Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mbowe: Tunatawaliwa na wakoloni weusi
Mbowe: Tunatawaliwa na wakoloni weusi
By Habari Tanzania | Published  07/4/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mobini Sarya, Bukoba


VIONGOZI wa vyama vinne vikuu vya upinzani wamehitimisha ziara yao ya siku 16 mikoani kwa kutoa hotuba nzito ambazo zinaweza kuliweka taifa katika mwelekeo tofauti kabisa miaka michache ijayo.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ambaye ni mmoja wa viongozi hao amesema ukombozi wa kweli wa taifa unaweza kuja si kwa silaha bali kwa kuwahamasisha wananchi kujikomboa kutoka katika makucha ya watawala na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi.

Katika hali inayoweza kuzusha maswali mengi, Mbowe aliwaelezea viongozi wa sasa kuwa ni wakoloni weusi ambao madhira ya uongozi wao ni mabaya kuliko ya wakoloni weupe walioondolewa zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Mbowe alitoa kauli hiyo nzito wakati yeye na viongozi wenzake watatu wa upinzani walipokuwa wakihutubia umati wa wakazi wa Bukoba na vitongoji vyake waliohudhuria mkutano wa viongozi hao kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini hapa.

“Tumezoea kuchekeana lakini ipo siku tutafanyiana kweli hadi kieleweke. Tuko tayari kwa mapambano na wakati wowote wake zetu wanaweza kuwa wajane, hii yote ni kuhakikisha mapenzi yetu na nia njema kwa Tanzania inakamilika na kuona Watanzania wa vijijini wanaishi kitajiri,” alisema Mbowe.

Alisema, serikali ya sasa chini ya CCM imeshindwa kulinda na kusaidia wananchi na kutoa mfano wa Mkoa wa Kagera kuwa mchana watawala wa CCM wanakuwa kazini na usiku majambazi yanashika nafasi yao na kuwaondolea amani wakazi hao.

Akifafanua kauli hiyo, mwenyekiti huyo wa Chadema, alisema katika pori la Biharamulo majambazi yamejikita na serikali imeshindwa kupeleka askari kutokana na ukosefu wa vifaa madhubuti vya kupambana na majambazi.

“Tunawachukia bure polisi wetu kwa sababu wanamnyanyasa Lwakatare, lakini wanafanya kazi katika mzingira magumu…tunaitaka serikali kuwapatia japo ‘bullet proof’ (fulana za kujikinga na risasi) wakati wa kukabiliana na majambazi,” alisisitiza Mbowe ambaye alimalizia kwa kusema serikali imekuwa ikienda likizo usiku.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema mwaka 2010 wapinzani hawataingia katika uchaguzi mkuu iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya katiba.

Alisema ingawa si lengo la wapinzani kususia uchaguzi huo, lakini bila kufanyika kwa marekebisho ya katiba yatakayoruhusu kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi, wananchi wasitarajie mabadiliko ya msingi.

“Hatuwezi kususia uchaguzi huo lakini bila tume huru na katiba mpya hakuna uchaguzi mkuu mwaka 2010…tunaiambia serikali mapema ijue hilo,” alisisitiza Lipumba na kuongeza kwamba, “Tunahitaji serikali inayowajali wananchi wake, tunataka tume huru ya uchaguzi na katiba iliyoboreshwa,” alisema.

Kuhusu suala la kuibwa kwa kura wakati wa uchaguzi, Profesa Lipumba alisema, hakuna demokrasia ya kweli, hali inayosababisha kutokea kwa wizi wa kura.

Awali Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, aliwaeleza wananchi wa Bandari ya Kemondo, kuwa siri ya vyama hivyo kuunganisha nguvu zao pamoja ni sehemu ya mkakati wa kuiangusha CCM, na kuwaomba wawe tayari kumuunga mkono mgombea mmoja atakayeteuliwa kutoka kambi hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alihitimisha mkutano huo kwa kuwataka wananchi waungane na kuondoa tofauti za kiitikadi ili kuiangusha CCM, kwa kuwa imeshindwa kuandaa mkakati wa maendeleo ya taifa na kuishia kuwabebesha mzigo wa kodi wananchi, hali inayowalazimu wengi wao kutoka kwenye umaskini na kuwa fukara zaidi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.