MAENEO mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam jana yaligeuka uwanja wa vita baada ya zoezi la kuondoa wapiga debe kuanza kutekelezwa na uongozi wa jiji.
Zoezi ambalo lilianza kutekelezwa katika maeneo mbalimbali, lilishuhudia kamata kamata ya wapiga debe hao iliyokuwa ikiendeshwa na askari wa Halmashauri ya Jiji huku wakiwa na silaha mbalimbali kwa ajili ya kupambana na wapiga debe.
Hali ilionekana kuwa mbaya zaidi katika eneo la Manzese, ambako zoezi hilo lilianzia, kwa askari wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa Manispaa ya Kinondoni kukamata kijana yeyote aliyehisiwa kufanya kazi hiyo.
Baadhi ya wapiga debe wengine walionekana wakiendelea kupiga debe huku wakiwa wanakimbia huku na kule, ili kuweza kuwakwepa askari hao, ambao walikuwa wamejazana katika vituo mbalimbali vya daladala jijini.
Katika kituo cha Ubungo, askari walikuwa wamejazana huku wakiendelea kupigana vita na baadhi ya wapiga debe ambao walionekana kukiuka agizo hilo.
Wengi wao walikuwepo kandokando ya barabara huku wakionekana kuendelea kuita abiria kinyemela kitu ambacho askari walikigundua na kuwakamata.
Katika kamata kamata hiyo, magari ya askari yalionekana yakizunguka huku na kule katika kila kituo na kuwakamata wapiga debe hao na kuwaingiza ndani na magari hayo.
Kwa hali ambayo si ya kawaida kila gari lililokuwa likipita barabarani lilionekana limewajaza wapiga debe huku wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi wenye silaha.
Vurugu nyingine ilitokea eneo la Manzese pale askari walipomkamata mtu mmoja ambaye alikuwa ni abiria, wakidhani ni mpiga debe kitu ambacho kilizua fujo.
Baada ya kukamatwa kwa mtu huyo ambaye hakuweza kutambulika jina lake mara moja, baadhi ya wananchi ambao walikuwepo karibu na eneo la tukio, waliingilia kati na kuwaambia polisi mtu huyu si mpiga debe bali ni abiria.
Purukushani hiyo ya polisi na wananchi, iliendelea huku wananchi hao wakipiga kelele wakisema wamwachie raia huyo ambaye alikuwa hana hatia yoyote.
Polisi na mgambo wa jiji walipoona kelele za wanachi zimezidi, ilibidi wamwachie mtu huyo na kumshusha kwenye gari walilokuwa wamempandisha.
Hali ya kukimbizana na wapiga debe iliendelea katika vituo mbalimbali kama Kimara, Mwenge, Usalama, Magomeni Mapipa, huku polisi wakihakikisha wanatimiza zoezi hilo la kuwaondoa wapiga debe hao ambao wamekuwa kero kwa siku nyingi sasa kwa abiria.
Katika hatua nyingine, makondakta wa daladala wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima, waliipongeza serikali kwa kuwaondoa wapiga debe hao ambao wamekuwa na usumbufu mkubwa kwa muda mrefu.
“Sisi tunatoa pongezi kubwa kwa mkuu wetu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro kwa kuweza kuwaondosha wapiga debe, kwani walikuwa wanatusumbua kwa muda mrefu kwa kutudai pesa, hivyo trumefurahi sana,” alisema mmoja wa makondakta ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Naye dereva aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamisi, alisema kwamba serikali imeweza kuona tatizo hilo na kulifanyia kazi hivyo sasa wataweza kufanya kazi zao kwa ufanisi wa hali ya juu bila ya kusumbuliwa na wapiga debe.
Nao baadhi ya wananchi waliipongeza serikali kwa zoezi hilo la kuwaondosha wapiga debe hao wakidai ya kuwa walikuwa ni kero kubwa pindi wanapofika kituoni kwa kuwasumbua abiria na hata kuwaibia simu zao.