.
Mtazamo wangu wa Blair na Brown wiki hii ulinirejesha kwenye picha ya mwaka 1995 kati ya Rais wa Tanzania wa sasa, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa. Viongozi hawa wakiwa vijana kwa maana ya siasa za Tanzania walikwenda Dodoma pamoja kwa kukodi ndege moja kuchukua fomu za kuomba tiketi ya kuwania urais kupitia CCM.
Ninakumbuka wakiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wa zamani, viongozi hawa walipoulizwa na waandishi wa habari nani alikuwa anamsindikiza mwenzake katika safari ya kusaka tiketi ya CCM kuwania urais walisema “tunasindikizana”. Jibu hilo halikuwa linawatosheleza sana waandishi wa habari waliokwenda uwanja wa ndege kuwasubiri (Kikwete na Lowassa) wakirejea kutoka Dodoma walikokuwa wamekwenda kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa na CCM.
“Tunasindikizana” ya mwaka 1995 ilikuja kuwa tunasindikizana kwa kipindi cha miaka 10 ya viongozi hao kujipanga kupata madaraka ya juu kabisa ya uongozi wa taifa hili.
Mafanikio hayo yalifanikishwa pamoja na mambo mengine na uundwaji wa mtandao wao ambao ulijipanga na hatimaye kushinda hata viongozi wa juu serikalini na kwenye chama ambao walikuwa wakiwania nafasi hiyo pia. Hawa ni kama Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Makamu Mwenyekiti wa CCM, John Malecela.
Kwa maana hiyo, “kusindikizana” kwa Kikwete na Lowassa hata sasa bado kunaonekana kuzidi kutanda hata kama mmoja ni bosi wa mwingine, kimkakati na uwajibikaji, kuna mwelekeo unaoonyesha kwamba wawili hawa bado wanasindikizana.
Si nia ya makala hii kueleza ni wapi wameonyesha kusindikizana kwa sababu mwisho wa yote Waziri Mkuu wa nchi amekula kiapo cha kumsaidia Rais kazi zake, na ndiyo maana ukimsikiliza kwa makini sana kila anapokwenda Lowassa jina la Rais Kikwete lipo karibu sana kinywani mwake.
Anajibidiisha kila wakati na kila mahali kuthibitisha kwamba anafanya kazi aliyotumwa na Rais, kwamba si Waziri Mkuu anayetaka kufanya kazi ili kumfunika rais wake.
Utendaji huu ukijidhihirisha kila wakati, swali moja linajitokeza kila wakati watu wanapomtazama Lowassa, nalo ni je, ya Blair na Brown yatajitokeza kwa Lowassa na Kikwete? Je, baada ya miaka 10 ya Kikwete ikulu kama Mungu atamjalia uzima na Watanzania watampa ridhaa kwa mara nyingine tena mwaka 2010, atampisha Lowassa?
Kama nilivyosema, yaliyotokea wiki iliyopita nchini Uingereza yanaweza kujitokeza hapa nchini baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wake. Haya yanawezekana, lakini pengine yatawezekana zaidi kama Lowassa atachanga karata zake sawasawa.
Nchini Uingereza Blair alipokuwa akifanya maamuzi yake ambayo hayakuungwa mkono hata na chama chake kama ya kuipeleka nchi vitani Iraq, au kuongeza ada ya elimu ya juu, watu walikuwa wakimtaja waziwazi Brown. Walikuwa wakimtaja kwa maana walitamani yeye ndiye achukue uongozi wa chama na hatimaye uwaziri mkuu. Hii ilikuwa na maana gani Brown kutajwa? Ilikuwa na maana kwamba, alionekana kwamba ni kiongozi bora zaidi kuliko bosi wake katika masuala fulani fulani hasa yale yaliyohusu sera za nje na uhusiano wa Uingereza na Marekani.
Kwa maana hiyo, kila wakati Waingereza walikuwa wanamwona Brown ni mbadala wa Blair. Ndiyo maana wiki iliyopita Brown alipokabidhiwa mikoba na Blair hakikuwa kitu kipya kwa maana ya jambo ambalo halikutarajiwa (a surprise). Kwa hiyo Brown wakati wote alifanya juhudi na bidii yote kuhakikisha kwamba anamsaidia bosi wake ili pengine kwa lolote litakalotokea makubaliano yao yasije kuvunjika.
