Na John Stephen
HOJA zilizotolewa bungeni na Mbunge wa Karatu, Dk Wilbroad Slaa zinaonekana kuendelea kuisumbua serikali baada ya mawaziri wawili kuwasilisha hoja za kumpinga kabla ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa kutoa maelezo juu ya kauli ya Dk Slaa.
Hivi karibuni Dk Slaa aliwasilisha bungeni hoja zilizomhusisha Gavana wa Benki Kuu, Balali, Mkewe Anna Muganda na wafanyabiashara kwamba wanahusika na ubadhilifu wa fedha za benki hiyo.
Juzi akizungumzia suala hilo, Waziri wa Fedha, Zakia Megheji alisema vyombo vya dola vitatumika kuchunguza ubadhirifu huo.
Naye Waziri wa Nishati na Madini, Nazar Karamagi, jana aliwasilisha hoja bungeni kuwa maelezo ya ubadhilifu aliyoyatoa Dk Slaa hivi karibuni dhidi ya Gavana na watu wengine, yameisikitisha serikali na kwamba yalikuwa ni ya uongo.
Karamagi alisema; "Serikali imesikitishwa na taarifa potofu zilizotolewa na Dk Slaa kwani habari hizo zina lengo la kuwapotosha wananchi."
Akizungumzia kampuni ya Meremeta, Karamagi alisema taarifa kwamba mke wa Gavana ni Mkurugenzi wa Time Mining si za kweli na kwamba maelezo yake yalikuwa ni ya kubuni.
Karamagi alisema pia kampuni ya Merameta haijawahi kukodishwa na kampuni ya Time Mining wala kuuzwa.
Alisema kampuni ya Meremeta ilisimamisha shughuli zake kutokana na matatizo ya fedha na kwamba serikali iliingilia kati kwa lengo la kuunusuru mgodi wa Buhemba.
"Serikali iliunda Task Force ili kuunusuru mgodi wa Buhemba na si vinginevyo kama ilivyoelezwa awali," alisema Karamagi.
Kuhusina na mke wa Gavana kwamba ana hisa katika kampuni ya Rand Gold, Karamagi alisema kuwa hana hisa.
Kutokana na hoja za Dk. Slaa hadi sasa mawaziri wawili wamesimama bungeni na kuzungumzia hoja hizo kabla ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa kulizungumzia ubadhirifu huo Jumatatu wakatia anawafanay majumuisho ya michango ya wabunge.
Juni 25 mwaka huu, Slaa amezidi kumbana Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Daudi Balali na sasa ameomba mwongozo wa Katibu wa Bunge jinsi ya kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka Bunge liunde Kamati Teule ya kuchunguza ubadhirifu huo.
Hatua hiyo, imekuja siku moja baada ya Dk Slaa kumbana Mbunge wa Kwela, Dk
Christant Mzindakaya, ambaye alikiri kupokea mkopo wa fedha kutoka Standard
Chartered ambao baadaye deni lake lilihamishiwa Benki ya Rasilimali (TIB) kwa
udhamini wa serikali kupitia Wizara ya Fedha, ambayo ilitoa mwongozo kwa Benki Kuu
(BoT).
Taarifa ambazo Mwananchi imepata jana na pia kuona nakala yake zinasema mbunge huyo alitoa taarifa hiyo kwa kutumia kifungu cha 104 cha kanuni za Bunge toleo la mwaka 2004.
Kifungo hicho kinasema: (1) Kamati Teule yaweza kuundwa na Bunge kwa madhumuni maalum, kwa hoja mahsusi itakayotolewa kwa ajili hiyo na kuafikiwa.
(2) Kamati Teule yaweza pia kuundwa endapo baada ya Bunge kujadiliwa hoja fulani, litaamua kuepeleka jambo fulani linalotokana na hoja hiyo kwenye Kamati Teule, ambapo utaratibu wake utakuwa kama ifuatavyo:-
Mara tu baada ya hoja iliyokuwa ikajadiliwa kuamuliwa, Mbunge yeyote mwenye nia ya kutoa hoja chini ya Kanuni hii aweza kusimama mahali pake na kutoa taarifa ya mdomo kwamba anakusudia kuleta hoja ya kuundwa Kamati Teule.
Baada ya hapo, Mbunge huyo atatoa taarifa ya hoja yake kwa maandishi kwa Katibu, na hoja hiyo itashughulikiwa wakati unaofaa kwa kuzingatia Mpangilio wa Shughuli uliowekwa na Kanuni ya 23(4).
(3) Wajumbe wa Kamati Teule watateuliwa na Spika, na watachagua Mwenyekiti wa Kamati hiyo kutoka miongoni mwao.
Barua ya Dk Slaa kwa Katibu wa Bunge, inataja kusudio la Bunge kuunda Kamati Teule ya Kuchunguza Ubadhirifu mkubwa dhidi ya Gavana wa BoT, Daudi Balali.
Katika taarifa hiyo ya maombi, Dk Slaa alisema wakati akichangia hoja ya Waziri wa
Fedha aliwasilisha nyaraka muhimu zinazohusu ubadhirifu huo na pia aliziwasilisha
wakati akichangia hoja ya Waziri Mkuu.
"Nilieleza na kunukuu vianzio mbalimbali vya habari kuhusu ubadhirifu huo ndani ya
benki kuu yaani BoT, zinazoeleza kumhusisha moja kwa moja na Gavana wa Benki Kuu," inasema sehemu ya barua yake.
Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, Dk Slaa alisema, analiomba Bunge kuunda Kamati Teule ya Bunge kwa mujibu wa kanuni hiyo ya 104.
"Katika muda mfupi ujao nitawasilisha kwako hoja kamili kuhusu suala hili, natunguliza shukrani zangu, na naomba maelekezo kama yatakuwepo," inasema barua hiyo.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, akichangia hotuba ya Waziri Mkuu juzi jioni, alisema kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu inaonyesha ubadhirifu mkubwa wa trilioni 1.2 na kwamba wabunge wasiendelee kuwatazama tu bila kuchukua hatua.
"Hatuwezi kuendelea kuwatazama watu hawa hivi hivi tu. Hapa tunasikia minong�ono mingine ambayo inahusisha taasisi za umma na inakuwa mbaya zaidi zinapotajwa taasisi ambazo hazina yetu ya nchi nzima ipo na hiyo ni Benki Kuu ya Tanzania," alisema.
Alisema uamuzi wa kuundwa kamati teule kwa ajili ya kuchunguza madai ya ubadhirifu Benki Kuu haliwezi kukwepwa. " Hili linahitaji majibu, haliwezi kukwepwa, tutoe ufafanuzi wa kutosha na ikibidi kuwaridhisha Watanzania kwa kuunda Kamati Teule ya Bunge ili Watanzania waendelee kuwa na imani na sisi wenyewe.
Kuacha kufanya hivyo haitaonyesha au itatia mashaka dhamira yetu ya kupambana na wabadhirifu wa mali ya umma na mimi ningetaka katika hili tujielekeze huko," alisema Mbunge huyo.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Owenya alisema jana kwamba anaungana na wabunge wengine kuomba Kamati Teule iundwe ili kuangalia madai ya hujuma ndani ya BoT.