Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mafuta, nauli zapanda
Mafuta, nauli zapanda
By Habari Tanzania | Published  07/3/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Ratifa Baranyikwa


IKIWA leo ni siku ya tatu tangu kuanza kwa mwaka mpya wa fedha wa 2007/08, machungu ya bajeti yanaonekana kuanza kupanda kidogo kidogo kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa za petroli na nauli za mabasi, Tanzania Daima imethibitisha.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili juzi na jana unaonyesha kupandishwa kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli kuanzisha kwa wasafirishaji wakubwa na kwenye vituo mbalimbali vya kuuzia mafuta.

Hali kama hiyo pia imejionyesha katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo cha jijini Dar es Salaam ambako mabasi kadhaa ya mikoani yalionekana yakipandisha bei ya nauli kwa wateja wake.

Kutokana na hali hiyo Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeeleza kushangazwa na hatua hiyo ya kupanda kwa nauli, wao wakiwa hawana taarifa.

Pamoja na kukiri kuwapo kwa taarifa hizo za nauli kupanda, maofisa wa juu wa SUMATRA walisema walikuwa hawajatoa kibali chochote cha watu kuanza kupandisha nauli.

Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam kutokana na kupanda kwa nauli za mikoani, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa SUMATRA, Haruna Songoro, alisema kuwa wamiliki wa mabasi yaliyopandisha nauli wamekiuka sheria ya leseni.

“Tungekuwa tumepata maombi ya kupandisha kwa nauli kutoka kwa wamiliki wao, sawa, na huwa tuna utaratibu wa kufanya majadiliano, lakini mpaka sasa hakuna ombi lolote lililowasilishwa, sasa wanaopandisha nauli hawa ni sawa na wahalifu sawa na wahalifu wa makosa mengine,” alisema.

Aidha, alilithibitishia gazeti hili kuwa, taarifa za kupanda kwa nauli wamezipata na wameshaanza uchunguzi wa suala hilo na watakaobainika hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kusimamishiwa kwa muda leseni zao au kufutiwa kabisa.

“Tumeshapeleka watu wetu kufuatilia, kwani hatuwezi kutoa maamuzi bila kuwa na uthibitisho, kwa sababu inawezekana aliyepandisha nauli si mmiliki, unaweza kukuta mfanyakazi tu ndiye aliyepandisha nauli na mmiliki hana taarifa.

“Inatupasa kufuatilia ili kubaini ukweli ili adhabu tutakayoitoa isiumize wale ambao hawakuhusika kwani si wote waliopandisha nauli,” alisema Songoro

Hali hiyo imekuja siku chache tu baada ya Bunge kupitisha bajeti kwa mwaka wa fedha 2007/08, ambayo pamoja na mambo mengine ilitangaza kuongezeka kwa ushuru kwenye mafuta ya petroli na dizeli.

Akihitimisha mjadala wa bajeti hivi karibuni, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alilieleza Bunge kwamba, mamlaka za umma hazitakuwa tayari kuona watu wakiongeza fedha za bidhaa na huduma kwa kisingizio cha bajeti kuongeza ushuru kwenye mafuta ya petroli.

Aidha, utafiti uliofanywa na Tanzania Daima katika vituo vya kukatia tiketi katika baadhi ya mabasi yaendayo mikoa ya Morogoro, Arusha, Kilimanjaro na Mbeya umebaini kuwa kuna ongezeko la nauli.

Kwa upande wa mabasi yaendayo Arusha, nauli imepanda kutoka sh 15, 000 hadi sh 17,000 kwa mabasi ya 'luxury', wakati Morogoro kwa sasa nauli ni sh 5,000 awali ilikuwa sh 3,000 na 4,000.

Wakati mabasi yaendayo Mbeya nauli imepanda kutoka sh 20,000 hadi sh 25,000, mabasi ya Moshi nauli kwa sasa ni sh 15,000 wakati nauli ya zamani ilikuwa ni sh 12,500.

Kwa upande wa mafuta ya dizeli bei zinaonekana kupanda kutoka sh 1,200 hadi kufikia sh 1,300 katika baadhi ya vituo, huku vituo vingine vikiuza kwa sh 1,400 kwa lita.

Kwa baadhi ya vituo vya mafuta bei ya petroli inaonekana kupanda kutoka sh 1,300 kwa lita moja hadi kufikia sh 1,400 katika baadhi ya vituo wakati vituo vingine vikiuza hadi sh 1,500.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.