NCHINI Kenya, mwaka jana Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo (KCB), Andrew Mullei, alishutumiwa kumtumia mtoto wake, Silla Mullei, kufanya kazi ndogo ya kitaalamu ya Benki Kuu.
Mtoto huyu alilipwa takriban dola za Marekani 30,000 tu na zilitosha baba yake kusimamishwa na kuchunguzwa na hatimaye kushitakiwa. Hata hivyo, mahakama haikumkuta na hatia.
Pamoja na kwamba Rais wa Kenya Mwai Kibaki si msafi kutokana na sakata la Anglo Leasing, ambapo yeye na maswahiba zake wamehusishwa, kuondoa hasira za umma na kupunguza madhambi yake, alimwajibisha haraka Mullei bila ya kujali alikuwa rafiki yake. Maana kesi yake ilikuwa wazi mno.
Hapa kwetu Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Balali, anangoja nini kuachia ngazi kwa tuhuma zinazomkabili?
Si siri kuwa Balali pamoja na kulindwa yupo msambweni.
Hii ni kutokana na kugundulika kwa kashfa kuu mbili zinazomhusisha yeye, mkewe na washirika wake wanaojulikana kwa majina.
Kashfa ya kwanza ni ya ujenzi wa minara miwili ghali sana kuliko minara yote katika ardhi ya bara hili hata dunia nzima.
Ya pili ni kushirikiana na baadhi ya viongozi na wafanyabiashara wezi kuitapeli benki hii ya wananchi.
Kutokana na majadiliano makali bungeni, mambo fulani yameishajibainisha. Nayo ni kwamba kumbe kuna Watanzania ambao huwezi kuwadhania kuwa wanaweza kwenda benki wakakopa mabilioni na kuitumia Benki Kuu halafu baada ya muda deni linalipwa na benki kuu wao wanaendelea kutanua.
Sakata hili limemhusisha Mbunge wa Kwela (CCM) Chrisant Mzindakaya. Kimsingi wachambuzi wengi hata wabunge wanashinikiza Gavana wa Benki Kuu (BoT), ajiuzulu haraka ili achunguzwe na kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja.
Na hili ni jambo sahihi kama watawala wetu watatumia uadilifu badala ya kuangaliana sura. Maana wakati wao wanalindana na kusafishana, kuna maelfu na mamilioni yanateketea kwa kukosa huduma muhimu tena za bei nafuu.
Na Balali hata swahiba wake Mzindakaya wasingoje Kikwete awakingie kifua kwa vile ameweza kumkingia Mkapa kifua kwa muda.
Inabidi wasifanye kosa kudhani kuwa na wao atawakingia kifua. Inatisha kukuta kuwa kumbe hata mbunge anaweza kushiriki vitendo vichafu kama hivi na bado akajidanganya kuwa anabakia kuwa mwakilishi wa umma. Ni aibu hata kwa nchi.
Hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete alikaribishwa kwenye miradi itokanayo na pesa ya mazabe. Lazima hili limtie hasira rais na kuwashughulikia wahusika isije kuchukuliwa kuwa ana masilahi katika uchafu huu.
Maana ukiangalia sababu zilizomfanya amkingie kifua Rais mstaafu Benjamin Mkapa zaweza kuwa mosi, huenda walikubaliana walindane kutokana na Kikwete kuwa katika serikali ya Mkapa ambayo inasifika kwa kuiingiza nchi yetu kwenye mabalaa mengi hasa kwenye uwekezaji.
Pia, Mkapa hakuwa tena kwenye ofisi ya umma. Hivyo ilikuwa rahisi kumkingia kifua na kumficha kama alivyopotea ukiachia mbali kuwa Rais mstaafu, cheo ambacho miaka minane ijayo atakuwa nacho Kikwete.
Na cha mno hata kama sera za CCM ni kulindana, na hii ya Balali na mkewe imezidi kipimo, ukichukulia kuwa aliajiriwa na Benki Kuu kama mtaalamu na si mwanasiasa.
