Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kingunge ayakanyaga makombora ya CUF
Kingunge ayakanyaga makombora ya CUF
By Habari Tanzania | Published  07/4/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Peter Nyanje, Dodoma


WAZIRI wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Siasa na Mahusiano ya Jamii, Kingunge Ngombale-Mwiru, ameleeza kushangazwa na hatua ya wapinzani ya kutaka kuharakishwa kwa mazungumzo ya kutafuta muafaka wa kisiasa wa Zanzibar.

Kingunge alitoa tamko hilo jana wakati akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2007/08, iliyowasilishwa bungeni juzi jioni na waziri mwenye dhamana hiyo, Hawa Ghasia.

Akizungumza katika hali ya utulivu, Kingunge, mmoja wa wanasiasa wakongwe na mabingwa wa propaganda za CCM, alisema Rais Jakaya Kikwete bado anayo dhamira ya kweli ya kuhakikisha kuwa mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar unapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kingunge ambaye pia ni mjumbe katika Kamati ya Makatibu wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) inayotafuta suluhu ya mpasuko huo, alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu hotuba ya wapinzani iliyosomwa na Waziri Kivuli katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Shoka Khamis Juma (Micheweni-CUF).

Shoka katika hotuba yake hiyo alieleza kushangazwa na maendeleo yasiyoridhisha katika mazungumzo hayo, hali aliyoielezea kuwa inayoweza kuleta balaa visiwani, iwapo hatua za kurekebisha mambo hazitachukuliwa mapema.

Akijibu hilo, Kingunge alishangaa kusikia kipindi cha kati ya Februari mwaka huu na sasa ukionekana kuwa ni muda mrefu na akasema huenda CUF waliingia katika mazungumzo wakiwa wameshajipangia muda wa kupata ufumbuzi.

“Hivi wao walikuwa wanategemea mazungumzo yaishe lini?

Haya yanatafuta ufumbuzi wa kudumu. Wao walikuwa wanapanga muda… katika mambo haya nadhani watu wakubali ukweli,” alisema Kingunge na kuongeza kuwa, anavyoelewa yeye mazungumzo yanaendelea vizuri.

Aliliambia Bunge kuwa, wao ndani ya CCM walikuwa wameshakubaliana haja ya lazima ya kutafuta muafaka wa kudumu wa kisiasa wa Zanzibar.

“Sote tunajua kuwa mpasuko wa Zanzibar ni hali iliyokuwapo muda mrefu. Kutokana na jitihada zake uongozi wa CCM umekubaliana suala hili lipatiwe ufumbuzi,” alisema.

Pasipo kuingia kwa undani, mwanasiasa huyo alisema, uamuzi wa wapinzani kuanza kutoa maneno ya kutaka mazungumzo ya kutafuta muafaka yafanyike kwa haraka unaonyesha kuwa huenda iko ajenda nyingine nje ya ile ya kutaka ufumbuzi wa kweli.

“Subira ni suala la msingi… wanaodhani wanaweza kulipua katika matatizo ya msingi ya jamii wangefikiri mara mbili. Kama wanataka ufumbuzi wa kudumu, au wana lao jambo wanalolitaka,” alionya Kingunge.

Mbali ya hilo, Kingunge alitetea uamuzi wa Kikwete kuvaa kofia zake zote mbili nyakati zote anapokuwa ama kwenye shughuli za kiserikali, kichama au wakati anahutubia mikutano ya hadhara.

“Sijui kinachotafutwa ni nini, kwa sababu huyu (Kikwete) ni rais kamili. Hata anapokuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya CCM, havui kofia ya urais. Lakini vile vile anapokuwa Ikulu, huwa haachi kuwa mwenyekiti wa CCM.

“Sasa anapokuwa kwenye mikutano ya hadhara avue kofia vipi? Na huo utaratibu wa kuvua kofia ukoje? Haya yanafanyika wapi? Wanasema aache siasa! Urais ni siasa tupu… atawezaje kuacha siasa? Au katika ile maana ya kejeli ya siasa?” alihoji Kingunge.

Alisema kuwa iwapo wapinzani wanafanya kejeli, upande wa CCM wanafanya siasa kwelikweli kushughulikia mwenendo wa utawala wa nchi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.