Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa: Tuhuma BoT zinashitusha
Lowassa: Tuhuma BoT zinashitusha
By Habari Tanzania | Published  07/3/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Peter Nyanje, Dodoma


WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema serikali imeshtushwa na kusikitishwa na kuwapo kwa tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni ya fedha katika Benki Kuu (BoT).

Lowassa aliyasema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati alipokuwa akihitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2007/08.

Alilieleza Bunge kuwa, kutokana na hali hiyo ndiyo maana serikali iliamua kuchukua mara moja hatua za kulishughulikia suala hilo ambalo limekuwa moja ya ajenda kubwa tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti katikati ya mwezi uliopita.

Lowassa alisema uamuzi wa kumuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ashirikiane na wakaguzi wa mahesabu wa kimataifa, kuchunguza tuhuma hizo ni matokeo ya msimamo huo wa serikali.

“Tumewataka wachunguze kubaini kama tuhuma hizo ni kweli, nani anahusika na wapendekeze hatua za kuchukua,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, alisema kuwa, serikali imekubaliana na washirika wa maendeleo kuhusiana na hatua zinazochukuliwa na kuwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, ripoti yake italetwa bungeni.

Lowassa alitumia fursa hiyo kuwasihi wabunge wa upinzani, akiwataja kwa majina, Hamad Rashid Mohamed na Dk. Willibrod Slaa, kuachana na hoja ya kutaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge itakayochunguza tuhuma hizo.

“Nawasihi sana wenzangu wa upinzani, jambo hili halihitaji kamati teule ya Bunge kwa sababu kuna taratibu tunazifuata… tuliache, tutalishughulikia na kutoa taarifa bungeni,” alisema Lowassa.

Lowassa aliwataka wabunge kuelewa uzito wa suala hilo akisisitiza kuwa BoT ni roho ya nchi, kama ilivyopata kusisitizwa na Slaa.

“BoT si chombo hivi hivi… hizi tuhuma, sijui, sina uhakika na yanayozungumzwa, lakini BoT ni moja ya Benki Kuu zinazokubalika Afrika. Ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi…inachangia sana uchumi… mle ndani kuna vijana wa Kitanzania wanaofanya kazi vizuri, si vema tukawajumuisha wote na kuwashushia tuhuma,” alisema.

Slaa ambaye ndiye Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyeibua hoja hiyo bungeni, aliliambia gazeti hili nje ya Bunge jana kuwa, alikuwa ameridhishwa na hatua ya serikali kuonyesha kuguswa na tuhuma hizo nzito.

“Wapinzani tumefarijika na kauli hii ambayo ni tofauti na ile iliyowahi kutolewa na mawaziri wengine huko nyuma. Ile concern (kujali) iliyoonyeshwa na serikali inatia moyo,” Dk. Slaa aliliambia gazeti hili mara baada ya Lowassa kumaliza kuhitimisha hoja yake majira ya saa 7:15 mchana.

Hata hivyo, katika maoni yake, Dk. Slaa alisema kuwa pamoja na hatua hiyo ya serikali, bado kuna haja ya kufanya mambo mengine zaidi ili kambi ya upinzani iwe na uhakika kuwa hatua zinazochukuliwa zitazaa matunda yanayotarajiwa.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kikubwa kinachotakiwa ni kuhakikisha kuwa, ripoti ya uchunguzi huo inawasilishwa bungeni, ili wananchi wapate kufahamu kilichotokea kupitia kwa wabunge wao.

Alisema kuwa pamoja na hayo, ni vema serikali ikaweka wazi wigo wa upelelezi utakaofanywa kwani kumekuwa na tuhuma za aina nyingi, zote zikiikabili BoT na baadhi ya watendaji wake.

“Hatuna uhakika iwapo uchunguzi huu wa serikali utahusisha akaunti ya madeni ya nje peke yake au la.

Tunavyofahamu kuna madai mengi sana na kiwango cha ubadhirifu ni kikubwa… tutataka kupata uhakika wa hilo,” alisema.

Hata hivyo wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Matumizi, Hamad Rashid alisimama na akaeleza kutoridhishwa na uamuzi wa serikali kupinga kuanzishwa kwa kamati teule ya Bunge.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.