Pia kiwango cha fedha anachoshutumiwa nacho ni kikubwa mno kiasi cha kutohitaji kinga wala utetezi wa mtu yeyote hata awe rais. Maana Kikwete akimtetea au kutomuwajibisha, umma utaanza kumshughulikia yeye kwani kwa nchi maskini kama yetu dola milioni zaidi ya mia ni pesa nyingi mno.
Kwa hiyo kwa kitendo cha Balali kushirikiana na mkewe chini ya kampuni zao binafsi, kina madhara makubwa sana kwa kazi yake na uadilifu wake.
Maana kisheria mke na mume ni kitu kimoja. Hivyo masilahi ya mke wa Balali ni ya Balali na ya Balali ni ya Anna Muganda.
Na isitoshe kwa kuwajibika atakuwa angalau amepunguza hasira za wananchi. Kwani kama watalazimika kumshinikiza, atawapandisha hasira zaidi kiasi cha kuwa na madhara makubwa.
Na asijidanganye kuwa anaweza kunusurika. Arejee yaliyowakuta viongozi waliotaka kubadili katiba Zanzibar.
Kama serikali yetu haitaacha tabia yake ya kupuuzia mambo, Balali hata Mzindakaya inabidi waachie nafasi zao ili wachunguzwe.
Tena wafanye hivyo haraka sana iwezekanavyo. Ningeshauri wafanye hivyo hata kabla ya kikao kinachoendelea cha Bunge kwisha. Wameishiwa udhu wa kuaminiwa na jamii.
Pia kufanya hivyo kutawasaidia kusimama mbele ya vyombo vya sheria na kusafisha majina yao. Maana bado wanafaidi presumption of innocence chini ya sheria ya mwenendo wa jinai ya Tanzania na kanuni za haki asilia (Natural justice).
Na Balali hayuko peke yake. Upo msururu wa wafanyabiashara matapeli kibao nyuma yake. Kama serikali itafaya kazi kama serikali kwa kutumia mkono wake mrefu wahusika wote ilibidi wakamatwe na kushitakiwa hata kufililisiwa mali zao maana ni za umma.
Na adhabu kubwa ingetolewa ili liwe somo kwa watu wanaotumia vibaya nafasi walizoaminiwa na umma.
Kwanza serikali na kina Balali inabidi wafahamishwe kuwa Watanzania wanajua kila kitu.
Wanajua ni kwa kiasi gani sasa wafanyabiashara matapeli wa Kihindi wamegeuka kuwa adui mkubwa kwao.
Maana kila uchafu wa wizi lazima kuna Wahindi. Hii itafanya tuwachukie sana. Na kuwachukia huko si uchonganishi wala ubaguzi.
Anayehoji ithibati ya ukweli huu arejee jinsi Mchungaji Christopher Mtikila alivyofanikiwa kuushawishi umma kiasi cha kutaka kuwatoa roho.
Lakini watawala hawataki kukubali kuwa chuki hii ipo na inatokota. Mwenye kuficha maradhi kilio kitamfichua. Tusingoje tufikie hapo si pazuri.
Pia tukio la hivi karibuni katika nchi ya jirani ya Uganda ambapo Mhindi mmoja aliuawa na mali nyingi kuharibiwa, laweza kuwa somo tosha kwa wale wanaodhani kufumbia macho na kudanganya badala ya kutatua matatizo ni njia sahihi.
Isitoshe hata kama hasemi, rais naye atakuwa amechoka kudhaniwa kuwa anatumia cheo na ofisi yake kama kichaka cha kila aina ya uhalifu.
Kwa vile tuhuma za Balali , Mkewe na wenzake zinahusiana moja kwa moja na harakati za kukwamisha juhudi na ahadi za Rais Kikwete kuboresha uchumi na hatimaye kuwaletea wananchi maisha bora, naamini hatamkingia kifua wala kusita kumuwajibisha angalau afungue ukurasa mpya kuwa sasa anaanza kuonyesha njia.
Hitimisho, Balali na wenzako pisha wenye moyo, taaluma na mapenzi na nchi yetu watutumikie badala ya nyinyi kututumia. inatia aibu na ni hatari.
mpayukaji@yahoo.com