Alikuwa ni Brown aliyewabadilisha mawazo wabunge watano kutoka Scotland mwaka 2004 dakika za majeruhi na kusaidia hoja ya Waziri Mkuu juu ya ongezeko la ada elimu ya juu kupitishwa na Bunge la makabwela la Uingereza kwa idadi ya tofauti ya kura tano tu. Ikumbukwe kwamba chama cha Blair, Labour, kilikuwa na wingi wa wabunge zaidi ya 100 kupita Conservative, kwa maana hiyo wabunge wengi wa Labour walipiga kura ya kukataa hoja (muswada) wa Waziri Mkuu wao.
Kwa hiyo Brown asingefanya kazi ya ziada usiku ule mwaka 2004 hakika serikali ya Blair ingekuwa katika shaka kubwa.
Kwa mfano huu, kitakachofanya makubaliano ya “kusindikizana” kwa Lowassa na Kikwete kuendelea kuwako hata baada ya 2015 ni jinsi aliye mdogo kwa madaraka atajibidiisha kuhakikisha kwamba, anamsaidia mkubwa asiumbuke. Kuumbuka huku ni kwa aina nyingi.
Kwa mfano miongoni mwa mambo ambayo sasa hivi watu wanatumia kuhukumu serikali ya awamu ya nne ni utekelezaji wa ahadi za Rais Kikwete wakati akiomba kura mwaka 2005. Moja ya ahadi zake kuu ni kuwapatia Watanzania wote maisha yenye neema tele.
Juni 14 mwaka huu yaani wiki mbili zilizopita serikali ya awamu ya nne iliwasilisha bajeti yake ya pili tangu iingie madarakani Desemba 2005. Katika kipindi cha miaka mitano cha utawala wake bado bajeti tatu.
Kwa maana hiyo kwa miaka mitatu ya fedha, au tuseme kwa kipindi cha miaka miwili na nusu hadi kwenye uchaguzi mwingine mwaka 2010, serikali hii ni lazima iweze kuonyesha kwa vitendo halisi kwamba, imeweza kutekeleza kwa kiwango kikubwa ahadi zilizotolewa na Rais akiomba kura.
Lowassa ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni anasikia vilio vya wabunge, wapo wanaosema wazi wazi kwamba wanaunga mkono hoja kwa sababu tu ya kubanwa na kanuni za nidhamu ya chama, vinginevyo wasingekubaliana na bajeti ya serikali ya mwaka huu wa fedha.
Hapa ndipo changamoto inaibuka kwamba ni kwa jinsi gani Lowassa anaweza kukaa mkao ambao watamtamani kuwa kiongozi wao mkuu baada ya Rais Kikwete, au hata pale Kikwete anapoteleza ni kwa jinsi gani Lowassa anakuwa chaguo kama Brown alivyokuwa kwa Waingereza.
Lowassa anapaswa kujitazama na kujihoji kama kweli haya yanayosemwa mitaani ni ya kweli kwamba anautaka urais baada ya Kikwete.
Kujitazama huku ni kujiweka kwenye nafasi ambayo wananchi watasema “ah! Afadhali huyu” huku kutakuwa ni kwa yeye kuwatumikia wananchi kwa dhati. Huku kutakuwa ni kuacha kuwakingia kifua watuhumiwa wa mali ya umma hata kama hawajasafishwa na vyombo halali vya kisheria (mfano sakata la Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali), mfano ni hoja ya kuvurugwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, hasa idara ya wanyamapori ambako inadaiwa Lowassa ana mikono yake kwa kumlinda mtu wake.
Lowassa hana budi kuanza kusoma na kufuata nyayo za Brown tangu walipofahamiana na Blair wakiwa wabunge miaka ya 80 na hatimaye madaraka ya juu ya taifa hilo kubwa duniani.
Hili ni somo kubwa kwa Lowassa kwamba Brown aliweka rekodi ya usafi, uaminifu na utendaji uliotukuka. Amemaliza kazi ya waziri wa fedha sarafu ya nchi hiyo, pauni, ikiwa ni fedha yenye nguvu kuliko sarafu zote za nchi za Magharibi. Hii ni kazi iliyotukuka.