Asema dawa dhidi yao iko jikoni inachemka
Awataka waanze kutafuta shughuli ya nyingine
Na Noor Shija
MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema baada ya kuwadhibiti majambazi, sasa linakuja fagio dhidi ya vibaka ambao dawa yao inachemka.
“…Tatizo la ujambazi tulisema hatutawaacha watambe, tunajua hawajaisha, lakini mzizi wa fitina tutaung’oa kwa kushirikiana na nchi jirani.
“Tukimaliza hili kubwa tutaingia kwa vibaka wanaowanyima raha wanawake wasipendeze, dawa iko jikoni. Tafuteni shughuli nyingine ya kufanya,” alisema hayo jana Mwenyekiti Kikwete alipokuwa akiwasalimia wananchi na wana-CCM wa mkoa wa Dar es Salaam.
Amewataka vibaka katika maeneo mbalimbali nchini watafute kazi nyingine kabla serikali haijaanza kushughulikia.
Mwenyekiti Kikwete alitoa salamu hizo kwenye sherehe za mapokezi yake zilizofanyika kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba mara baada ya kuwasili kutoka Dodoma ambako Mkutano Mkuu wa CCM ulimchagua kuwa Mwenyekiti wa CCM.
Katika uwanja wa ndege, Mwenyekiti Kikwete alipokelewa na Wazee wa CCM mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa Hemed Mkali.
Kikwete ambaye aliwasili kwa ndege ya serikali aina ya Fokker 50 alikuwa ameongozana na mkewe Mama Salma Kikwete, Katibu Mkuu, Luteni Yusuf Makamba, Naibu Katibu Mkuu (Bara) Kapteni mstaafu Jaka Mwambi na Katibu wa Itikadi na Uenezi Aggrey Mwanri.
Alisema kazi kubwa iliyo mbele ni kuimarisha Chama, kukuza uchumi na ulinzi na usalama wa wananchi na alifafanua kuwa uchumi, ulinzi na usalama ni mambo ambayo ya serikali imeamua kuyapa kipaumbele.
Mwenyekiti huyo wa CCm Kikwete alisema kazi hiyo wameianza kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya ambapo katika suala la uchumi hoja kubwa ni kuinua hali ya maisha ya Watanzania.
Alisema umasikini ni mateso na ndiyo maana serikali imetilia mkazo suala la kujiajiri ambapo juzi Waziri Mkuu Edward Lowassa alitangaza Bungeni kwamba serikali imetenga sh. milioni 500 kwa kila mkoa wa Tanzania Bara.
Rais Kikwete alisema fedha hizo ni kwa ajili uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kuongeza ajira nchini.
Alisema lengo la fedha hizo zitatolewa kila mwaka. “Hatutaingia kichwa kichwa, tunataka kuona kwanza hizi za mwaka huu zimefanya kazi vipi. Je, walengwa zimewafikia au zimeenda kwa wale wenye unafuu,” alifafanua Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kuwa mwakani wataangalia namna fedha hizo zilivyofanya kazi na kurekebisha makosa yaliyotokea.
Aliwaambia wananchi kwamba fedha hizo zikitumika vizuri zitanufaisha watu wengi zaidi na kwamba watakaopewa wazitumie kufanya shughuli walizoombea na pia wakumbuke kurejesha mikopo hiyo.
Alisema kuwa fedha hizo zitatolewa kupitia benki na wamelipwa kwa ajili ya shughuli. “Tumeziondoa mikononi mwa wanasiasa kwa kuwa hazitarejeshwa na hivyo zitatolewa kupitia benki kwa kuwa wao wanaweza kudai,” alisema.
Alisema mikopo kutokana na fedha hizo itatolewa na benki zilizokubaliana na serikali kwa masharti ambayo serikali yenyewe imeyaweka na siyo kwa masharti ya benki hizo.