Na Dunstan Bahai, Dodoma
MBUNGE wa Mufindi Kusini (CCM), Benito Malangalila jana alijikuta na wakati mgumu baada ya kutoa tuhuma nzito kwamba mmiliki wa Kampuni ya SPM Mgololo ameiweka serikali mkononi akiwemo Waziri Mkuu Edward Lowassa.
Tuhuma hizo nzito alizitoa wakati akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kutokana na tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama aliyekuwa akiongoza bunge alimtaka mbunge huyo kutoa ushahidi dhidi ya kauli yake nzito.
Mbunge huyo ambaye alipewa wiki moja kuwasilisha ushahidi huo, aliliarifu bunge kuwa anatoa hoja hiyo na Mwenyekiti huyo alimsamehe na kutakiwa kuendelea na mchango wake.
Awali, mbunge huyo aliliambia bunge kwamba kuwa mmiliki huyo aliyemwita kwa jina la 'mhindi' ni mbaguzi na kwamba anafikia kuwaita watu weusi kuwa ni mbwa huku akijigamba kuwa serikali yote ameiweka mfukoni akiwemo Waziri Mkuu.
"Hata wewe waziri mkuu, Edward Lowassa umewekwa mfukoni," alisema na kumfanya waziri mkuu kutingisha kichwa kuashiria hakubaliani naye.
Waziri Mkuu alipokuwa akitikisa kichwa kuashiria ni uongo unaozungumza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Masuala ya Bunge), Juma Akukweti alisimama na kumwomba Mwenyekiti, Mhagama kumtaka Malangalila kutoa ushahidi wa tuhuma zake.
Hata hivyo, alipotakiwa kufanya hivyo alisema anao na atautoa, lakini Akukweti aliposimama tena na kumwomba Mwenyekiti ampe muda mbunge huyo wa kuwasilisha ushahidi wake kwa spika ambapo mwenyekiti wa bunge alifanya hivyo na kumpa muda wa siku saba.
Lakini Malangalila alisimama na kusema kuwa, ingawa anachozungumza kina ukweli ndani yake, lakini muda aliopewa kuwasilisha ushahidi huo ni mdogo na hivyo anafuta kauli yake. Alikubaliwa na mwenyekiti na kuendelea kuchangia kwa kuunga mkono hoja.