Na Patricia Kimelemeta
VYAMA vya siasa nchini vimeweka mkakati wa kuhakikisha vinaondoa na au kupunguza hisia za uzanzibari na upemba kama tiba ya hali ya kutokuelewana kisiasa visiwani Zanzibar.
Wakizungumza katika mkutano wa kuzungumzia hali ya siasa visiwani humo uliyofanyika jijini Dar es Salaam jana chini ya Taasisi ya TCD, wanasiasa hao walisema kuwa hatua hiyo ina lengo la kupunguza mivutano na kustawisha maelewano miongoni mwa wananchi visiwani humo.
Walisema kuwa hatua hiyo wanayoikusudia ina lengo la kuleta changamoto kubwa ya maendeleo na kuondoa hali ya kubaguana kati yao.
Mwakilishi kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Siasa, Juma Muchi alisema kuwa maamuzi wanayoyakusudia yanaweza kuzaa matunda na kuondoa tofauti zao.
�Nia safi ya vyama vyote yataweza kuleta mabadiliko ya kuondoa hali ya ukabila inayotuzunguka visiwani kwetu hasa ya upemba na uzanzibar ambao unaweza kutuletea matatizo makubwa siku za baadaye,� alisema Muchi.
Aliongeza kuwa Zanzibar wameweza kushuhudia machafuko ya vurugu kwa sababu ya hali hiyo, hivyo kama kikao hicho watazungumza na kutekeleza kama ilivyokusudiwa basi wanaweza kuliondoa suala hilo.
Muchi alisema kuwa ikiwa watazungumza suala la kuleta maendeleo basi hilo ni jukumu la wananchi wote kwa ujumla na sio la CUF wala CCM kwa hiyo wanachotakiwa ni kutetea maslahi ya wananchi na kujadiliana jinsi ya kuleta maendeleo kwa pamoja.
Naye Katibu Mwenezi kutoka Chama cha United Democratic Party (UDP), Isack Cheyo alisema kuwa ikiwa viongozi wa vyama vya siasa wataacha ubinafsi na uroho wa madaraka wakikaa pamoja na kujadili maendeleo ya demokrasia yatapatikana haraka.
�Sisi watu wa vyama vya siasa tukikaa pamoja na kuangalia matatizo yaliyopo na kuyatatua kwa pamoja, tunaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa malengo ambayo tumeyakusudia,� alisema Cheyo.
Hata hivyo Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa wa NCCR- Mageuzi, Dk Sengondo Mvungi alisema kuwa demokrasia inahitaji moyo safi unyenyekevu na uadilifu hivyo misingi ya kikao hicho ni kutumia katiba ambayo inaonyesha mambo yote ili kuleta usawa kati ya vyama vyote.
�Demokrasia ni uadilifu, hatutaki ufisadi ambao unafanywa na chama tawala kwa vyama vya siasa vilivyobaki hivyo tunataka ushirikiano uwepo kati ya vyama vyote, changamoto zilizotolewa zifanyiwe kazi kipitia vyama vyote na sio tugeukane baadaye,� alisema Mvungi.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Dk Hussein Mwinyi alisema wao watapitia maamuzi yote na kuyafanyia kazi kama kuna marekebisho watakaa pamoja na kurekebisha.