BAADHI ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wamemlaumu Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, kwa kushindwa kusimamia kazi zake ipasavyo na kuonyesha woga kwa watendaji walio chini yake.
Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi ya makadirio na mapato ya matumizi ya mwaka wa fedha wa 2007/2008, Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma (CCM), alisema inaonekana wazi kwamba, Waziri Kiongozi amekuwa akionyesha hofu kwa watendaji wake hasa katika kusimamia kazi za maendeleo ikiwemo ujenzi wa bararaba.
Alisema Waziri Kiongozi amekuwa akionyesha woga kwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Brigedia mstaafu Adam Mwakanjuki.
“Mheshimiwa Spika, nasema hivyo si kwa utani, tulitegemea mawaziri hawa washirikiane pale ambapo kuna kero ya wananchi.
“Naangalia Televisheni ya Taifa, Waziri Mkuu ni mtu ambaye ni very hard worker, lakini waheshimiwa wetu inaonyesha Waziri wa Mawasiliano wanamuogopa, lazima tuzungumze ukweli, anatisha Mheshimiwa Spika, kwa sababu Waziri Kiongozi sisi tumeshazungumza tokea mwaka jana kwamba barabara hizi ni mbovu,” alisema mwakilishi huyo.
Nahodha alishauriwa kutumia nguvu ya mawaziri wenzake akiwemo Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, aliyeteuliwa hivi karibuni, Machano Othman Said, kumkabili Mwakanjuki.
“Waziri Kiongozi akijipima, akimtizama Waziri wa Mawasiliano anaona nikienda kule itakuwa mtihani. Leo pana mawaziri viongozi watatu, basi mvamieni, hizi ziro ziro hatuzitaki,” alisema mwakilishi huyo.
Alisema Zanzibar kuna barabara 19 ambapo barabara moja pekee ndiyo iliyofikia asilimia 10, ambayo ni Paje –Pingwe urefu wa kilomita 16.6, kiwango cha lami ni asilimia 10, kifusi ni asilimia 16.
Alisema Waziri Kiongozi amekuwa akimsifu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi lakini kazi iliyofanyika haionekani, hivyo lazima jitihada zichukuliwe.
Mwakilishi huyo alisema katika ujenzi wa barabara ya Mazizini-Fumba kilomita 17.8m kiwango cha lami 0, kiwango cha kifusi 0, barabara ya Mfenesini- Bumbwini urefu wa kilomita 13.2, kiwango cha lami 0, kiwango cha kifusi 0.
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni ile ya Welezo- Dunga kilomita 12.7. Kiwango cha lami 0 na kiwango cha kifusi 0. Licha ya kazi yote hiyo ilivyokuwa ziro lakini waziri huyo husifiwa kwa kazi nzuri.
Alisema Kampuni ya PRISMO ilikuwa ikijenga barabara ya Mkoani Pemba na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliwahi kusema kwamba, kampuni hiyo haifai, lakini Waziri wa Mawasiliano aliitetea na kusema kuwa matatizo ni mvua nyingi na milima, huku akitoa sababu za uchambuzi yakinifu.