RAIS Jakaya Kikwete jana alilazimika kuingilia kati na kuwataka walinzi wake waache kuwabughudhi wapiga picha ambao walikwenda kutekeleza majukumu yao katika mapokezi ya Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza.
Rais alichukua hatua hiyo baada ya kushuhudia wapiga picha wakisukumwa na kutakiwa kusimama mbali na eneo la tukio jambo ambalo lingewafanya washindwe kupata picha nzuri za mapokezi ya kiongozi huyo wa Msumbiji.
Rais Kikwete ambaye alikuwa akifutilia tukio hilo kwa muda, wakati anasubiri mwenyeji wake ateremke katika ndege iliyomleta, aliwaamuru maofisa hao waache kufanya hivyo lakini mmoja kati yao hakuonekana kuelewa.
“Wee njoo hapa.....” alimuita ofisa aliyekuwa anaongoza operesheni hiyo na kumuuliza kwanini anawazuia wapiga picha kufanya kazi yao.
“Acha watu wafanyekazi yao, kwanini unawazuia?” alihoji Rais na kumfanya ofisa huyo na walinzi wake wengine kujiweka pembeni na kuwaacha wapiga picha watekeleze wajibu wao.
Hali hiyo ilionekana kuwapa faraja wapiga picha ambao walisema kwa nyakati tofauti kuwa maofisa hao wamekuwa na tabia ya kuwasukuma bila sababu za msingi na wakati mwingine kuhatarisha vitendea kazi vyao.
Rais Guebuza akiwa nchini atakutana na wanajamii wa Msumbiji waliopo nchini kabla ya kufungua Maonyesho ya 31 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam na jana alikuwa na mazungumzo na mwenyeji wake.
Rais Kikwete aliwasili uwanja wa ndege akitokea nchini Ghana na kumsubiri mgeni wake, na waliondoka wote hadi Ikulu.