MSIMAMO ulioonyeshwa na wabunge kuhusiana na posho za madiwani, umeilazimisha serikali kuangalia uwezekano wa kurejesha baadhi ya kodi zilizofutwa.
Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliliambia Bunge jana kuwa serikali inaangalia uwezekano wa kuziruhusu halmashauri zitoze kodi za aina gani ambazo zilishafutwa hapo awali, kama njia ya kuwaongezea mapato na kuwapa uwezo wa kuwalipa madiwani wake.
Alisema Serikali Kuu haiwezi kulipa posho hizo kama ilivyopendekezwa na wabunge kwa sababu kufanya hivyo kutazipunguzia halmashauri uhuru wake.
“Ili kuhakikisha kuwa waheshimiwa madiwani wanawajibika kwa wananchi na halmashauri zao na kuimarisha dhana ya kupeleka madaraka kwa wananchi, serikali inasisitiza kuwa posho hizo zitokane na mapato yanayotokana na vyanzo vinavyokusanywa na halmashauri zenyewe,” alisema Lowassa.
Alibainisha hivi sasa, serikali inaangalia na kuchambua vyanzo vya mapato vya serikali kwa madhumuni ya kuzongezea halmashauri vyanzo vya mapato zaidi ili ziweze kutoa huduma bora na kumudu gharama za uendeshaji.
Aliainisha viwango vya posho wanazostahili kulipwa madiwani kuwa ni posho ya mwezi (sh 60,000), posho ya kikao (sh 40,000), posho ya madaraka kwa wenyeviti wa kamati (sh 40,000) kwa mwezi na posho ya madaraka kwa mwenyekiti au meya wa halmashauri (kati ya sh 100,000 hadi sh 350,000).
Wabunge wengi waliochangia hoja hiyo, walionyesha kusikitishwa na ongezeko la posho ya madiwani kutoka sh 30,000 hadi sh 60,000 na kudai kuwa bado ni kidogo kulingana na majukumu ya wawakilishi hao.
Aidha, wabunge walionyesha masikitiko yao dhidi ya hatua ya serikali kuzitaka halmashauri kuwalipa madiwani kulingana na uwezo wao.
Walidai halmashauri nyingi hazina uwezo, hivyo kuwataka kuwalipa madiwani hao ni kuwaongezea mzigo ambao hawawezi kuubeba.
Wakati huo huo, serikali imeikabidhi Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kazi ya kukusanya kodi za majengo baada ya kubaini kuwa halmashauri nyingi zimeshindwa kukusanya kodi hiyo kwa ufanisi.
Ripoti nyingi zimeonyesha kuwa iwapo kodi ya majengo ingekusanywa kikamilifu, ingezipatia halmashauri uwezo mkubwa wa kugharamia mahitaji yake bila kuhitaji msaada mkubwa kutoka vyanzo vingine.
Akitangaza maamuzi hayo jana, Lowassa alisema baada ya kukusanya fedha hizo, TRA itazirudisha kwa halmashauri ambao watazitumia katika utekelezaji wa mipango yao.